Archive for September 2008

JE, UNAKUMBUKA KUIOMBEA NCHI YAKO?

September 23, 2008

 

Na: Patrick Samson Sanga.

 

Yeremia 29:7

 

Ukisoma huu mstari utaona Mungu akiwaagiza hawa ndugu kwamba kautakieni amani mji ule miloko ndipo na amani yenu itakapowajilia. Kwa lugha nyepesi Mungu alikuwa akiwaambia  kama mnataka kuwa na amani katikati yenu basi uombeeni huo mji mlioko uwe na amani.  

 

Wiki ya pili ya mwezi huu wa tisa nikiwa nimelala niliona katika ndoto naamshwa halafu nikaanza kuomba, “nikiombea hali ya hewa ya nchi yangu”.

 

Mpaka sasa ninapoandika ujumbe huu, mzigo wa kuombea nchi bado haujaisha. Kila ninaposimama kuomba lazima na ajenda hii ije hata kama sikukusudia rohoni kuombea nchi yangu kwa wakati huo.

 

Kibiblia hatma ya nchi yoyote ile iko mikononi wa waombaji katika nchi husika. Na hii ina maana kama waombaji hawataomba kwa ajili ya nchi yao basi uwe na uhakika wametoa fursa/ruhusa/mpenyo/nafasi (Waefeso 4:27) kwa Shetani kufanya mambo yake kwa urahisi kwenye nchi husika.

 

Kama unataka kufanikiwa katika nchi  yako basi suala la kuiombea nchi yako ni la lazima. Mambo yanapoharibika kwenye nchi ujue waombaji hawakukaa kwenye nafasi zao vizuri/ au kwa lugha nyingine ujue waombaji  wamejisahau.

 

Watu wengi ni wepesi kulaumu sana viongozi wa nchi zao, wengine utawasikia wakisema kiongozi gani huyu, haya maamuzi anayofanya ameyatoa wapi, mbona kila kitu kwenye nchi hakijakaa sawa. Sikiliza, kama wewe ni muombaji, na unaona huyo kiongozi ana matatizo basi jua kabisa wewe ni sehemu au chanzo cha matatizo kwa huyo kiongozi. Kama maamuzi yake unaona ni mabaya, basi na wewe umechangia kwenye hayo maamuzi mabaya. Najua pengine jambo au lugha hii ni ngumu kwako kuielewa, endelea kusoma ujumbe huu  utelewa nini maana yake mambo haya.

 

Jambo lolote baya au la kuiathiri nchi kiuchumi, kijamii, kisiasa nk linapotaka kutokea/kabla halijatokea katika nchi, Mungu huwa anatoa taarifa hiyo kwa waombaji na kuwataka waombe kwa kadri atakavyowaongoza. Sasa utekelezaji unabakia kwa walinzi/waombaji, kama wakiomba mambo yatakaa sawa sawa/ wasipoomba mambo yataharibika.

 

Mambo yoyote unayoona yanatokea katika ulimwengu wa mwili ujue yalianzia katika ulimwengu wa roho. Waombaji/walinzi walishaoona kabla wengine hawajaona. Kama unachokiona kimefanyika katika ulimwengu wa mwili ni kitu chema jua kabisa waombaji waliopewa kusimamia/kuombea jambo hilo walisimama kwenye zamu zao vizuri. Na kama likiwa baya jua kabisa kwamba tatizo liko kwa waombaji hawakusimama vema kwenye zamu zao.

 

Maafa/ajali/vita/matetemeko/vimbunga nk yanapotokea kwenye nchi kwa wingi na kuharibu miundo mbinu, uchumi, watu kupoteza maisha, makazi nk hata kama ukikataa uwe na uhakika kuna namna fulani waombaji hawakukaa sawa   kuombea maeneo hayo. Hapa sina maana haya mambo hayawezi kutokea lakini maana yangu ni hii kama waombaji wangeomba vizuri, athari  zilizojitokeza zisingetokea kwa ukubwa huo na watu wengi wasingepoteza maisha yao, tena kwa  hakika kuna baadhi ya ajali zisingetokea kabisa.

 

 

Siku moja, nilikuwa nazungumza na mtu mmoja juu ya nchi yetu na utendaji wa viongozi wetu. Huyu ndugu aliwalaumu sana viongozi wa serikali yetu, na akasema kwamba haoni kitu gani viongozi wanafanya kwenye nchi hii. Nilimuuliza maswali kadhaa, nikasema tangu wameingia madarakani umewaombea mara ngapi? Na je ni kawaida yako kuwaombea? Akataka kukwepa kujibu swali langu, nikarudia Umewaombea mara ngapi au kwa kiwango gani viongozi wako?.

 

Akakiri sijaomba kwa ajili yao. Nikamuuliza swali la pili kwa nini unawlaumu? Je huoni kama kwanza unamkosea Mungu na pili hao viongozi?. Nilimweleza hayo kwamba  wewe unajua kabisa katika 1Timotheo 1:2, Biblia imekuagiza kuwaombea viongozi wako kila iitwapo leo. Sasa wewe hujawaombea hata mara moja halafu unabakia kuwalaumu, maana yake nini? Wewe ndiye unawajibika kuomba halafu huombi unategemea nini? Mpenzi msomaji angalia neno linasema, usihukumu usije ukahukumiwa. Je, na wewe je ni kawaida yako kuombea nchi yako na viongozi wake?

 

Imenilazimu kuandika  waraka huu  ili kukuhamasisha tuweze kuomba pamoja kwa ajili ya nchi yetu na viongozi wake. Mungu alinde nchi yetu na mipaka yake, aiponye nchi yetu dhidi ya roho za ajali,vimbunga, matetemeko nk, alinde watanzania wa ndani na wa nje, thamani ya fedha yetu izidi kuimarika, miundombinu izidi kuboreshwa na kujengwa, huduma za kijamii ziboreshwe, hali ya kisiasa na kiuchumi, amani izidi kutawala na mengine kadha wa kadha kadri Mungu atavyozidi kutujulusha.

 

Mwombaji mwenzangu nakusihi na kukagiza kama mtumishi wa Kristo kwamba tangu sasa, jifunze kuiombea nchi yako, na kama ulikuwa unaomba ongeza bidii yako. Nilipohoji rohoni niombee nini kwenye hali ya hewa ya nchi yangu/ au je ni hewa gani Mungu ana maanisha? Roho mtakatifu alinifunulia mambo mengi ya kuombea ndani yake.

 

Nawe nakusihi anza kuomba katika yale unayoyafahamu. Kwa kuwa hili ni agizo la Mungu kwamba tuombee nchi yetu, kadri unavyoendelea kuomba, tena kwa nidhamu ya muda anaotaka yeye uombe, ndivyo atavyoendelea kukufunulia mambo mengi zaidi siku kwa siku. Nidhamu yako kwa yale anayokuletea kuyaombea itamfanya aendelee kujifunua kwako kila wakati kukupa ajenda nyingine za kuombea na kukushirikisha mawazo yake juu ya nchi yako.

 

Msukumo uliokuwa ndani yangu siku napata jambo hili ulikuwa ni mkubwa sana na kuonyesha kwamba kama hatutaomba, kwanza tutakuwa tumemkosea Mungu kwa kuwa tumeshindwa kuwajibika na pili tutakuwa tumetoa fursa/kumpa ibilisi nafasi ya kufanikisha mambo yake. Naomba ujumbe huu uamshe nia/roho ya kuomba ndani yako ili kwa pamoja tuweze kuombea nchi yetu na watendaji wake wote.

 

Kuto kuombea nchi yako, Kibiblia ni makosa. Si watu wengi wanaojua na kulitazama suala la kuto ombea nchi yao kama  kumkosea Mungu. Nimalize kwa kusema kama hutaomba basi lolote litakalotoea nchini mwako usilwalaamu viongozi wako, anza na wewe kwanza.

 

Omba, omba, omba… ni wito Mungu kwako siku ya leo (Mwenye sikio na asikie.)

 

MATOKEO YA DHAMBI YA UZINZI/UASHERATI KWA MTU ALIYEOKOKA.

September 11, 2008

 

 

Na : Patrick Samson sanga.

Waraka wa Septemba.

 

Nakusalimu katika jina la Bwana mwezi huu wa tisa. Katika mwezi huu nimesukumwa ndani yangu tujiunze habari hii juu ya athari/matokeo ya dhambi ya zinaa/uasherati pale kwa mtu aliyeokoka. Yaani kitu gani kinatokea mtu aliyekwisha kuokoka anapoanguka katika dhambi hii.

 

Katika Mithali 6:32 Biblia inasema “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake” na pia katika  Mithali 6:26 inasema “Maana kwa Malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani”

 

Ni watu wengi sana ambao wamerudi nyuma na kuanguka katika dhambi hii, wapo ambao kwa hiari yao walikuja kwangu moja kwa moja niweze kusaidiana nao katika hili, wapo wengine ambao hata wao pasipo kuniambia walilofanya Mungu alifunulia na kunionyesha jinsi watu hao walivyoanguka katika dhambi hii na madhara yake. Hadi sasa bado kuna kundi kubwa la watu waliokoka ambao bado dhambi hii ina nguvu juu yao na bado wanafanya jambo hili kinyume na mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

 

Si kana kwamba Mungu anafuga dhambi kwa kutokuwadhihirisha hao watu na uovu wao, isipokuwa hataki jina lake litukanwe, kwa kuwa ikijulikana huyo mtu au hao watu wameanguka huenda  kutokana na nafasi zao kiuongozi, kihuduma kiushuhuda nk jina la Mungu litatukanwa sana na mataifa lakini pia hata na wale waliokwisha kuokoka. Kwa lugha rahisi hao watu au huyo mtu atakuwa ametoa nafasi ya jina la Mungu kutukanwa.

 

Kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya watumishi wa Mungu katika makanisa yao wanoona athari ya hili jambo katika upana wakekama Biblia inavyosema.   Inafika mahali baadhi yao wanawafariji wale walioanguka kwa kusema jipe moyo, tubu na Mungu ni wa rehema atakusamehe. Na wengine utasikia wanasema haukuanza wewe, Daudi naye yalimshinda sembuse wewe.

 

Wengine wanatumia maandiko kabisa wanasema mwenye haki huanguka mara saba, we mara moja tu wala isikusumbue sana tengeneza tu Mungu atakusamehe, na wengine wanasema mimi mwenyewe nilishindwa so, hata wewe isikusumbue sana kazana tu uoe wa kwako au omba upate mume. Ni kama vile watu wanatumia rehema/neema ya Mungu kuendelea kutenda dhambi (It seems as if people are taking the advantage of God’s mercy/grace to commit sin). 

 

Si kana kwamba napingana na neno au na mawzo ya hao watumishi wenzangu. Nakubali  kwamba Mungu husamehe dhambi na maovu  ikiwa ni pamoja na dhambi hii ya uasherati/uzinzi. Mungu husamehe kwa sababu moja hafurahii kifo cha mwenye dhambi na pili ni ili kukurejesha kwenye nafasi yako ili uweze kulitumikia kusudi lake. Lakini je, unajua madhara/matokeo ya dhambi hii kwa mtu aliyeokoka anapoifanya? Hata kama akikusamehe/amekusamehe, unajua nini kimetokea/kilitokea kwako pale ulipofanya dhambi hii? Au je unaijua gharama ya kurejea kwenye nafasi yako aliyoikusudia Mungu?

 

Katika miaka zaidi ya sita niliyomtumikia Mungu nimejifunza na kukutana na kesi nyingi sana za watu mbalimbali  katika suala hili. Kwa hiyo ninapoandika haya si tu maadamu naweza kuandika ila naandiaka vitu ninavyojua vinatokea kweli na athari yake ikoje. Na mwezi huu wa tisa ndio kitu ambacho nasikia rohoni tujifunze kwa pamoja.

 

Biblia inasema aziniye na mwanamke afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake? Huenda huwa unausoma tu huo msitari bila kujua uzito wa hayo maneno. Ni vizuri kwanza ukajua kwamba ndani ya nafsi ya mtu ndiko kwenye hisia, nia, akili, na maamuzi. 

 

Mambo matatu yafuatayo ndiyo yanayotokea mtu aliyeokoka anpofanya dhambi hii ya uasherati/zinaa ;

 

Moja, Kuharibika kwa mfumo wa mahusiano na mawasiliano kati yake na Mungu.

 

Katika  mfumo wa ufalme wa Ki – Mungu ni kawaida kwa mtu aliyeokoka na mwenye mahusiano mazuri na Mungu, kuona Mungu akiwasiliana naye kwa njia mbalimbali ili kumshirikisha mawazo na mipango yake ikiwa ni namna ya kumuongoza mtu huyo katika kusudi lake chi ya jua.  Hii ina maana suala la mawasiliano kati ya mtu na Mungu ni la kawaida kwa mtu mwenye mahusiano mazuri na Mungu wake.

 

Sasa mtu anapofanya dhambi hii, athari yake ni hii, dhambi inaharibu mfumo huu wa mahusiano kati ya mtu na Mungu. Na mahusiano kati ya mtu na Mungu yakiharibika  mawasilano kati ya Mungu na mtu yanakatika/kuharibika pia. Ninaposema yanakatika ina maana si rahisi kwa Mungu kusema tena na huyo mtu au huyo mtu kusema tena na Mungu wake kwa sababu asili/mazingira ya mfumo huu hayaruhusu na hili linapelekea mafunuo/sauti ya Bwana kuwa hadimu kwako, kwa kanisa, kwa jamii, kwa kampuni na hata nchi tegemeana na nafasi yako katika ufalme wa Mungu.

 

 

Pili, Kuharibika kwa mfumo wa kufanya maamuzi/kufikiri ndani yako.

 

Dhambi hii inaharibu mfumo wa kufanya maamuzi, shetani anapomuongoza mtu kufanya dhambi hii, lengo/interest yake ipo kwenye nafsi ya mtu huyo. Shetani akikamata nafsi ya mtu maana yake amekamata akili/nia ya mtu huyo, akikamata akili ya mtu huyo maana yake amekamata maamuzi yake pia.   Na akikamata maamuzi yako amekamata matokeo ya maisha yako ya sasa na ya baadae.

 

Hivyo mtu huyu hataweza tena  kufikiri mambo ya rohoni kama Paulo anavyoagiza kwa Warumi ile sura ya 8:5 “Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili, bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Hivyo kufanya dhambi hii ni kuathiri mfumo wako wa kufanya maamuzi, na hii ina maana hata Mungu akileta wazo lake kwako huwezi kulipokea maana mfumo wa kuamua umeukabidhi kwa Shetani kwa njia ya zinaa/uasherati.

 

Tatu, Kuharibika kwa mfumo wa utiifu ndani yako.

 

Warumi 2:13 says ‘Kwa sababu sio wale wasikiao sheria walio  wenye kuhesabiwa haki, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki”. Kuharibika kwa mifumo huu huu, ni matokeo ya kuharibika kwa mifumo miwili hapo juu yaani ule wa mahusiano na ule wa kufanya maamuzi. Ubaya wa dhambi hii inaharibu mifumo hii ambaayo ndiyo misingi ya mwenye haki. Fuatili maisha ya watu wengi sana walioanguka kwenye dhambi hii angalia utiifu wao mbele za Mungu ukoje. Nakuhakikishia utagundua ni ngumu sana kwao kutii maagizo ya Mungu kwao. Mtu wa aina  hii hata Mungu akimpa maagizo ya kutekeleza hataweza kwa kuwa tayari mahusiano yamevunjika, mamuzi yametekwa .

 

Nini Mungu anataka tujifunze katika hili? 

 

Unapokuwa na mahusiano mazuri na Mungu  hii mifumo yote mitatu inafanya kazi vizuri. Dhambi hii inapoingia inasababisha kuharibka kwa mifumo hii mitatu. Kitu kibaya au kinacho muumiza Mungu ni kwamba  hata kama akikusamehe pale utakapotubu, kwa sababu hii ni mifumo itakugharimu sana kuirejesha mahali pake. “It will cost you taking the systems back to the ancient paths”. Na ndio maana neno linasema afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Hii ina maana kila kilichomo ndani ya nafsi pia kinaangamizwa. Ili kuirejesha mifumo hii maombi ya muda mrefu  ya rehema na kutengeza mahali palipobomoka ni ya lazima.  

 

 

Yamkini unaweza kusema la muhimu Mungu amenisamehe, hayo mengine sijali sana.Unaweza kusema hayo maneno kama hujui/ huelewi muda unathamani kiasi gani kwa Mungu, na pia mahusiano kati ya muda na Mungu. Ngoja nikuambie siri ya Mungu na muda japo kidogo. Muda na Mungu ni marafiki, na tena wote wana mahusiano mzuri sana.  Muda anaongoza maamuzi ya Mungu na Mungu anaongoza matumizi ya muda kwa kuiweka mipango katika ndani ya mtu na kumwagiza atekeleze ndani ya muda. Hivyo kwa Mungu muda ni muhimu sana.

 

Kitu gani namaanisha hapa;

 

Mungu hakutenga/kuweka muda wa mtu kurejesha mifumo hii kwa sababu umeanguka katika dhambi. Katika kipindi ambacho wewe unatubu na kutengeneza kwa Mungu wako ili kurejesha mifumo hii, basi uwe na uhakika upande wa pili umesha athiri kusudi la Mungu  duniani kupitia wewe. Sasa kama utatumia siku tano, mwezi mmoja, miezi sita, mwaka mzima nk, kurejesha hii mifumo basi kwa kipindi hichocho utakuwa umekwamisha kusudi la Mungu kupitia wewe. Na ndio maana biblia inasema Shetani anawinda nafsi yako iliyo ya thamani, maana anajua akikamata nafsi yako amekamata akili, nia, hisia na maamuzi yako na hivyo amefanikiwa kuharibu hiyo mifumo na kusababisha mipango ya Mungu isifanyike kwa muda aliokusudia kupitia wewe.

 

Labda tujifunze kwa mfano huu;

 

Fikiria umepangiwa na Mungu kusafiri umbali wa kilomita 500 ndani ya masaa saba (7).  Mungu amekupa gari ambalo ni kusudi lake kwako. Hivyo litazame   gari ulilopewa kama kusudi la Mungu kwako na wewe ni dereva. Sasa wewe ukaamua kuliendesha  gari bila kuweka maji kwenye injini. Baada ya kusafiri umbali wa kilomita 300 injini ya gari ikafa kwa kukosa maji na mbele yako zimebaki kilomita 200. Je unajua utakuwa umeathiri kwa kiwango gani kusudi la Mungu?. Kutokana na mfano huu unapotenda dhambi hii  je unajua ni kwa kiwango gani utakuwa umeathiri mipango ya Mungu kupitia wewe duniani kwa kipindi chote ambacho utakuwa unairejesha mifumo mahali pake?.

 

Kinacho muumiza/huzunisha Mungu kimsingi si kwa sababu umeanguka dhambini, lakini ni kwa sababu kuanguka kwako dhambini kunamzuia yeye kukutumia wewe mpaka hiyo mifumo yote irejee mahali pake. Hii ina maana interest ya Mungu ipo kwenye muda. Maana anajua itakugharimu wewe muda wa kutengeneza na itamgharimu yeye muda wa kukusubiri wewe utenegeze mifumo hii.

 

Nisikilize  Mungu hategemei wewe uanguke katika dhambi hii, maana kadri unavyoanguka ndivyo unavyokwamisha na kuchelewesha kazi ya Mungu duniani kupittia wewe? Je unajua hasara na matokeo ya kukwamisha na kuchelewesha kazi ya Mungu?.

 

Naamini ujumbe huu utakusaidia kuhakiksha unafanya maamuzi ya kutofanya tena dhambi hii si kwa sababu imeandikwa tu usizini bali ni kwa sababu unampenda Mungu na unataka kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa bila kukwamishwa kwa dhambi hii.

 

 

 

Barikiwa tuzidi kuombeana.