Archive for August 2008

ANGALIA MAAMUZI UNAYOFANYA KATIKA KUTAFUTA MWENZI WA MAISHA YASIHARIBU KUSUDI LA MUNGU KWAKO.

August 26, 2008

 

Na : Sanga P.S

 

Isaya 55: 8 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana”.

 

Najua yamkini umeusoma au kusikia na hata kuufundisha sana huu mstari. Lakini leo katika kona  hii ya ndoa nataka nikuonyeshe tafsiri ya huu mstari kwa kadri ya neema ambayo Bwana amenijalia kwenye hili eneo. 

 

Ukisoma vizuri huu mstari utagundua kwamba kulikuwa na ushindani/ kutofautiana kimawazo kati ya Mungu na hawa watu anaowasema hapa. 

 

Yeremia 29:11 inasema “maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi asema Bwana….” Sasa ukiunganisha maneno ya Yeremia 29:11 na yale ya Isaya 55: 8 utagundua kuna mawazo na njia za kutekeleza hayo mawazo  ambazo Mungu alikuwa nazo juu ya maisha ya hawa watu.

 

Sasa tatizo na wao kuna mawazo na njia walikuwa nazo juu ya maisha yao ambazo hazikuwa sawasawa na zile za Mungu. Na ndiyo maana akasema mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu. Kwa lugha rahisi Mungu alikuwa akisema geukeni/acheni hayo mawazo (mipango) na njia zenu tekelezeni mawazo yangu na njia zangu ndipo mtafanikiwa. Mungu alisema hayo maneno bada ya kuona matokeo ya mawazo na njia zao ni mabaya, kwa kuwa yalikuwa nje ya kusudi lake juu yao.

 

Ukitaka kuthibitisha kauli hii soma ule mstari wa 7 katika Isaya 55 Biblia inasema “Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie Bwana naye atamrehemu, na arejee kwa Mungu wetu naye atamsamehe kabisa”.

Anaposema mtu mbaya/asiye haki anamaanisha mtu ambaye anataka kutekeleza mawazo na njia ambazo zipo kinyume na mawazo na njia za Mungu juu ya maamuzi/suala/jambo lolote linalomkabili huyo mtu.

 

Maana yake nini mambo haya?

 

Katika maamuzi ya kupata/kutafuta mwenzi wa maisha najua kabisa  kuna mambo/vitu ambavyo ungependa huyo mwenzi wako awe navyo. Kuna namna fulani ungetamani awe kiumbile, kiumri, kikabila, kielimu, kiutajiri, nk, kwa kifupi tuseme haya ni mawazo yako juu ya mwenzi wako wa maisha . Niseme kwamba ni kweli haya ni mawazo yako lakini usifikiri Mungu naye hana mawazo ya nani anastahili/anafaa kuwa mwenzi wako wa maisha. Hakika Mungu anayo  mawazo tena mazuri kabisa juu ya nani anafaa kuwa mwenzi wako.

 

Hii ni  kwa sababu yeye ndiye aliyekuumba na ndani yako ameweka kusudi lake ambalo anataka litekelezwe kwa njia au mikakati yake. Moja ya mikakati hiyo ni kuhakikisha unoa au kuolewa na mtu aliyemkusudia yeye.

Jifunze kuruhusu mawazo ya Mungu na njia za Mungu zitekelezwe katika maisha yako,  ili kusudi lake liweze kufikiwa.

 

 .

Kumbuka Mithali 16:1 inasema, maandalio ya moyo ni mwanadamu, bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana. Unaweza kupanga au kuamua aina ya  mwenzi unayemta na ukaweka sifa/vigezo kadha wa kadha lakini  Kibiblia/Ki- Mungu SI LAZIMA iwe kama ulivyopanga kwa sababu mwenye kutoa jawabu la ulimi juu ya maandalio ya moyo wako ni Mungu.

 

Nimalizie kwa kusema kazi ya Roho mtakatifu ni kukushauri na kukuongoza  na si (kukulazimisha) katika yaliyo mapenzi ya Bwana. Hivyo hata katika suala la mwenzi wako yeye atafanya wajibu wake ikiwa utamruhusu. Maamuzi yanabakia kwako kutekeleza mawazo na njia zake kwako, ukikakataa uwe na hakika umekaribisha  mabaya na kutotendewa haki katika ndoa yako sawasawa na Isaya 55:7 na mwisho wenu ni majuto.

 

Mpendwa wangu angalia sana maamuzi unayotaka kufanya, hakikisha yamepata kibali cha Bwana ukikumbuka haya ni maamuzi makubwa na yanagharimu sana.

 

Nakutakia safari njema katika hili, tukumukane katika maombi.

MAOMBI PEKE YAKE BILA IMANI HAYATOSHI KUTENGENEZA JIBU LA MAHITAJI YAKO.

August 26, 2008

Waraka wa Agosti. 

Na: Sanga P.S

 

 

Marko 9:14-29.

Hii ni habari ya yule baba aliyekuwa na mwana mwenye pepo bubu na kiziwi, akamleta kwa wanafunzi wasiweze kumtoa. Wakati huo Yesu alikuwa mlimani akiomba na wanafunzi wengine watatu, aliposhuka baba mwenye mtoto akamwambia, Mwalimu nimemleta mwanangu kwako , ana pepo bubu, na kila ampagaapo humbwaga chini , naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda , nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo wasiweze, akawajibu akasema enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu akamponya.

 

Ukisoma ule mstari  wa 28 Biblia inasema “ Hata alipongia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza, mbona sisi hatukuweza kumtoa? Akawaambia namna hii haiwezi kutoka kwa neno lolote , isipokuwa kwa kuomba.

 

Mpenzi msomaji katika mwezi huu wa nane nimeona ni  vema nikushirikishe mojawapo ya siri nyingi za ajabu katika fungu hili la maneno, nayo ni ‘Maombi peke yake bila imani hayatoshi kutengeneza jibu la mahitaji yako’.

 

Katika habari hii, huyu baba alimleta mwanawe kwa Yesu ili amponye, sasa kwa bahati nzuri hakumkuta Yesu bali   wanafunzi tisa na watu wengine. Nasema kwa bahati nzuri kwa sababu Yesu angekuwepo huenda tusingejifunza kutokana na makosa ya wanafunzi wale tisa.

 

Wale wanafunzi walijaribu kumuombea yule kijana mgonjwa lakini wakashindwa kumtoa yule pepo. Yesu alipowasili na kupewa taarifa hizo aliumia sana akawauliza enyi kizazi kisicho amini nikae nanyi hata lini, kwa lugha rahisi alikuwa akiwaambia kukosa kwenu imani kumesababisha mshindwe kutoa huyu pepo na si kitu kingine.

 

Sasa swali walilomuuliza Yesu kwenye mstari wa 28 linaonyesha wanafunzi hawakuelewa kwa nini wao walishindwa kumtoa pepo? Ndipo Yesu akawajibu namna hii haiwezi kutoka kwa neno lolote, isipokuwa kwa kuomba.

 

Ukiliangalia jibu la Yesu si rahisi sana kumuelewa. Unaweza kufikiri aliwachanganya zaidi wanfunzii kwa jibu lake. Kwa sababu aliposema namna hii haitoki isipokuwa kwa kuomba alimaanisha nini? Je ina maana wanafunzi walikuwa hawaoombi? Kwa vyovyote vile walikuwa wanaomba, Je nini kilipungua kwenye maombi yao? Mstari wa 19 unatoa jibu pale aliposema enyi  kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Na hapa ndipo tunapojua kumbe maombi peke yake bila imani hayatoshi kutengeneza jibu la mahitaji yatu.

 

Imani ni nini? Waebrania 11:1 inajibu “ Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarijiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”. Ule mstai wa sita pia unasema “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza , kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”.

 

Kitu gani tunajifunza hapa? wakati wanafunzi wanaomba ndani yao walikosa uhakika wa mambo yatarijiwayo, kwa lugha rahisi maombi yo yalikosa au kupungukiwa imani, yaani ndani yao uhakika wa yule pepo kutoka haukuwepo wakati wanaomba.

Neno linasema kila amwendeaye/aombaye lazima aamini kwamba yeye yupo.

Hivyo wanafunzi walitakiwa kuomba + imani = jibu la hitaji la yule baba.

Au walitakiwa kuomba/kukemea/kutaja hitaji lao + uhakika kwamba yule pepo atatoka = Pepo kutoka na kijana kufunguliwa.

 

Mpenzi msomaji nimalize kwa kusema hata wewe najua unakutana na changamoto nyingi sana ambzo unazipeleka mbele za Mungu kila siku kwa maombi sasa jifunze katika mwezi huu kuwa maombi pekee bila imani hayatengenezi jibu lako. Hivyo kwa kila unalo omba hakikisha umejumlisha na imani ndani yake nawe utaona jibu lako.

 

Barikiwa, maombi yako ni muhimu sana katika huduma hii.