Archive for February 2008

NAMNA AMANI INAVYOWEZA KUAMUA KWA AJILI YAKO.

February 5, 2008

Waraka wa Februari. 

Na; Patrick Samson sanga.
Wafilipi 4:7 inasema ‘Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote , itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu’.

Wakolosai 3:15″ Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja tena iweni watu wa shukrani “.

Yohana 14: 27 ‘Amani yangu nawaachieni; amani yangu nawapa;niwapavyo mimi si kama ulimwengu utoavyo.Msifadhaike mioyoni mwenu wala msiwe na woga’

Ule mstari wa 6 wa kitabu cha Wafilipi sura ya nne unasema “Msijisumbue kwa neno lolote ;bali katika kila neno kwa kusali na kuomba , pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu’’ Kimsingi mstari huu unazungumza suala la mahitaji/maombi ambayo watu wanakuwa nayo siku zote na wanayapeleka mbele za Mungu. Katika haya mahitaji mhusika anakuwa anahitaji kujua/kupata jibu kwa kuwa linamsaidia au litamsaidia katika kufanya maamuzi fulani.

Haya ni maombi ambayo mhusika anasubiri kwa hamu jibu ili afanye maamuzi. Mfano, Binti anayeomba kujua je, kijana aliyemfuata kutaka kumuoa ni wa mpango wa Mungu au kijana anayetaka kujua ni binti gani katika wengi waliopo ambaye hakika ni mapenzi ya Mungu waoane, au pia mtu anayeomba kujua je ni mpango wa Mungu aache kazi na kuanza huduma n.k au tuseme mwanafunzi ambaye anenada kuanza mwaka wa kwanza chouni na anataka kujua ni kozi gani Mungu anataka asomee? Nk.

Sasa, Kibiblia amani imewekwa au unapewa amani ili ikusaidie kufanya hayo maamuzi. Maana imeandikwa katika Wakolosai 3:15 “Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu…………’.Sasa hii ina maana ni lazima amani iamue kwanza na kisha wewe ufuate uongozi wa amani yaani amani ya Kristo ikuongoze wewe kufanya mamuzi, ikuelekeze upi ni uamuzi sahihi na mzuri.
Je, amani inaamuaje ?

Kwa kuuhifadhi moyo wako na nia yako katika Kristo Yesu.

Ezekieli 38:10 inasema Bwana Mungu asema hivi; itakuwa katika siku hiyo, mawazo yataingia moyoni mwako, nawe utakusudia kusudi baya; na pia Nehemia 6:8 kwenye kipengele cha mwisho inasema ‘Lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni’, ukisoma pia ‘Mathayo 15:19 inasema ‘kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati,wivi,ushuhuda wa uongo na matukano’. Hivyo basi ukiiunganisha hiyo mistari mitatu utajua kwamba kumbe mawazo huingia moyoni, mawazo hubuniwa moyoni na kisha mawazo hutoka moyoni.

Moyo wa mtu ni uwanja wa mapambano ambao ndani yake kuna mawazo mengi sana ambayo humwingia mtu na kubuniwa yakisubiri kutoka. Yapo mawazo ya kutoka kwa Mungu,shetani au ya mtu binafsi. Na mara zote yale ya shetani ni ya kupinga kusudi la Mungu kwa huyo mtu na pia mara nyingi ya kutoka kwa mtu pia huwa hayalingani na ya Mungu.

Sasa kwa kujua hilo Yesu alituachia amani, kinachotokea wakati unaomba ni hiki , amani inaukamata moyo wako ili kuhakikisha kwamba mawazo mengine ya Shetani yanayoweza ingia ndani yako yasiweze kuuondoa moyo wako kwenye nafasi ya wewe kukaa ndani ya kusudi la Bwana ili kulinda nia ya Kristo ndani yako isiharibiwe.

Hii ina maana kazi ya amani ni ya ulinzi. Kwa hiyo tunaweza kusema licha ya amani kuwa mwamuzi, amani pia ni mlinzi. Amani anafanya kazi ya kuulinda moyo wako na nia yako isiharibiwe na mawazo ya kutoka kwa shetani kwa kuwa mawazo hayo yamebeba kusudi baya.
Kwa hiyo amani inapigana kuhakikisha moyo wako hauharibiwi na mawazo mengine yaliyoko kinyume na mapenzi ya Mungu juu ya ombi au hitaji ulilonalo mbele za Mungu. Sasa ikishaulinda moyo wako dhidi ya mawazo mengine kuhakikisha kwamba hayaharibu mpango wa Mungu juu yako ndio inakuongoza katika uamuzi ambao ni sahihi.

Na ili kujua uamuzi huo ni sahihi amani itakupa raha nafsini mwako, utajisikia furaha na nafsi yako kufunguka juu ya kufanya jambo fulani. Ukiona hayo mazingira ndani yako fuata amani inakokuelekeza kumbuka amani ni mwamuzi na mlinzi. Sasa siku zote mlinzi huwa hampeleki bwana wake kwenye hatari na hii ina maana amani itakuongoza kufanya uamuzi ambao ni bora na ulio katika mpango wa Mungu.

Uzuri wa amani ya Kristo ni huu inakuonyesha uamuzi ambao ni wa hatari/mbaya kwako na pia inakuonyesha na kukuongoza katika uamuzi ambao ni mzuri kwako. Inakuonyesha kwamba huo uamuzi ni mbaya kwa kukosesha raha, furaha na uhuru juu ya uamuzi unaotaka kuufanya. Na pia inakuonyesha kwamba huo ni uamuzi bora kwa kukupa raha na furaha na uhuru juu ya huo uamuzi.Kwa kifupi niseme unapoomba maombi ya namna hii halafu ukakosa amani ndani ya moyo wako jua kwamba huo uamuzi huenda ni wazo la shetani au huenda ni la Mungu lakini, huo sio muda muafaka wa kutekeleza hilo wazo japo hili linategemeana na aina ya hitaji ulilonalo.

Hivyo ukikosa amani usitekeleze hayo mawazo yanayokujia kama jibu, endelea kuomba na kama hali hiyo ikiendelea basi usifanye huo uamuzi maana mlinzi hayuko na wewe. Sasa kama ni la Mungu lakini muda wake bado, Mungu ni waminifu atakujulisha na kukufunilia hilo pia.

Lakini unapoomba ukiiona amani katika mawazo yanayokuja kama majibu jua kabisa hilo ni wazo la Mungu na ndani yake limebeba mpango na njia za Mungu za jibu la ombi lako. Lakini pia pima kwanza hayo mawazo kwa njia ya neno la Mungu uone kama viko sawa maana Shetani hujigeuza ajifanye malaika wa Nuru. Hata siku moja shetani hawezi kukuletea wazo ambalo linaendana na neon la Mungu.

Soma huu mstari utaelewa ninchosema zaidi Zaburi 34:14 ‘Uache mabaya ukatende mema, utafute amani ukaifate’.Maana yake achana na maamuzi mabaya tulia sikiliza amani iankuongoza wpi na kisha ifuate maana yeye ndiye mlinzi wa moyo wako.
Ni imani yangu kwamba ujumbe huu utakusaidia kujibu mawali mengi uliyokuwa nayo mbele za Mungu.

Amani ya Kristo na iwe pamoja nawe.

KWA NAMNA GANI ROHO MTAKATIFU NI MSAIDIZI?

February 5, 2008

Na; Patrick Samson Sanga.

Yohana 14:16-17‘Nami nitamwomba baba, naye atawapa msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata akae milele; ndiye roho wa kweli amabye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui bali ninyi mnamtambua , maana anakaa kwenu na atakuwa ndani yenu.Kabla Bwana wetu Yesu hajapaa kwenda mbinguni aliyasema maneno hayo hapo juu akiwaeleza kwamba si muda mrefu yeye ataondoka kwa kuwa wajibu alioujia ameumaliza (Yohana 17:4) na kwa sababu hiyo atamwomba baba (Mungu) ili awape msaidizi mwingine yaani Roho mtakatifu. Kwa lugha nyepesi hapa Yesu alikuwa akimtambulisha Roho mtakatifu kwa wanafunzi kama msaidizi mwingine badala yake. Lengo la waraka huu ni kujifunza, je Roho mtakatifu kwa namna gain ni msaidizi?

Roho mtakatifu ni msaidizi katika nyanja zifuatazo;

*Msaidizi katika kutufundisha na kutukumbusha.
Ndani ya biblia kuna mafumbo mengi sana ambayo bila msaada wa Roho kutusaidia kuyafunua kwetu hakuna anayeweza kuyaelewa wala kuyajua. Hivyo Roho mtakatifu ni wa muhimu kwetu kwani anatusaidia kuyaelewa mawazo ya Mungu katika neno lake.

*Msaidizi katika kutushuhudia juu ya Yesu (Yohana 15:26).

 Hapa Roho mtakatifu anafanya kazi ya kutushuhudia hata sasa juu ya uweza na nguvu za Yesu Kristo na utendaji wake. Mfano mzuri ni pale baada ya Yesu kupaa na kuwaacha mitume na walipoanza kuandika nyaraka zao, ni Roho mtakatifu aliyewashuhudia na kuwakumbusha zaidi kimapana juu ya uweza wa Yesu .Neno atanishuhudia lina maana Roho mtakatifu atawafunulia habari zangu(Yesu) na kuwahakikishia kwamba mimi ndiye ninayewaagiza.

*Kuuhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu.
 (Yohana 16;8) Huu wajibu unahusishwa na kufanya maamuzi, hapa msaada wa Roho mtakatifu upo katika kutujulisha lipi ni dhambi na lipi sio hasa katika yale unayotaka kufanya, pia lipi ni la haki na lipi sio. Mwisho anatusaidia katika kufanya maamuzi, neno hukumu linawakilisha kuamua, hivyo roho mtakatifu anatusaidia kuchukua uamuzi ambao ni mzuri na wa kufaa ili kusudi la Mungu kwetu lifikiwe.

*Msaidizi kama kiongozi mwnye kututia kwenye kweli yote na mwenye kutupasha habari za mambo yajayo (Yohana 16:13).

Katika zaburi 32:8 neno linasema nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea,nitakushauri jicho langu likikutazama. Roho mtakatifu ndiye anayefanya kazi ya kutuongoza na kuhakiksha tunadumu katika kweli ya neno la Mungu kwa kila tulifanyalo.

Ni imani yangu kwa kuwa umejua, Roho mtakatifu anafanyikaje msaidizi basi utamtumia vizuri. Nafasi ya Roho ni sawa kabisa na nafasi ya chakula katika mwili wako. Nafikiri unajua usipokula kwa muda mrefu utakufa tu kwa lazima. Na hii ina maana ni lazima utumie chakula, hivyo basi ili uweze kulitumikia kusudi la Bwana katika kizazi chako ni lazima umtumie vizuri Roho mtakatifu kama msaidizi.

KWA NINI ULIZALIWA AU KUUMBWA?

February 5, 2008

Na: Patrick Samson Sanga.

Mwanzo: 1:26“Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, WAKATAWALE samaki wa baharini na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi”

Katika waraka huu nataka tujifunze juu ya kusudi la wewe kuumbwa na nini ufanye ili uweze kutawala.    Zipo sababu nyingi za wewe kuumbwa lakini moja wapo na kubwa ni ili wewe uweze kutawala. Dhana ya  utawala ni pana, mimi nimeigawanya katika nyanja za kiroho, kidini, kisiasa, kiuchumi, ki-ardhi, kibiashara, ki-taaluma nk.
Sasa aina ya utawala ninayotaka kuzungumza ni utawala katika nyanja ya siasa inayopelekea utawala katika serikali. Yafuatayo ni mambo ya msingi ambayo yatakusaidia wewe uweze kutawala sawasawa na kusudi la Mungu la kukuumba;

(a)Kwanza amini kwamba wewe unaweza kuwa kiongozi mzuri na pia siku moja utakuja kuwa kiongozi mzuri  katika serikali ya nchi yako. Amini kwamba hauna upako wa kupiga kura tu, bali pia tayari Mungu ameshakupaka mafuta (upako) wa kupigiwa kura na wakati ukifika wapiga kura watathibitisha hilo.

(b) Pili, amini kwamba inawezekana kabisa kuokoka na wakati huohuo ukawa mwanasiasa na kiongozi mzuri wa taifa lako. Jifunze kutoka kwa wafalme mbalimbali katika Biblia kama vile Daudi, Yehoshfati nk. Siasa sio mchezo mchafu kama wengi wanavyofikiri, shida ipo kwa wale waliojiingiza kwenye siasa. Kama wanasiasa unawaona kama hawafai kwa kuwa ni waongo, au wala rushwa haina maana siasa ni mbaya. 

(c)Fanya maamuzi ya kujiunga na chama chochote chenye sera nzuri katika nyanja zote za msingi na hasa kiuchumi. Nakushauri kabla hujajiunga na chama chochote, soma kwanza sera zao, uzielewe na kuzipima vizuri na kisha sasa amua kujiunga na chama hicho baada ya kuwa umeridhika na kuamini kwamba unaweza fanya nao kazi.

(d)Gombea kila aina ya uongozi katika chama chako kwa nafasi zake mbalimbali.
Kuanzia chini mpaka nafasi ya juu. Chukua fomu za uongozi, jaza bila kuwa na shaka, mwombe  Mungu akufanikishe, usiogope kushindwa katika uchaguzi, hayo ni matokeo na haina maana kwamba haufai, huenda sio wakati wa Bwana lakini pia kama kuna makosa uliyofanya jirekebishe

(e)Jenga mahusiano mazuri na makundi mengine katika jamii.
 Usiwabague watu kwa rangi, umri, kabila wala dini zao. Maana hao watu kwanza ndio utakaowaongoza ukipita, wao ndio watakaokupigia kura na zaidi baadhi
yao utafanya nao kazi katika ofisi moja.

(f)Mwisho ongeza ufahamu na Imani yako kuhusu siasa/uongozi. Nenda kwenye Biblia soma mistari yote inayohusu mambo ya utawala na uongozi ili uongozeke kiimani na pia zaidi ya hapo pia ongeza elimu ya dunia hii kuhusu mambo ya siasa. 

Naamini ujumbe huu mfupi utakubadilisha kufikiri kwako kuhusu utawala (siasa) na kisha utayafuatilia mambo ya uongozi kwa karibu, hii ikiwa ni pamoja na kujiunga na chama chochote cha kisiasa hapa nchini. 

MTAZAMO WA MUNGU KUHUSU UTAWALA.

February 5, 2008

Na: Patrick Samson sanga.

Mwanzo 22:17 ‘Katika kukubariki nitakubariki na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamilki mlango wa adui zako”

Siku zote Mungu anapofanya jambo au kitu huwa anafanya kwa kusudi. Mungu ametuumba/amekuumba ili uweze kutawala kila kiumbe kiendacho juu ya nchi. Sasa kwa bahati mbaya sana imefikia mahali kanisa la Mungu limejisahau,limeona kwamba siasa, madaraka na utawala ni dhambi.
Mtazamo wa wengi ambao wachungaji, viongozi wa makanisa na makundi mbalimbali ya kidini wanafikiria kwamba huwezi kuwa mwanasiasa, kiongozi wa serikali halafu kwa wakati huohuo uwe na maendeleo mazuri kiroho.Wanaaamini ukiingia kwenye siasa basi suala la mbinguni kwako ni kitendawili. Na yapo baadhi ya makanisa ambayo tayari yameshapanda mawazo ya namna hii kwa washirika wao. 

Hao hao wenye mawazo ya namna hii ndio wanakuwa wa kwanza kuilaumu serkali iliyopo madarakani mara wanasema rushwa imezidi, haki haitendeki, umaskini haupungui n.k swali ni kwamba wanamlalamikia nani wakati wao wamekataa kugombea nafasi hizo za uongozi na wamewazuia wengine kufanya hivyo na hawawahamasishi wengine kugombea na zaidi hata kadi ya chama chochote cha siasa hawana.  

Lengo la waraka huu ni kukuonyesha kibiblia suala la utawala au uongozi kupitia siasa Mungu analitazamaje.Tutajifunza somo hili kwa kuangalia mambo manne yafuatayo:- 

*Mungu anatumia madaraka ili kuliimarisha agano lake.

Mwanzo17:6-7 “Nitakufanya uwe na uwezo na uzao mwingi sana,nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao,kuwa agano la milele,kwamba nitakuwa Mungu wako na kwa uzao wako baada yako.     Sikiliza siku zote Mungu ili aweze kuimarisha agano lake anatumia madaraka/uongozi.Agano linalozungumziwa hapa ni la Mungu kukaa pamoja na wanadamu.Katika Yeremia 31:33 anasema “ Bali agano hili ndilo nitakalolifanya na nyumba ya Israel,baada ya siku zile asema BWANA, Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu kwao nao watakuwa watu wangu.  

Mungu anapotaka kuimarisha uhusiano wake na watu wake na kuimarisha agano lake ni lazima aweke baadhi ya watu katika nafasi za juu serikalini ili kuweza kuliimarisha hili agano lake. Maana yake anatumia madaraka ili kuimarisha uhusiano wake na watu wake.Ndiyo maana anawaambia Ibrahim wafalme yaani watawala kwa lugha ya sasa,watatoka kwako,maana yake ni hii nitauzidisha na kuubariki uzao wako na ndani yake  watatoka watawala ili kuliimarisha agano langu.       

Mungu alipotaka kuliimarisha agano lake katika kujenga hekalu ambapo watu watakuwa wakija kumuabudu ilibidi amuweke Sulemani kwenye utawala,alipotaka kuyaondoa machukizo katika nchi na kuimarisha uhusiano wake na watu alimweka mfalme Asa kwenye utawala, mwenye sikio la kusikia na asikie. Soma habari hizo katika 1 wafalme 6 na 2mambo Nyakati15. 

*Mungu anatumia madaraka/uongozi ili kulifanya kanisa kumiliki mlango wa adui zao.

Mwanzo 22:17 “katika kukubariki nitakubariki,na katika kuzidisha nitakuzidishia uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani,na uzao wako utamiliki mlango wa adui zako”.  Sikiliza Mungu anayatazama madaraka au uongozi kama nyenzo ambayo watu wake wataitumia kumiliki mlango wa adui zao. Ngoja nikuambie siri hii ya ufalme wa mbinguni. Siasa/madaraka ni mlango. Huu mlango ukikaliwa au kutawaliwa na watu wanaomjua Mungu nakuambia kazi za Ibilisi katika ulimwengu wa roho zitakosa nguvu.Mlango huu huu ukikaliwa na watu wasiomjua Mungu basi kazi za shetani zitapata nguvu.

Je adui zako/zetu ni akina nani au ni nani? Ile Waefeso 6:12 imeweka wazi adui zetu ni akina nani? Neno linasema “kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama,bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”   Sasa falme na mamlaka,wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho ndio adui wa uzao wa Mungu.

Utawala wa mfalme Daudi ni mfano mzuri wa utawala ambao Mungu aliutumia ili kuwafanya Israel kumiliki mlango wa adui zao. Na ndiyo maana Mungu anawaambia Ibrahim nitakubariki na kukuzidisha ili uzao wako uweze  kumiliki mlango wa adui zao. La sivyo uzao wako utatawaliwa kimwili,kiroho na kiuchumi na adui zao. Mwenye sikio na asikie yale ambayo roho waBwana asema na kanisa.  

*Mungu anatumia madaraka ili kuwarithisha watu wake baraka/ahadi  alizowaahidi katika Neno lake.

Yoshua 1:6 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa,maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa”. 

 Ukisoma pia ule mstari wa pili Mungu anawaambia Yoshua, Musa mtumishi wangu amekufa, sasa nataka wewe Yoshua uwe hodari na moyo wa ushujaa maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii, kwa lugha nyepesi Mungu anasema nchi hii/ahadi hii au hizi nilizowaahidi watu wangu hawawezi kuzipokea au kuzirithi bila mimi Mungu kukuweka wewe kwenye utawala.    Sasa kumbuka nimekuambia madaraka ni mlango, Hivyo Mungu atatumia mlango huo kupitishia  baraka zake kwa watu wake kwa yeye kumuweka mtu wa uzao wake.  

*Mungu anatumia/anayatazama madaraka kama njia ya kuliponya taifa lake na watu wake.

 Mwanzo 41:33 inasema”Basi Farao ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri”.Ukisoma sura nzima ile ya 41 utaona habari Farao aliyeota ndoto kuhusu taifa lake la  Misri. Na Yusufu ndiye aliyeweza kutafsiri ile ndoto ya mfalme kwa kumueleza kuwa kutakuwa na miaka saba ya njaa inakuja,lakini kabla ya hiyo miaka saba ya njaa kutatangulia miaka saba ya neema au shibe au wingi wa chakula.

Hivyo mfalme atafute mtu wa akili na hekima amuweke juu ya nchi ili kwa miaka saba ya shibe kikusanywe chakula kitakachotumika katika miaka saba ya njaa.

Na ukiendelea mstari ule wa 34 unasema,Farao akaweka wasimamizi juu ya nchi. Hata sasa hakuna mtu ajuaye kwamba katika nchi yako nini kitatokea baada ya mwaka mmoja au miwili, huenda ni njaa,mafuriko,ukame,Rushwa, kushuka kwa fedha ya nchi yako au uchumi kwa ujumla nk, ni Mungu tu. Sasa ili apate kuliponya taifa na mambo yenye kuleta athari katika uchumi  nchini au hata kwa mtu mmoja mmoja Mungu anamweka  madarakani mtu ambaye ndani yake amebeba neno la kuwavusha  katika majanga hayo bila kuathari Uchumi wa nchi na hivyo kuliponya taifa. 

Naamini baada ya kuwa umesoma ujumbe huu,mtazamo wako sasa kuhusu mambo ya utawala ,uongozi na siasa kwa ujumla utakuwa umebadilika.Nakupa changamoto nenda katika chama chochote cha kisiasa nchini soma sera zao halafu fanya maamuzi ya kujiunga kwenye hicho chama. Usiishie hapo bali pia gombea kila aina ya nafasi kuanzia katika ngazi za chama na kuendelea.

Neema ya Bwana wangu Yesu Kristo na iwe pamoja nawe.