Archive for October 2008

JIFUNZE KUOMBA KWA NIDHAMU YA “MUDA WA KUOMBA”.

October 3, 2008

 

Na: Patrick Samson Sanga.

Waraka wa Oktoba.

 

Nakusalimu kwa jina la Bwana.

 

Imenilazimu  katika mwezi huu wa kumi tuweze kujifunza jambo hili juu ya “kuomba kwa kuzingatia muda wa kuomba”. Maombi ni somo pana sana, ndani yake kuna vitu vingi sana ambavyo kila siku Roho matakatifu yuko tayari kutufunza kwa kila aliye tayari kujifunza.

 

Hebu leo tujifunze kwa shuhuda kadhaa;

 

Ushuhuda wa kwanza;

Tarehe 18/09/2008, nikiwa mkoa wa Dare s salaam nilikaribishwa nyumba fulani kwa chakula cha jioni na kupumzika hapo. Kwa kawaida mimi ni mpenzi sana wa kuangalia kanda za video za vita. Baada ya chakula cha jioni mtoto mmoja wa ile familia akaniwekea mkanda wa vita niliouchagua. Basi tukaanza kuangalia huku tunazungumza mambo kadha wa kadha. Kama wewe ni mpenzi pia wa kanda hizo utagundua nyingi zake huwa zinaanza na kisa fulani halafu mbeleni ndio kunakuwa na mapambao mazuri kweli kweli, (mniwie radhi msiopenda kanda za vita, maana najua mpo) nimelazimika kutumia ushuhuda huu ili ujumbe uweze kueleweka.

 

Sasa mkanda ulipofika mahali ambapo ni patamu au pazuri kwa maana ya mapigano kuanza ghafla nikasikia rohoni msukumo wa kuomba uliokuja kwa kasi ya ajabu. Nikajaribu kujivuta vuta ili mkanda uishe kwanza, msukumo ukazidi kana kwamba utafikiri kuna mtu anachochea jiko, (ndani niilijua nini natakiwa kufanya lakini akili ilikuwa kwenye mkanda). Nikamwambia Roho mtakatifu niache nga nimalizie mkanda ndio nikaombe. Ghafla nikaletewa kwenye ufahamu wangu picha ya watu katika nchi fulani wanaoteseka na kuuwawa kwa sababu ya kumwamini Yesu. Ndipo likaja swali huo mkanda na hizi roho za watu walioniamini kipi muhimu?

 

Nakumambia licha ya kwamba nilikuwa ugenini nikamwambia yule ndugu niruhusu nikitumie chumba chako kuomba kwa muda usiojulikana. Niliingia kwenye maombi usiku ule bila kujali nipo ugenini maana rohoni nashuhudiwa usipoomba kuna roho zinaangamizwa usiku huu. Niliomba maombi ya kumanaisha mpaka nilipoona shwari rohoni mwangu. Nilipomaliza nakumbuka ilikuwa kama saa sita  hivi, hapo ndipo nikarudi kwenye kideo sasa, kwa raha zangu niliangali hadi saa nane. Nasema ka raha zangu kwa sababu ule msukumoulkuwa umekwisha saa hiyo. Baada ya hapo tukaenda kulala kulipokaribia kucha ndipo Roho wa Yesu akanionyesha kitu kilichotokea wakati waombaji wengine nikiwemo na mimi tulipokuwa tukiombea ile nchi. Maana najua jambo hili Mungu aliweka kwa watu wengi siku ile na ndio maana nimeandika na tarehe kabisa. Kristo akanishuhudia kwamba kwa kutii kule tuliubariki  sana myo wake. Nikamshukuru na kuendelea na kazi za siku hiyo.

 

Ushuhuda wa pili;

 

Siku moja, Ijumaa asubuhi, wakati najiandaa kwenda ofsini ghafla ukaja msukumo ndani yangu wa kumuombea kijana mmoja ninaye mfahamu, maana alikuwa ana kesi fulani mahakamani na Jumatatu ya wiki iliyofuata ndiyo ilikuwa hukumu yake. So nilichokifanya nilitii agizo la Mungu nikaanza kuomba, nikaomba kwa muda kiasi na kisha nikaendelea na kazi zangu za siku ile. Ilipofika Jumatatu yule ndugu akaenda mahakamani, kumbe kwa bahati mbaya alichanganya tarehe alitakiwa kwenda ile Ijumaa na siyo Jumatatu. Na kwa sababu hiyo mshtaki wake akawa amepewa kibali tangu Ijumaa cha kumkamata lakini ahsante kwa Yesu hakufanya hivyo, na baada ya taratibu nyingine za kimahakama kufuatwa wakapangiwa tarehe nyingine ya kufika mahakamani.

 

Ushuhuda wa tatu;

Ilikuwa ni Jumapili asubuhi nikiwa najiandaa kwenda kanisani, wakati naomba nikaletewa ndoa ya Mchungaji fulani wa kanisa lililoko hapa kwetu Tanzania, nikaagizwa kuiombea, basi nikaacha ajenda nyingine nikaingia kuombea ile ndoa na za watumishi wengine pia kwa ujumla. Nikaomba kwa muda mpaka niliposikia ndani yangu kuko shwari. Nilipoenda ibadani nikazima simu, baada ya kutoka ibadani nikapewa taarifa kwamba mke wa Mchungaji niliyesukumwa kuiombea ndoa yao  siku hiyo hakwenda ibadani.

Na kisa ni tofauti kati yake na huyo Mchungaji mpaka ikapelekea huyo mama kuondoka kabisa nyumbani na kwenda eneo jingine. Ahsante kwa Yesu ndani ya ule muda wa mchana kabla ya jioni kwenye hilo kanisa mambo yaliwekwa sawa na kisha mama mchungaji akarudi nyumbani.

 

Nini nataka ujifunze katika shuhuda hizi tatu;

 

30/09/2008 yaani Jumanne asubuhi, baada ya kufanya maombi ya kawaida, Roho mtakatifu akaanza kunifundisha akisema ndio maana siku zote huwa nakutaka na ninawataka watu wangu  waombe kwa kuzingatia muda wa kuomba. Kila ajenda ninayokuletea kuiombea, jua kabisa ina upako wa kukusaidia wewe kuombea suala hilo na pia unatakiwa kuomba kwa kuzingatia muda ule ninapolileta kwako bila kujali una ratiba gani kwa wakati huo, kwani mpaka nikalileta nilishajua kwamba una ratiba nyingine, ni nikaona kuwa licha ya hizo ratiba hilo nililolileta ndilo linalohitaji uharaka.

 

Ndipo akaniuliza unajua nini kingetokea kwa wale ndugu kwenye ile nchi waliokuwa wakiteswa , kwa yule kijana mwenye kesi mahakamni na pia kwenye ndoa ya yule Mchungaji kama usiongeomba katika muda niliokuletea msukumo wa kuombea hayo mambo ndani yako. Matokeo uliyoyaona  juu ya ile nchi,  kwa yule kijana katika kesi yake na kwenye ile ndoa yamesababishwa na kuomba kwako (kwenu) ndani ya muda niliokuagiza /niliokutaka uombe. Kwa lugha nyingine maombi yako (yenu) yamezaa unachokiona. Nikasikia furaha sana  kwa sababu nilishuhudiwa rohoni mwangu kuwa waaombaji wote walioiombea ile nchi, pamoja na haya mengine  nikiwemo na mimi tuiliubariki sana moyo wa Mungu kwa kutii na kuomba ndani ya muda alionitaka/aliotutaka tuombe.

 

Kwa sababu hili ni jambo zuri nimeona ni vema na wewe nikushirikishe. Maadamu, umeokoka na mahusiano yako na Mungu ni mazuri basi nina uhakika kwa namna moja au nyingine na kwako pia Mungu huwa anakuletea msukumo wa kuombea kitu/jambo fulani. Sasa si wengi wenye ufahamu kwamba mara nyingi kila ajenda ambayo Mungu anakuletea kuiombea, huwa inakuwa imewekwa kwenye muda maalumu na hivyo ni LAZIMA uombe ndani ya huo muda. Si watu wengi pia  wenye nidhamu ya kuomba kwa muda uliokusudiwa, na athari yake ni hii kadri Mungu anavyokuletea msukumo wa kuomba na akaona wewe hauzingatii muda wa kuomba, anachofanya ni kutafuta mtu mwenye nidhamu ya kuomba kwa muda bila kujali kwa wakati huo alikuwa anafanya nini, amtumie kwa ajili ya ufalme wake na jina lake.

 

Hivyo basi jifunze kujali muda wa kuomba katika maombi unayopewa kuyaombea, akikuleta msukumo kwenye basi/kazini/shuleni/ofsini nk uwe na uhakika ameshangalia hayo mazingira na kujua kwamba unaweza/utaweza kuomba kama utatii. Ili Mungu aweze kukutumia katika ofisi yake ya Kifalme jifunze kuujali muda wa kuomba.

 

Unajua kwa nini? 

 

Kwa sababu Mungu na muda  ni marafiki, na pia muda ni rafiki wa mtu anayejua kuutumia vizuri/kuukomboa wakati (muda). Muda ukikabidhiwa kwa mtu asiyejua kuutumia (kuukomboa) lazima wagombane. Na kwa sababu Mungu hataki kuharibu mahusiano yake na muda basi anachofanya ni kukuonya wewe kwamba ndugu jali/zingatia muda katika yale ninayokuagiza. Usipotii anchofanya ni kutafuta mtu mwingine amtumie, na hii ni kwa sababu kwa Mungu muda ni muhimu kuliko mtu.

 

Jifunze kuukomboa wakati ili kutimiza maksudi ya Mungu kupitia wewe na kuboresha mahusinao yako na Mungu .

 

Barikiwa na Bwana.

UNAJIFUNZA NINI KUPITIA HUDUMA YA ANANIA NA BARNABA KWA PAULO?

October 3, 2008

 

Na; Patrick Samson Sanga.

Utangulizi;

 

Nakusalimu katika jina la Bwana, mpenzi msomaji.

 

Katika nyanja hii, leo nimeona ni vema tushirikishane kile ambacho Mungu alikifanya  kwa Paulo kupitia huduma ya Anania na Barnaba. Si watu wengi sana wanofahamu nafasi ya Barnaba na Anania kwa Paulo, kwanza mtu mwingine ukimuuliza unawafahamu kina Anania wangapi kwenye kitabu cha Matendo ya mitume wangekutajia Anania, mume wa Safira tu yule aliyeuawa kwa kuiba sadaka ya kiwanja na mkewe.

 

Nafasi ya Anania na Barnaba kwa Paulo.

 

Matendo ya Mitume 9: 10 -19 “kulikuwa na Mwanafunzi huko Dameski, jina lake aliitwa Anania……..

Matendo ya Mitume 9:27 inasema “ na Barnaba akamchukua—-‘

 

Watu wengi sana wanamfahamu vizuri Paulo na kumsifu kwa kazi nzuri aliyoifanya, hata mimi nuaungana na watu wenye mtazamo huo. Lakini si watu wengi pia wanaojua kwamba kazi aliyoifanya Paulo ni matunda ya uaminifu na utiifu wa Anania na Barnaba kwa Mungu wao. Watu wengi wanafikiri Paulo baada ya kuokoka tu, hapo hapo alianza huduma, si kweli wanatheolojia wansema inawezekana Paulo alikaa miaka 14 kwanza ndipo akaanza huduma. Na ukisoma vizuri kitabu cha wagalatia utagundua Paulo alikaa miaka 17 tangu kuokoka kwake na ndipo huduma yake ikapata kibali machoni pa mitume na watu wote.

 

Sasa katika kipindi hiki cha mpito licha ya kuendelea na huduma, Paulo alikuwa akifunzwa au akielekezwa kitu cha kufanya kupitia watu mbalimbali na hasa Anania na Barnaba. Anania ndio mwanafunzi wa kwanza aliyejenga msingi wa huduma ya Paulo, hii ina maana Anania angekosea huenda huduma ya Paulo ingesumbua pia.

 

Vivyo hivyo na Paulo alipokwenda Yerusalemu wanafunzi wote walimtenga. Barnaba ndiye aliyemchukua akamtia moyo na kumfariji na kisha akaitambulisha huduma yake kwa mitume na wanafunzi wengine na ndipo Paulo akapata kibali na uhuru wa kufanya huduma hiyo. Unaweza ukaona kama ni kitu kidogo lakini katika ulimwengu wa roho hawa watu waliweka alama kubwa sana na ndio maana hadi leo mimi na wewe tunabarikiwa na nyaraka za Paulo.

 

Jifunze yafuatayo kupitia ndugu hawa.

 

Moja, usiidharau nafasi yako mbele za Mungu, kumtumikia Mungu si mpaka usimame madhabahuni ufundishe maelfu ya watu. Wapo waliopewa kusimama madhabahuni lakini pia wapo waliopewa kutengeneza wale watakaosimama madhahuni. Using’ang’anie wajibu usiokuwa wa kwako. Kila mmoja katika mwili wa Kristo ana wajibu wake.

 

Paulo amejulikana sana lakini mbele za Mungu Anania na Barnaba wanaheshima zao kubwa zaidi kwa kukubali maagizo ya Mungu juu ya Paulo. Haijalishi watu wanaidharau kiasi gani huduma yako, uwe na uhakika Mungu anaithamini sana kazi yako. Huenda wanadamu wasikutukuze au kuona umuhimu, mchango wako katika ufalme wa Mungu bali uwe na uhakika pia Mungu ameiona na kuiheshimu sana kazi yako. Kwa Mungu Anania na Barnaba wana nafasi ya kwanza kuliko Paulo kwa sasbabu wao walikuwa walimu wa Paulo kiroho. Na neno linasema  mwanafunzi hampiti mwalimu wake.

 

Tekeleza wajibu wako na Bwana Mungu atakubariki katika hilo. Usitafute kuonenkana na watu, tambua kwamba Mungu yu pamoja na wewe. Siku zote zote lenga kutengeneza watu watakaotengeneza na kubadilisha maelefu ya watu. Usibakie kung’anga’nia madhabahu isiyo ya kwako kwa kugombana na wachungaji. Kama Mungu amekuletea hata mtu mmoja kama Anania, tekeleza wajibu wako vema kwa kumfunza huyo. Nani ajuaye huenda atakuwa mfano wa Paulo kwa kizazi cha leo. Sasa ni vema ukae kwenye nafasi yako na ndipo ufanisi wako utakuwa mzuri zaidi. Kadri unavyokuwa mwaminifu kwa huyo mmoja ndivyo Mungu atavyowapitisha na wengine wengi kwako upate kuwajenga na kuwafundisha njia ya Kristo ili waje kuwa watumishi wazuri wa kesho.

 

Neema ya Kristo izidi kuwa nawe.