Archive for July 2008

KIJANA ZINGATIA HILI, ILI UWEZE KULITUMIKIA KUSUDI LA MUNGU.

July 12, 2008

bible2 

“Huu ni waraka maalumu kwa vijana wote ambao bado hawajaoa au kuolewa”.

Na :  Sanga.P.S.

 

Kijana mwenzangu ninakusalimu kwa jina la Bwana. Katika mwezi huu nina neno fupi ambalo nimeona ni vema nikushirikishe na wewe juu ya ‘UMUHIMU WA KUUTAFAKARI MWISHO WAKO UKIUHUSIANISHA NA KUSUDI LA MUNGU JUU YAKO’

 

Tarehe 29/04/2008 nilifanya maombi maaulumu yaliyolenga kuombea vijana ambao bado hawajaoa au kuolewa, nikimsihi Mungu afungue milango ya wao kuoa au kuolewa, kwa sababu wengi wao ninaowasiliana nao bado hawajaoa au kuolewa.

 

Katika kunijibu Mungu alinipa mistari kadhaa na kunifunulia tafsiri yake, nami nikaandika kwenye kumbukumbu zangu na mwezi huu nimeona ni vema na wewe nikushirikishe mafunuo haya maana naamini yatakusaidia;   

 

Fungu la kwanza ni, Luka 19:41 – 44.

Soma fungu hili lote, mimi nitanukuu maneno machache tu. “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akasema, laiti ungalijua hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani … siku zitakuja adui zako watakujengea boma … watakuangusha chini wewe na watoto wako … kwa sababu hukutambua  majira ya kujiwa kwako.

 

Fungu la pili ni, Isaya 1:2-3

“Sikieni enyi mbingu tega sikio ee nchi … kwa maana Bwana amenena; nimewalisha watoto na kuwalea nao  wameniasi, ng’ombe amjua Bwana wake, punda ajua kibanda cha Bwana wake, bali Israel hajui, watu wangu hawafikiri”.

 

Fungu la tatu (3) ni , Kumbukumbu  la Torati 39:29.

 “Laiti wangalikuwa na akili hata wakafahamu haya, ili watafakari mwisho wao”.

 

Katika mafungu haya matatu ya maandiko Roho mtakatifu alinifunulia yafuatayo;

 

*Kwanza alisema, usifikiri hao watu unaowaombea siwajibu. Wengi nilishawajibu, lakini wengine kwa sababu zao binafsi, wazazi wao, Viongozi wao n.k  hawajatii wazo langu juu yao/mapenzi yangu juu yao. Mimi ni Mungu ninayeangalia kesho/mwisho wa mtu/watu na lolote ninalofanya nimeliona mwisho wake. Sasa kwa kuwa hawa vijana wamekataa wazo langu kwa kutofikiria mwisho wao na kusudi langu kupitia wao na ndoa zao,  basi, hakika ndoa zao   zitakuwa na shida na baadhi yao wataniacha kabisa.

 

*Pili, Mungu kwa uchungu sana anataka mbingu na nchi zisikie na zijue kwamba   watoto wake ambao amewalisha na kulea  wamemuasi. Watoto hao wameshindwa kujifunza kupitia ng’ombe na punda, na tatizo lao ni kutokufikiri. Hii ina maana kutokufikiri kwao kumepelekea wao washindwe kumjua Mungu.  Kinamuuma sana Mungu, anapoona watu aliowaokoa na kuwafundisha au kuwaonyesha njia wapasayo kuiendea   wanakataa kwenda katika njia yake.

 

Zaburi 32:8 anasema “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama”. Sasa kitu kinachomuumiza ni pale anapowaonyesha watu njia yake au mapenzi yake kwao kuhusu wake/waume zao watarajiwa na akina nani halafu wao wanashindwa kutii. Licha ya kuwaonyesha au kuwajulisha mapenzi yake bado wameasi.

 

 

Ndugu kijana mwenzangu, natamani Mungu alete kitu hiki ndani yako kwa uzito ule ule aliouleta ndani yangu, ili usije ukakataa wazo la Mungu kwako na ukamkosea hata kuikosa mbingu kwa sababu tu ya mke au mume.

 

Sasa fanya yafuatayo ili kukaa katika mapenzi yake;

 

(a)   Jifunze kutafakari mwisho wako, ukijua ya kwamba mwisho wako uko mikononi mwa Mungu. Na kwa sababu hiyo maamuzi yoyote unayoyafanya ni lazima,  na si ombi umruhusu Mungu akuongoze ili uenende katika njia zake.

(b)   Haijalishi kwa jinsi ya mwili huyo mtu ana upugnufu/udhaifu wa aina gani kwa mtazamo wako, maadam una uhakika ni mtu wa mapenzi ya Mungu uishi naye, basi usijaribu kukataa huyo mtu kwa sababu Mungu ameona unakokwenda kukoje na huyo aliyemleta ndiye ambaye mtafika naye mwisho wenu.  

(c)    Hivyo basi wazo lolote/kijana/mtu yoyote anapokuja kwako kutaka   muoane na ndani yako unaona hakika ni mtu wa mapenzi ya Mungu, basi  kabla hujakataa kwa sababu zako binafsi, kaa chini utafakari, mhoji Mungu kwa maswali yanayokutatiza. Unapokwenda mbele za Mungu siku zote yeye ni mwaminifu atakupa majibu ya msingi na nina kuhakikishia unapotii uongozi wa Mungu kuna baraka za ajabu sana. Lakini unaposhindwa kutii  itakugharimu kuliko unavyofikiri.

 

  *Mungu anapokuonyesha/anapokupa mke au mme hamleti kwako kwa lengo la kukukomoa, bali anakua ameangalia kwanza kusudi lake, changamoto zilizopo mbele yenu na umbali mnaotakiwa kusafiri kwa pamoja kisha ndio anawaunganisha kwa kukupa mtu (mke au mume) ambaye anajua ukiwa naye hakika kusudi lake litafikiwa na mtaweza kuzikabili na kuzishinda changamoto zote zitakazojitokeza.

 

Hivyo mwenzi yoyote unayempata kama una hakika katoka kwa Mungu hata kama ana mapungufu gani kwa fikra zako au wazazi au dhehebu lako mimi nakushauri usimkatae, kwa sababu kwa huyo wewe utaweza kulitumikia shauri la Bwana.

 

Aliye na masikio na asikie lile ambalo Roho wa Bwana asema na vijana.

 

 

 

 

 

LAKINI NAMNA HII HAITOKI ILA KWA KUSALI NA KUFUNGA.

July 12, 2008

 Waraka wa Julai.

 

 

Na: Patrick Samson Sanga.

 

 

Mathayo 17:12 “lakini namna hii haitoki, ila kwa kusali na kufunga”.

 

Mpenzi msomaji naamini kwa sehemu huenda unaijua vizuri habari ya Mathayo 17:14-21 “Habari hii inahusu kijana mmoja aliyekuwa na pepo wa kifafa, wanafunzi wa Yesu wakamwombea wasiweze kumponya. Yesu alipokuja toka mlimani akamponya yule kijana. Baadae walipokuwa faragha wanafunzi walitaka kujua kwa nini wao walishindwa kumtoa pepo. Yesu aliwapa sababu 2, moja kwa sababu ya upungufu wa imani yao, na pili akawaambia namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”.

 

Sasa mwezi huu nataka tutafakari swali hili kwa pamoja, Je, ni wakati gani/au kwa mahitaji gani unatakiwa kusali na kufunga? Hapa Yesu alimaanisha kuna mambo/maombi mengine hayawezi kujibiwa mpaka kwa maombi ya kufunga.. Sasa swali ni wangejuaje kwamba hitaji hili/namna hii inataka kusali na kufunga au kusali bila kufunga.

 

Nina amini hata msomaji wnagu una mahitaji mengi unayoombea, yapo ya kwako binafsi, familia, kanisa, nchi, kazi, mume, mke, mchumba, biashara, watoto nk.

 

Hii ina maana kuna baadhi ya maombi yako hayatajibiwa haraka au kabisa hadi uombe na kufunga. Swali ni Je, unajuaje kwamba sasa natakiwa kusali na kufunga au kusali bila kufunga.

 

Mambo matatu yafuatayo yatakusaidia;

 

a)         Kutokuona matokeo ya maombi ya bila kufunga.

Hii ina maana huenda kwa muda mrefu umekuwa ukiombea jambo fulani bila kuona matokeo yake. Usibakie kusema kwamba natakiwa kuwa mvumilivu. Huenda hiyo ni taarifa kwamba ndugu namna hiyo haitoki ila kwa kusali na kufunga. Hivyo ongeza kufunga kwenye maombi yako, utaona matokeo yake kwa kipindi kifupi.

 

b)        Uzito na uharaka wa suala unaloombea.

Uzito wa jambo unaloombea ni kwa mtu binafsi (too personal). Jambo ambalo kwako ni zito/mzigo kwa mwingine si zito. Mfano suala la binti anayetafuta mume/mtu anayetafuta kazi uzito wa hili suala hauwezi kulingana kati ya mtu na mtu. Huenda huyu dada ameomba miaka 3 na hajaona mtu akija kumsemesha, kwa mtu huyu tatizo hili ni zito sana. Hatua kama hii inamtaka afunge na kuomba.

 

Mfano mwingine ni hatari ya kifo kama mazingira yaliyowakuta kina Esta katika utawala wa mfalme Ahusuero, pindi ulipoandaliwa mpango wa kuua wayahudi wote, tunaona walifunga kwa siku tatu, au watu wa mji Ninawi walipoambia na Yona kwamba wasipotubu mji wao pamoja na wao wataangamizwa, nao walifunga. jifunze kwa Esta, Daniel, Yona, Nehemia, Yesu n.k

 

c)   Kwa uongozi wa Roho mtakatifu.

   Mathayo 4:1 Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani… akafunga siku arobaini …………”

Awali ya yote kumbuka Roho mtakatifu ni msaidizi  hata kuomba anatusaidia. Roho mtakatifu ndiye anayeleta au kuweka  mzigo wa kuomba ndani ya mtu. Roho mtakatifu ndiye anayejua habari ya mambo yajayo, kwa sababu hiyo huwa anamsukuma mtu kufanya maombi ya kawaida au ya kufunga tegemeana na hitaji husika na kile kilichopo mbele ya mtu husika. Kwa lugha nyepesi Roho mtakatifu humuongoza mtu katika maombi ya kawaida au ya kufunga pia.

 

Hivyo basi Roho mtakatifu akikuongoza kufunga wewe usimzimshe au usikwepe maana yeye anajua nini kinaenda kutokea mbele yako na kinahitaji nguvu kiasi gain ya maombi ili uweze kuvuka au ili namna hiyo iweze kutoka.

 

Ni imani yangu kuwa ujumbe huu mfupi utakusaidia kukujengea nidhamu katka maombi yako kwa ujumla na utakuwa makini na maombi unayoyafanya.

 

Barikiwa na Yesu kristo.