MTAZAMO WA MUNGU KUHUSU UTAWALA.

Na: Patrick Samson sanga.

Mwanzo 22:17 ‘Katika kukubariki nitakubariki na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamilki mlango wa adui zako”

Siku zote Mungu anapofanya jambo au kitu huwa anafanya kwa kusudi. Mungu ametuumba/amekuumba ili uweze kutawala kila kiumbe kiendacho juu ya nchi. Sasa kwa bahati mbaya sana imefikia mahali kanisa la Mungu limejisahau,limeona kwamba siasa, madaraka na utawala ni dhambi.
Mtazamo wa wengi ambao wachungaji, viongozi wa makanisa na makundi mbalimbali ya kidini wanafikiria kwamba huwezi kuwa mwanasiasa, kiongozi wa serikali halafu kwa wakati huohuo uwe na maendeleo mazuri kiroho.Wanaaamini ukiingia kwenye siasa basi suala la mbinguni kwako ni kitendawili. Na yapo baadhi ya makanisa ambayo tayari yameshapanda mawazo ya namna hii kwa washirika wao. 

Hao hao wenye mawazo ya namna hii ndio wanakuwa wa kwanza kuilaumu serkali iliyopo madarakani mara wanasema rushwa imezidi, haki haitendeki, umaskini haupungui n.k swali ni kwamba wanamlalamikia nani wakati wao wamekataa kugombea nafasi hizo za uongozi na wamewazuia wengine kufanya hivyo na hawawahamasishi wengine kugombea na zaidi hata kadi ya chama chochote cha siasa hawana.  

Lengo la waraka huu ni kukuonyesha kibiblia suala la utawala au uongozi kupitia siasa Mungu analitazamaje.Tutajifunza somo hili kwa kuangalia mambo manne yafuatayo:- 

*Mungu anatumia madaraka ili kuliimarisha agano lake.

Mwanzo17:6-7 “Nitakufanya uwe na uwezo na uzao mwingi sana,nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao,kuwa agano la milele,kwamba nitakuwa Mungu wako na kwa uzao wako baada yako.     Sikiliza siku zote Mungu ili aweze kuimarisha agano lake anatumia madaraka/uongozi.Agano linalozungumziwa hapa ni la Mungu kukaa pamoja na wanadamu.Katika Yeremia 31:33 anasema “ Bali agano hili ndilo nitakalolifanya na nyumba ya Israel,baada ya siku zile asema BWANA, Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu kwao nao watakuwa watu wangu.  

Mungu anapotaka kuimarisha uhusiano wake na watu wake na kuimarisha agano lake ni lazima aweke baadhi ya watu katika nafasi za juu serikalini ili kuweza kuliimarisha hili agano lake. Maana yake anatumia madaraka ili kuimarisha uhusiano wake na watu wake.Ndiyo maana anawaambia Ibrahim wafalme yaani watawala kwa lugha ya sasa,watatoka kwako,maana yake ni hii nitauzidisha na kuubariki uzao wako na ndani yake  watatoka watawala ili kuliimarisha agano langu.       

Mungu alipotaka kuliimarisha agano lake katika kujenga hekalu ambapo watu watakuwa wakija kumuabudu ilibidi amuweke Sulemani kwenye utawala,alipotaka kuyaondoa machukizo katika nchi na kuimarisha uhusiano wake na watu alimweka mfalme Asa kwenye utawala, mwenye sikio la kusikia na asikie. Soma habari hizo katika 1 wafalme 6 na 2mambo Nyakati15. 

*Mungu anatumia madaraka/uongozi ili kulifanya kanisa kumiliki mlango wa adui zao.

Mwanzo 22:17 “katika kukubariki nitakubariki,na katika kuzidisha nitakuzidishia uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani,na uzao wako utamiliki mlango wa adui zako”.  Sikiliza Mungu anayatazama madaraka au uongozi kama nyenzo ambayo watu wake wataitumia kumiliki mlango wa adui zao. Ngoja nikuambie siri hii ya ufalme wa mbinguni. Siasa/madaraka ni mlango. Huu mlango ukikaliwa au kutawaliwa na watu wanaomjua Mungu nakuambia kazi za Ibilisi katika ulimwengu wa roho zitakosa nguvu.Mlango huu huu ukikaliwa na watu wasiomjua Mungu basi kazi za shetani zitapata nguvu.

Je adui zako/zetu ni akina nani au ni nani? Ile Waefeso 6:12 imeweka wazi adui zetu ni akina nani? Neno linasema “kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama,bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”   Sasa falme na mamlaka,wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho ndio adui wa uzao wa Mungu.

Utawala wa mfalme Daudi ni mfano mzuri wa utawala ambao Mungu aliutumia ili kuwafanya Israel kumiliki mlango wa adui zao. Na ndiyo maana Mungu anawaambia Ibrahim nitakubariki na kukuzidisha ili uzao wako uweze  kumiliki mlango wa adui zao. La sivyo uzao wako utatawaliwa kimwili,kiroho na kiuchumi na adui zao. Mwenye sikio na asikie yale ambayo roho waBwana asema na kanisa.  

*Mungu anatumia madaraka ili kuwarithisha watu wake baraka/ahadi  alizowaahidi katika Neno lake.

Yoshua 1:6 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa,maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa”. 

 Ukisoma pia ule mstari wa pili Mungu anawaambia Yoshua, Musa mtumishi wangu amekufa, sasa nataka wewe Yoshua uwe hodari na moyo wa ushujaa maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii, kwa lugha nyepesi Mungu anasema nchi hii/ahadi hii au hizi nilizowaahidi watu wangu hawawezi kuzipokea au kuzirithi bila mimi Mungu kukuweka wewe kwenye utawala.    Sasa kumbuka nimekuambia madaraka ni mlango, Hivyo Mungu atatumia mlango huo kupitishia  baraka zake kwa watu wake kwa yeye kumuweka mtu wa uzao wake.  

*Mungu anatumia/anayatazama madaraka kama njia ya kuliponya taifa lake na watu wake.

 Mwanzo 41:33 inasema”Basi Farao ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri”.Ukisoma sura nzima ile ya 41 utaona habari Farao aliyeota ndoto kuhusu taifa lake la  Misri. Na Yusufu ndiye aliyeweza kutafsiri ile ndoto ya mfalme kwa kumueleza kuwa kutakuwa na miaka saba ya njaa inakuja,lakini kabla ya hiyo miaka saba ya njaa kutatangulia miaka saba ya neema au shibe au wingi wa chakula.

Hivyo mfalme atafute mtu wa akili na hekima amuweke juu ya nchi ili kwa miaka saba ya shibe kikusanywe chakula kitakachotumika katika miaka saba ya njaa.

Na ukiendelea mstari ule wa 34 unasema,Farao akaweka wasimamizi juu ya nchi. Hata sasa hakuna mtu ajuaye kwamba katika nchi yako nini kitatokea baada ya mwaka mmoja au miwili, huenda ni njaa,mafuriko,ukame,Rushwa, kushuka kwa fedha ya nchi yako au uchumi kwa ujumla nk, ni Mungu tu. Sasa ili apate kuliponya taifa na mambo yenye kuleta athari katika uchumi  nchini au hata kwa mtu mmoja mmoja Mungu anamweka  madarakani mtu ambaye ndani yake amebeba neno la kuwavusha  katika majanga hayo bila kuathari Uchumi wa nchi na hivyo kuliponya taifa. 

Naamini baada ya kuwa umesoma ujumbe huu,mtazamo wako sasa kuhusu mambo ya utawala ,uongozi na siasa kwa ujumla utakuwa umebadilika.Nakupa changamoto nenda katika chama chochote cha kisiasa nchini soma sera zao halafu fanya maamuzi ya kujiunga kwenye hicho chama. Usiishie hapo bali pia gombea kila aina ya nafasi kuanzia katika ngazi za chama na kuendelea.

Neema ya Bwana wangu Yesu Kristo na iwe pamoja nawe.

Advertisements

4 comments

  1. Mungu aishie milele yote aliyekuwako kabla ya kuweko kwamisingi ya dunia awazidishie hekima na roho ya maarifa mbarikiw

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s