Archive for May 2009

RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE KUHUSU MWENZI WA MAISHA YAKO.

May 7, 2009

 Na: Sanga P.S.

Najua yumkini upo njia panda kwa habari ya kuoa au kuolewa. Si kwa sababu hakuna mtu wa kuoa au kukuoa, bali ni kwa sababu kila anayekuja ni tofauti kabisa na kile ambacho wewe unapenda na unafikiri pia ni mapenzi ya Mungu iwe utakavyo. Huenda kibinadamu kuna sifa/vigezo ambavyo ulijiwekea vya mtu ambaye ungependa kumuoa au kuolewa naye, lakini kila unapoomba unaona mtu anayekuja ni tofauti kabisa na vile ulivyotaka wewe. Na unapoomba zaidi kumhoji Mungu anakuhakikishia kwamba huyohuyo ndiye mtu wa mapenzi yake.

Hukuishia hapo umeshirikisha na wapendwa wenzako au hata watumishi wengine wameomba nao wamethibitisha huyo ndiye mtu wa mapenzi ya Mungu kwako. Kila unapojitahidi kufikiri kumwacha unakosa amani. Mimi ninakushauri inapofika mahali kama hapo we ruhusu tu mapenzi ya Mungu yatimie kwako. Zipo sababu nne za msingi  zinazonifanya nikushauri hivyo;

 • Mapenzi ya Mungu ndio utimilifu wa kusudi lake kukuleta wewe duniani.

Haukuja duniani kwa sababu ni kawaida ya wanadamu kuzaa, bali ni kwa sababu ni Mungu alikusudia wewe uzaliwe.Hii ina maana lipo kusudi la Mungu kukuleta duniani. Na ili kusudi lake liweze kufikiwa ni lazima ujifunze kuishi maisha ya mapenzi yake. Uishi ili kutimiza mapenzi yake hapa duniani.

Ni mapenzi ya Mungu pia kuhakikisha unaoa/kuolewa na mtu ambaye anajua mtasaidiana katika kutekeleza makusudi yake hapa duniani. Kwa hiyo si suala la kuoa au kuolewa unavyotaka, bali ni kuoa au kuolewa kwa mapenzi yake.

 • Mapenzi ya Mungu si lazima yakubaliane/yaendane na ya kwako.

Ni muhimu ujue kwamba mapenzi ya Mungu si lazima yaendane na ya kwako. Na hii ni kwa sababu mawazo yako si mawazo yake na njia zake si njia zako (Isaya 55:8). Jua kabisa mapenzi ya Mungu si lazima yakupendeze, yakufurahishe au yalinde heshima yako.

 • Kuna nyakati ambazo mapenzi ya Mungu kuyapokea ni machungu, yanaliza, yanafadhaisha, yanaogopesha.

Katika kuyakubali au kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie wakati mwingine     yanaweza kuwa machungu, kukufadhaisha, kukuliza, kukuumiza, kukuogopesha au hata kukuabisha kwa jinsi ya kibinadamu.

 • Mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake.

Ingawaje yanaumiza, kufadhaisha au hata kuaibisha kwa jinsi ya kibidamu /kiheshima/kimahusiano/kijamii /kiuchumi nk. Na hata kama  kwako yana athari kiasi gani uwe na uhakika mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake, hii ina maana HAYO NDIYO MAPENZI YAKE na si ya KWAKO. Tunapoomba kusema mapenzi yako (Mungu) yatimizwe ina maana mapenzi/matakwa ya kwetu (wanadamu) yasitimie.

Hebu tuangalie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

Mfano wa Yakobo Mwanzo 29:15-31.

Hii ni habari ya Yakobo alipokwenda Harani kwa Labani nduguye. Labani alikuwa na binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo aliitwa Raheli amabye alikuwa na uso na umbilie zuri. Raheli ndiye ambaye Yakobo alimpenda na alikubali kutumika kwa miaka saba ili apate kumuoa. Baada ya miaka saba, Yakobo alipewa Lea ambaye hakumpenda kama mke bali alimpenda Raheli. Ingawa zilipopita siku saba ndipo alipopewa na Raheli kama mke wa pili.

Nikuulize swali, je Yakobo angeambiwa atumike miaka saba kwa ajili ya kumpata Lea, angekubali? Je unafikiri ni kwa nini Mungu aliruhusu Yakobo  mtumishi wake kufanyiwa hili? Sababu kubwa ni hii, ilikuwa ni mpango/mapenzi ya Mungu Yakobo amuoe na Lea pia. Hii ni kwa sababu ya umuhimu wa watoto aliowazaa ukihusianisha na uzao/ukoo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Namaanisha kupitia Lea, Yakobo alizaa naye watoto wane, mmoja wao aliitwa  Yuda. Ukifuatilia ukoo wa Yesu Kristo utalikuta jina la Yuda linajitokeza (Mathayo 1:2). Kwa hiyo japo Yakobo hakumpenda Lea kabisa lakini Mungu alitaka na akajua kupitia wao atazaliwa Yuda ambaye ni kiungo muhimu katika uzao wa Yesu Kristo.

Mfano wa nabii Hosea – Hosea 1:1-4

Mstari wa pili unasema ‘… Bwana alimwambia Hosea enenda ukatwae mke wa uzinzi…’ Ukisoma hii habari yote utaona jinsi Mungu alivyomwagiza Hosea kwenda kuoa mawanamke mzinzi na aliyekubuhu kwenye dhambi hii. Sasa kwa jinsi ya kibinadamu haikuwa rahisi kulikubali. Lakini kwa sababu ilikuwa ni jambo la MAPENZI YA MUNGU ili mlazimu akubaliane nalo hata kama yeye hakutaka. Na ukiendelea kusoma sura za mbele utaona fundisho na uponyaji ambao ulitokea kwa watu wa taifa la nabii Hosea kutokana na utiifu wake katika mapenzi ya Mungu.

 Mfano wa nabii Samweli – 1Samwel 16:1-13.

Hii ni habari inayoelezea agizo la Mungu kwa Samweli kwenda kwenye nyumba ya Yese kumtia mmoja wa watoto wake mafuta kuwa mfalme wa Israel baada ya Mfalme Sauli kuasi. Yese alikuwa na jumla ya wana nane wa kiume, Mkubwa  wao aliitwa Eliabu na mdogo aliitwa Daudi. Sasa Samweli alipofika kwa Yese, Yese aliwaita watoto wake wote isipokuwa Daudi aliyekuwa anachunga kondoo wa babaye, akaanza kuwapitisha kwa Samweli ili amtie mafuta yule ambaye ndio mfalme.

Alipopita mtoto wa kwanza, nabii Samweli akasema moyoni mwake Yakini masihi wa Bwana yupo hapa mbele yake, kwa lugha nyepesi alisema yamkini huyu ndiye Mfalme ninayepaswa kumtia mafuta. Je Mungu alimjibu nini alipowaza hivyo moyoni mwake. Mungu alimwambia ‘usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama mwanadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’. Mwishowe walipita watoto wote saba na Bwana akawakataa, hadi alipofika Daudi aliyetiwa mafuta.

Jifunze yafuatayo kutoka kwenye mifano hii mitatu;

 • Upo duniani sasa kwa ridhaa/ruhusa/mapenzi ya Mungu.
 • Na kama upo kwa ridhaa yake, ni lazima uishi kwa uongozi wake (Zab 32:8).
 • Thamani ya maisha yako ipo katika kuyatenda mapenzi ya Mungu.
 • Ni kipaumbele (priority) cha Mungu kujua nani atakuwa ni mkeo au mumeo. Sio suala la kuoa au kuolewa unayotaka wewe.
 • Mtazamo wako kuhusu mkeo au mumeo sio mtazamo wa Mungu. Ndoa yoyote anayo iunganisha Mungu ameshaiangalia mpaka mwisho wake.
 • Hivyo anapokupa mtu wa aina fulani, hata kama haendani na vigezo vyako, kumbuka lengo lake sio kukukomoa au kukuhuzunisha bali ni kuhakikisha anachotaka/mapenzi yake na si ya kwako yanatimia.
 • Smweli na Yakobo walitaka kukosea kwa sababu ya maumbile na mvuto wa sura kwa nje. Angalia sababu kama hizi zisikufanye ukaharibu mahusiano yako na Mungu na hivyo kukwamisha makusudi yake duniani.
 • Japo lilikuwa ni jambo gumu kwa Hosea kulikubali kibinadamu, yeye alitii na akabarikiwa kwa kulitumikia shauri la Bwana katika kizazi chake.
 • Ni mfano wa mfinyanzi na vyombo alivyovifanya. Mfinyazi ndiye anayejua sababu na matumizi ya chombo alichokifanya. Kazi yake huyu mfinyazi ni kuhakikisha lengo la ubunifu/uumbaji wake linafikiwa.
 • Na Mungu ndivyo alivyo, yeye ndiye aliyekufanya na anajua unachotakiwa kufanya hapa dunani, kazi yake ni kuhakikisha anakuongoza na kukuweka kwenye mazingira ya kusudi lake kupitia wewe kufanikiwa. Sasa mazingira au uongozi huo ni pamoja na kuhakikisha unaoa au kuolewa na mtu wa mapenzi yake.
 • Mtu wa mapenzi yake anaweza akawa tofauti na ulivyokuwa unataka. Ndugu yangu inapofika uko mahali kama hapa “the only option/alternative ni kuruhusu mapenzi yake yatimie na si kulazimisha yako kutimia”. This means there is no an option or alternative, you cannot escape it (Je unakumbuka habari za Yona, au Yesu pale Gethesemane?). Let his will be made in your life i.e.   Totally submit yourself to his will.
 • Usipokubali wakati una hakika hayo ni mapenzi ya Mungu kwako maana yake umeasi, ukiasi unatafuta matakwa yako na si yake. Mungu hata kulazimisha kuyatii mapenzi yake ila atakushauri kwa njia mbalimbali na mojawapo na mafundisho kama haya. Ukikataa ushauri wake ujue huko unakoenda yeye/uwepo wake hauko pamoja na wewe. Je unajua gharama ya kukosea au kutokutii mapenzi ya Mungu katika hili? Waulize wanandoa waliokosea ndio utajua madhara yake.
 • Naamini ujumbe huu umekuongezea maarifa na ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi. Zaidi ni imani yangu kwamba kama ukijua hakika haya ni mapenzi ya Mungu kuhusu mwenzi wako basi utahakikisha yanatimia. Haijalishi hayuko unavyotaka, ndugu zako, ukoo wako, kanisa au hata Mchungaji wako hawamtaki, kama unahakika ni mtu wa mapenzi ya Mungu mpendwa nakushauri RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE, KINYUME CHA HAPO NI MAJUTO.
 • “Asomaye na afahamu, msukumo ambao nimeupata kuhusu kuandika ujumbe huu haukuwa mdogo, ni kama nilikuwa naambiwa hakikisha ujumbe huu unakamilika haraka iwezekanavyo ili kuwapa maarifa haya watu wangu”.

 Mwenye sikio na asikie lile ambalo Roho wa Yesu anasema na kanisa. Amen.

JIANDAE KUZIKABILI CHANGAMOTO NA KUZITUMIA FURSA ZINAZOKUJA.

May 7, 2009

 Na: Sanga P.S.

Waraka wa Mei.

Jiandae kwa sababu mbele yako kuna changamoto zinakuja. Nyingine zimeruhusiwa na Mungu, au wewe mwenyewe kwa kumpa Ibilisi nafasi (Waefeso 4:27). Na bila maandalizi changamoto hizi zinaweza zikaharibu mahusiano yako na Mungu na kupelekea makusudi ya Mungu kupitia wewe kutofanikiwa.

Zaidi nataka ujiandae kwa sababu zipo fursa ambazo Mungu anazileta ili kukufanikisha. Lakini pia zipo fursa ambazo Shetani anazileta na usipokuwa makini nazo zitakuvuruga na kuharibu mahusiano yako na Mungu. Lengo la huu ujumbe ni kukuandaa na kukufunza ujue namna ya kujiandaa kuzitumia fursa ili kukabilana na changamoto mbalimbali zinazokuja.

 Changamoto ni nini?– ni mazingira kinzani, ya upinzani kwenye kila nyanja yanayokuja katika maisha yako. Kwa jina jingine ni matatizo. It is a situation that demands innovativeness, a situation/a trial available to test an organizational/personal capacity/ability.

Kwa hiyo haya ni mazingira/matatizo/vikwazo vinavyojitokeza ili kupima uwezo wa mtu au taasisi/kampuni. Lengo la changamoto ni kukusaidia  uwe mbinifu, mvumbuzi. Changamoto haziwezi kukwepeka kwenye maisha, kwa sababu zimeruhusiwa na Mungu mwenyewe na ndio sehemu ya maisha, soma Mithali 16:4 Ayubu 1:11 Waamuzi 3:1-6   Kumbukumbu 8:1-3

 Fursa–ni nafasi, mlango, uwezo, uwezekano, tukio, muda unaojitokeza/uliopo ili kukuvusha kwenye changamoto inayokukabili.

Fanya maandalizi kwa sababu mbele yako kuna fursa zinakuja ambazo hautakiwi kuzikosa hata moja. Fursa zinakuja ili zikusaidie kukabilana na changamoto ulizonazo. “A big/better opportunity favors the prepared mind”. Hii ina maana fursa inapojitokeza inakuja kuwa jibu la changamoto unayoipitia au itakayokuja kwa hiyo ni vema ukaitumia hiyo fursa vizuri.

Changamoto na fursa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu kutoka kwa Mungu. Si watu wengi wanaojua kuzitumia vizuri fursa ambazo Mungu amezileta kwenye maisha yao. Ngoja nikueleze siri hii, kila mwaka una changamoto na fursa zake. Sasa unatakiwa kujiandaa ili kukabiliana na changamoto na kwa kuzitumia fursa  husika.

Mifano ya watu walioshindwa kuzitumia vizuri fursa zao. Soma habari hii katika Luka 19: 41-44. Ukisoma hii habari utaoona jinsi Yesu alivyoulilia mji wa Yerusalemu kwa kushindwa kuzitumia fursa ambazo alizitengeneza kwao lakini wao wakashindwa kuzitumia.

Kosa la Jerusalem ni kutokujua muda wa kujiriwa kwake.. “All this will happen to you because u did not know the time of your salvation”. Kumbuka tulikotoka muda ni fursa Kumbe kuna magumu, mabaya, matatizo yanatupata kwa sababu tu hatujajua namna ya kuzitumia fursa zilizopo mbele yetu. 

Hebu tujifunze kutoka kwa nabii Haggai 1:3-11. Soma pia habari hii vizuri. Kosa la watu wa kkipindi cha nabii Hagai ni kusema huu si muda wa kujenga nyumba ya Bwana bali za kwetu. Kwa kuwa walishindwa kuitumia hii fursa wakajikuta kwenye hayo matatizo makubwa ya kijamii na kiuchumi.

Nini maana yake?

Ili uweze kuzikabili changamoto na kuzitumia vizuri fursa zilizopo ni LAZIMA/SHARTI UJIANDAE. Lada niseme hivi maandalizi ni ya LAZIMA ili uweze kukabiliana na changamoto na kuzitumia fursa mbalimbali vizuri.

Zifuatazo ni njia kadhaa ambazo zitakusaidia kujiandaa kukabilina na changamoto zinazokuja mbele yako;

 • Kwa kuwa na malengo. Mithali 29:18.
 • Kwa kuomba bila kukata tamaa (ombeni msije mkaingia majaribuni).
 • Tafuta kujua kusudila Mungu katika maisha yako i.e kwa nini uliumbwa. Ukijua kusudi ni rahisi pia kujua mipango yake katika maisha yako.
 • Ukishajua nini wajibu wako hapa duniani, basi tekeleza kwa bidii, moyo na uvumilivu hayo majukumu. Ongeza ufahamu katika nyanja (field) yako ili upate maarifa ya kukusaidiauwe na ufanisi mzuri zaidi.
 • Kuwa makini na maisha yako (Zaburi 1:1). Hili litakujengea maisha ya nidhamu ili kuhakikisha unakaa kwenye mpango wa Mungu. Kuishi katika mpango wa Mungu kuna gharama zake. Gharama kubwa ni kujikana, ni lazima ujifunze na ukubali kuyahesabu mambo mengine kuwa hasara ili shauri la Kristo liweze kufanikiwa.
 • Weka ndani yako/tafakari neno/sheria ya Bwana usiku na mchana. Hii itakupa kuona njia ikupasayo kuiendea. “Neno la Bwana ni taa ya miguu yangu”.
 •  Jifunze kuwa na muda wa utulivu wa kuomba na kuwaza. Mungu huwa anasema katika utulivu. Utulivu wako ni fursa kwa Mungu kukufunulia FURSA za kukabiliana na changamoto unazozipitia na zinazokuja. 

Mungu akubariki, naamini ukiyaweka haya katika utendaji taratibu utaanza kuona fursa ambazo mungu anazileta kwako ili kukufanikisha. Kumbuka siku zote kwamba mawazo yake ni ya amani, kukupa tumanini siku zako za mwisho.

Nawapenda wale wanipendao na wanitafutao kwa bidii wataniona.

Neema ya Kristo iwe nawe.

UNAUTUMIAJE UPAKO WA MUNGU JUU YAKO?

May 7, 2009

 

Na; Sanga p.S

Mathayo 21:28-32 – Ukisoma andiko hili utaoona habari  baba mmoja aliyekuwa na wana wawili, akamwita yule wa kwanza akamtuma aende kwenye shamba lake la mzabibu ili akafanye kazi za huko. Huyu kijana alikubali aksema nitaenda lakini hakwenda, babaye akamwendea yule wa pili akmwagiza kama wa kwanza, huyo wa pili akasema sitaki badaye akatabu akaenda.

Yohana 1:12 inasema “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”. Soma vizuri huu mstari tena, Biblia haisemi wote waliompokea walifanyika kuwa wana wa Mungu, kama wengi tulivyozoea kusema au kuomba, bali inasema aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu, hii ina maana suala la kufanyika mwana litategemea wanautumiaje ule uwezo/ au upako ulioko juu yao.

Hebu tujiunze hili somo kwa kuwatumia hawa vijana wa Mathayo 21: 28 32;

Kijana wa kwanza;

 • Alipewa uwezo/upako wa kumsaidia katika shughuri ile aliyokuwa ametumwa na babaye.
 • Lakini yeye hakutambua kwamba ndani yake kuna wezo/upako.
 • Alikubali kwa kinywa kwamba naenda lakini hakwenda kama alivyokiri.
 • Hakuwa tayari kutekeleza agizo la babye licha ya kuwezeshwa .
 • Hii inatufundisha kwamba alikosa unyenyekevu na utiifu kwa babaye.
 • Tunajifunza pia kwamba alishindwa kuutumia uwezo aliopewa na  babaye.

Babaye hakurudi kumuuliza kwa nini hukwenda shambani?. Hii ni kwa sababu kubwa mbili, moja jibu alilolitoa lilionyesha anaujua wajibu ila hataki kuutekeleza (kiburi) i.e alikosa unyenyekevu na pili alishindwa kutumia  uwezo aliopewa babaye, hivyo babaye akaamua ahamishie kwa mwingine.  Na hichi ndio kitu kilichotokea kwa Sauli na Daudi. Mungu alihamisha upako toka kwa Sauli na kumpa Daudi kwa sababu Sauli alishindwa kuutumia vizuri upako wa Mungu uliokuwa juu yake kama Mfalme.

Kijana wa pili.

Kitendo cha kukataa kwake kwenda na kisha kutubu na kwenda kinatufundisha kuwa;

 • Makosa huwa yanafanyika, mtu akitubu Mungu anasemahe.
 • Tunapotubu makosa tuliyofanya, Mungu yuko tayari kusamehe na kututuma tena.
 • Kuna upako wa ziada wa kukusaidia kutekeleza agizo hadi likamilike.
 • Huyu kijana alimpenda babaye na aliujua wajibu wake ndio maana mwishowe alienda.

Kwa nini licha ya kuamua kwamba ataenda shambai alirudi kwa babaye alirudi  kutubu?

 • Asingefanya kazi kwa amani.
 • Kazi isingekuwa na mafanikio mazuri.
 • Hivyo alirudi kuomba upako/uwezo/nguvu tena maana asingeweza bila upako huo.
 • Alihofu baba yake angeweza kumpa upako huo mtu mwingine. 

Jifunze yafuatayo toka kwa vijana hawa;

 • Mungu anapokupa uwezo/upako/nguvu za kufanya jambo fulani hakikisha unatumia vizri huo upako.
 • Kama awali umeshindwa kuutumia vizuri, omba rehema, na kisha usirudie tena makosa uliyofanya awali.
 • Upako unahitaji mahusiano yako na Mungu yawe mazuri na ndivyo kazi yako itakavyokuwa rahisi na yenye mafanikio.
 • Ukiweza kuutumia vizuri upako ambao Bwana ameweka juu yako kwa ajili ya kusudi lake tegemeana na nafasi yako hapo ndipo unafanyika mwana wa Mungu yaani unakuwa umefanya mapenzi ya muumba wako.

Kilio cha Mungu ni pale anapoona watu wake aliowapa uwezo kwa ajili ya kazi hapa duniani wanajisahau na kuanza kuifuatisha namna ya dunia hii. Wamesahau kwamba na Shetani naye amewapa uwezo watu wake ili kuhakikisha kwamba makusudi yake yanafanikiwa. Kumbuka kuwa Mungu na Shetani ni falme/kambi mbili tofauti siku zote. Kufanikiwa kwa makusudi ya kila falme kunategemea matumizi ya upako ambao kila mfalme anauachilia kwa watu watu wake.

Natoa wito wa kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake, tukikumbuka kwamba muda wa Bwana wetu Yesu Kristo kurudi umekaribia, hivyo tumia upako na nguvu zake vizuri kwa kazi yake. Kama ni Mchungaji, Mwalimu, Mtume, Nabii, Mwimbaji, Mwombaji nk tumika kwa bidii, Je atakapokuja  Bwana wako atakuhesabu kama mtumwa mwaminifu au la?. Biblia inaposema mtumwa mwaminifu inamaanisha mtumwa ambaye anafanya sawasawa na mapenzi ya Bwana wake.

Kanisa tuache kulumbana na kugombana, kumbukeni kwamba ili Shetani aweze kututawala ni lazima atugawanye. Hivyo tusikubali kugawanywa na Shetani, bali kila mmoja aingie shambani kwa ajili ya kazi ya Bwana.  Na ndio maana alisema mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache. Hakuwa na maana ya kwamba hakukuwa na watu , watu walikuwepo lakini walishindwa kuutumia upako/nguvu zao vizuri. Kwa hiyo uwepo wao haukuwa na maana kwa Bwana wao. Maana/thamani ya uwepo wao ingekuwepo kama wangeutumia uwezo/upako/nguvu walizopewa vizuri ili kuhakikisha makusudi ya Bwana wao yanatimia.

Naamini ujumbe huu mfupi utaamsha nia ndani yako ya kusimama na kujipanga kwa upya kuutumia vizuri uwezo/upako wa Mungu juu yako. 

Barikiwa, maombi yako ni muhimu sana juu ya huduma hii .