Archive for January 2009

ZINGATIA HAYA ILI 2009 UWE MWAKA WA BARAKA NA MAFANIKIO KWAKO.

January 4, 2009

dsc01032

Heri ya mwaka mpya mpenzi msomaji.

Waraka wa Januari.

 

Mpenzi msomaji kwanza nikupe hongera kwa kuweza kuingia mwaka huu wa 2009, ni neema iliyoje, wengi wa ndugu zetu, jamaa zetu ,rafiki zetu na majirani zetu tuliokuwa nao baadhi yao hawajafanikiwa kuingia mwaka huu wa 2009. Nakuambia si kwa bahati tu, au siyo nguvu n apesa zako. It is not for granted my dear; it is a special grace from God, for a special purpose.

 

Mpenzi msomaji labda nianze kwa kukuuliza maswali kadhaa kwamba je hivi unajua kwa nini umeingia mwaka huu wa 2009?. Ni watu wangapi unaowafahamu wamekufa lakini wewe umebaki?. Kibiblia Mungu anapokupa neema ya kuingia mwaka mwingine kama hivi analenga  mambo matatu;

 

ü      Uweze kutengeneza maisha yako kwa maana ya kuokoka kama hujaokoka na kwa maana ya kujenga mahusaiano yako na Yesu kama uliyaharibu kwa kufanya dhambi.

ü      Uweze kulitumikia kusudi lake hapa chini ya jua.

ü      Uweze kuufurahi uumbaji wake na fursa mbalimbali ndani yake.

 

Ujumbe huu unalenga sababu ya pili ya kulitumikia shauri la Bwana katika kizazi chako. Najua watu wengi sana wanataka kufanikwa sana katika maisha yao hapa chini ya jua. Niseme hivi ikiwa unataka kufanikiwa katika maisha yako hapa chini ya jua katika kila nyanja basi unataikiwa kutembea katika mpango na kusudi la Bwana. Kuafanikiwa kwako kumefungwa ndani ya kusudi la Mungu. Kamauanataka kuona mafanikio kwenye maisha yako basi fuata maagizao ya Mungu yanayohusu kusudi lake juu yako.

 

Sasa ili uweze kulitumikia shauri la Bwana katika kizazi chako na hivyo kupata mafanikio yaliyobebwa na kusudi hilo tekeleza mambo yafuatayo;

 

1. Kuwa makini na maisha yako.

 

Zaburi 1:1 ‘Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji, wala hakuketi barazani pa wenye mizaha”.

Umakini mkubwa unatakiwa katika maisha yako ukijijua ya kwamba wewe ni mtoto wa mfalme (Mungu) kwa hiyo huwezi kuishi kama watu wengine wanavyoishi. Unatakiwa kuishi kwa kanuni za mfumo wa ufalme wa Mungu na si za mfumo wa dunia hii. Kusudi la Mungu ndani yako linakutaka wewe uweze kuishi kwa taratibu za Ki – Mungu na si zile za kidunia. Kuwa makini sana na ushauri, mikakati unayopewa juu ya maisha yako  na mwisho kuwa makini na watu unaoshirikiana nao katika kutekeleza kusudi la Mungu kwenye maisha yako.

 

2. Usimpe Ibilisi nafasi.

 

Waefeso 4:27 “Wala msimpe Ibilisi nafasi”.  Kuna namna nyingi amabzo watu humpa Ibilisi nafasi, lakini kubwa na ya kwanza ni kutokutii maagizo ya Mungu katika maisha yako hasa yale yanayohusu kusudi la Mungu juu yako. Kukosa utiifu ni mlango wa Ibilisi kufanya kazi zake  kupitia wewe. Kutokutii kwako ni kumpa Ibilisi nafasi ya kukutumia katika kusudi lake.

 

Hivyo hakikisha unatii maagizo ya Bwana Mungu wako. Kadri unavyotii maagizo ya Mungu kwako ndivyo unavyompa Mungu nafasi ya kujifunua zaidi na kukupa maagizo mengine ya ngazi ya juu zaidi katika kutekeleza kusudi lake kupitia wewe. Si hivyo tu bali ndivyo na baraka zitavyoongozana kukujia. Maana Mungu ameziamuru baraka ziwaendee watu wanaotii maagizo yake. Kumbuka kila mtu chini ya jua ana kusudi lake maalumu la kuumbwa ambalo halifanani na mwingine. Kwa hiyo usiishi kwa kuangalia maisha ya mtu mwingine kama reference yako.

 

3. Kuwa na bidii katika kazi zako.

 

Mithali 22:29 “Je, umemwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme, hatasimama mbele ya watu wasio na cheo”.

Mhubiri 9:10 “Lolote mkono wako utakaolipata kulifanya ulifanye kwa nguvu zako…”

 

Bidii ni jitihada za kufanikisha. Hii ina maana katika kutekeleza kusudi la Bwana Mungu juu yako weka na jitahada za kufanikisha. Jifunze kutumia muda wako vizuri, lolote unaloanza kulifanya basi hakikisha unajituma mpaka uhakikishe unafanikisha ukijua kwamba yupo Mungu anayekutia nguvu, Wafilipi 4:13.

 

Hakikisha nguvu anazokupa Bwana Mungu unazitumia vizuri kufanikisha shauri la Bwana maishani mwako. Sikiliza bidii inahitajika kwa sababu kuna upinzani. Lakini upinzani hauna nguvu kwa mtu mwenye bidii bali kwa mtu mvivu. Jitihada unazozitumia kutafuta fedha, zitumie kwa kipimo hicho kutekeleza kusudi la Bwana katika kizzazi chako.

 

Nakutakia baraka za Mungu na mafanikio makubwa katika mwaka huu wa 2009. Ukizingatia mambo hayo matatu katika mwaka huu naamini kabisa utaenda vizuri katika kulitumikia kusudi la Bwana Mungu wako na hivyo kuzipata baraka zako na mafanikio yote ambayo Mungu amekukusudia katika mwaka huu pasipo kukosa hata moja. Labda niseme hivi kila mwaka una changamoto, fursa na baraka ambazo Mungu amekuandalia. Sasa njia rahisi ya wewe kuzipata kwa urahisi ni  kutembea katika kusudi la Mungu kwako. Nje ya hapo hata ukifanikiwa uwe na uhakika hujafikia kiwango cha baraka za Mungu alizokukusudia kwa mwaka huo.

 

Neema ya kristo iwe nawe mwaka huu wa 2009.