Archive for August 2007

NAMNA YA KUJENGA MAHUSIANO MAZURI NA ROHO MTAKATIFU.

August 17, 2007

Yohana 14:16-17. Biblia inasema “ Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni, wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”. Ukiaangalia vema mistari hiyo miwili hapo juu utagundua Yesu alikuwa akiwaambia wanafunzi wake mambo yafuatayo;Moja, alikuwa akiwaaga na kwa hiyo akawaambia nitamwomba Baba awape msaidizi mwingine ambaye ndiye Roho wa kweli yani Roho mtakatifu.

Mbili, huyo msaidizi ulimwengu hauwezi kumpokea kwa kuwa haumwoni na wala haumtambui.Tatu, wanafunzi wake watampokea kwa sababu kwanza wanamtambua na kisha atakuwa ndani yao. Ukisoma kile kipengele cha mwisho kinasema “Bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”

Sasa leo nataka nizungumzie kipengele cha mwisho kinachosema “naye atakuwa ndani yenu”. Biblia inasema atakuwa, maana yake ni tendo la wakati ujao, au si la sasa au kwa lugha nyingine ni baada ya vitu fulani kufanyika. Roho mtakatifu kukaa ndani yako ni kwa ajili yako wewe binafsi. Hii ina maana atakua ndani yako kwa ajili ya kukusaidia uweze kulitumika shauri la Bwana katika kizazi chako.
Ili Roho mtakatifu aweze kuwa ndani yako na kukuongoza vema katika njia unayopasa kuiendea ni lazima ufanye maamuzi ya ndani ya kumruhusu akae ndani yako kwa kujenga mahusiano mazuri katika maisha yako au kiwango cha yeye kukusaidia katika maisha yako binafsi.Mambo yafuatayo yatakusaidia kujenga mahusiano mazuri na Roho mtakatifu ili akusaidie;

*Kuliweka neno la kristo kwa wingi ndani yako.
Wakolosai 3:16.Hakikisha kila siku unatenga muda wa kutosha wa kusoma na kulitafakari neno la Mungu. Unapolitafakari neno la Mungu, ndivyo jinsi linavyokaa kwa wingi moyoni mwako.

*Kutenga muda wa kuwa pamoja naye.
Jifunze kujenga mahusiano na Roho mtakatifu kama rafiki yao, usimuone kama ni adui. Kumbuka yeye ni msaidizi na bila yeye huwezi lolote. Mara nyingi marafiki wazuri huwa wanakuwa na muda wa kutosha wa kuwa pamoja. Hivyo jifunze siku zote kutenga muda wa kuongea naye kwa maombi na pia kutulia tu ili na wewe usikie kutoka kwake.

*Kutafakari mambo ya Rohoni.
Warumi 8:5bSiku zote jifunze kutafakari mambo ya roho. Kutafakari mambo ya roho ni ile hali ya kutumia muda wako mara kwa mara kutafakari zaidi juu ya Roho mtakatifu na kazi zake na kisha kukaa kwenye mkao wa kusikiliza kila analokuagiza.

*Kuwa mtiifu kwake.
Yesu alipomtambulisha Roho mtakatifu kwa wanafunzi wake aliwaambia moja ya kazi zake itakuwa ni kuwafundisha na kuwakumbusha yale yote aliyowaambia (Yohana 14:26). Sasa kitu cha muhimu kuliko vyote ili kuboresha mahusiano yako na Roho mtakatifu ni wewe kuwa mtiifu kwake kwa kila analokuagiza.

Watu wengi wameshindwa kumpa Roho mtakatifu heshima kisa lile neon linalosema yeye ni msaidizi. Nisikilize kama umesoma mstari wa mwanzo kabisa vizuri utagundua kwamba hata Yesu alikuwa ni msaidizi, Neno msaidizi halina maana yuko chini yako kibiblia. Ina maana unahitaji msaada wake ili uweze kufika unakotakiwa kwenda na bila yeye hutaweza. Hivyo mpe Roho mtakatifu nafasi ile ile uliyompa na Yesu pia.

Asikiaye na afahamu,
  Ndimi Sanga P.S.

NINI MAANA YA KUMPENDA BWANA?

August 17, 2007

Kumbukumbu la Torati 6:5 Nawe, mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote na Pia ile Mathayo 22:37 inasema Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote”. Hivyo basi kwa kutumia hiyo mistari miwili tunaona kwamba mtu anatakiwa kumpenda Bwana Mungu wake kwa;

Moyo wake wote, Roho yake yote, Nguvu zake zote, Na akili zake zote.
Lakini pia ukisoma kile kitabu cha 1 Yohana 5:3 Biblia inasema “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba, tuzishike amri zake, wala amri zake si nzito”. Hivyo basi kumpenda Mungu ni kuzishika amri zake. Sasa kuzishika amri za Mungu ni suala linalohitaji Moyo wako, roho yako, nguvu zako na akili zako vyote kwa pamoja vifanye kazi ya kumpenda Mungu kwa maana ya kuzishika amri zake.

*Kumpenda Bwana kwa moyo wako.
Kumpenda Bwana kwa moyo wako ni kwa kuutafakarisha moyo wako amri za Bwana kwa maana ya maagizo yake unayotakiwa kuyashika. Hii ni pamoja na kutumia muda wako siku zote kuliweka neno la kristo kwa wingi ndani yako kwa kulitafakari. Unapolitafakari neno la Bwana ndipo pia unapopata mawazo na njia za Mungu za kukufanikisha kimaisha. Zaburi 27:4.

*Kumpenda Bwana kwa roho yako.
Hapa unatakiwa kuitafakarisha roho yako neno la Bwana ambalo linazungumzia wakati ujao (future yako) isibishe roho yako ahadi za Mungu ili imani yako iongezeke na uanze kuona mambo ya wakati ujao kana kwamba yapo halisi kwa wakati wa sasa. Hili litakusaidia kuishi kwa Imani, maana siku zote utakuwa unafanya yale yanayompendeza Mungu.

*Kumpenda Bwana kwa nguvu zako zote.
Nguvu ni uwezo alionao mtu katika kufanya kazi fulani. Sasa tumia nguvu zako zote za kimwili za kiufahamu, za kifedha nk katika kutekeleza yale yote ambayo neno la Mungu linakuagiza kila siku unapolitafakari kumbuka nimekuambia katika kulitafakari neno la Bwana utapata mawazo ya Bwana juu yako na ndani ya hayo mawazo kuna mipango na mikakati ya kuitekeleza.

*Kumpenda Bwana kwa akili zako zote.
Vile vile akili ni uwezo wa kiufahamu alionao mtu katika kufanya mambo. Hivyo basi wakati unatumia nguvu kutekeleza maagizo ya Bwana basi hakikisha unatekeleza kwa kutumia akili ili ufanye kitu sahihi, kwa wakati sahihi na kwa usahii.

Neema ya bwana na iwe nawe.
Ndimi katika huduma hii Patrick Sanga.

SABABU ZA KUKOSA UTIIFU MBELE ZA MUNGU.

August 17, 2007

Ndani ya Biblia tunajifunza maisha ya watu mbalimbali ambao kupitia wao, Mungu alifanya mambo makubwa sana katika kizazi chao. Yapo mambo mengi mazuri na makubwa ambayo hawa ndugu waliyafanya na pia kuna baadhi yao ambao walikosa utiifu mbele za Mungu na matokeo yake wakafa kifo cha kipumbavu. Biblia haijanyamaza hata wale ambao walikosea haikuficha makosa yao na dhambi zao, bali Biblia inasema katika kitabu cha 1 Wakorinto 10:11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani .

Hivyo basi hata katika kizazi cha leo, Mungu siku zote anatoa maagizo yake kwa watu wake kupitia neno lake ambayo anataka wayatekeleze ili kwanza waweze kulitumikia kusudi lake katika siku zao na kisha baadae waweze kuurithi uzima wa milele na si kutupwa jehnam ya moto Lakini kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo tunaona wana damu wanazidi kuvunja maagizo ya Mungu na sheria zake, watu wana mdharau Mungu na imefika mahali uovu na dhambi zimezidi na watu wamejisahau kabisa kama kuna Mungu na siku moja watu wote tutasimama mbele za kiti cha hukumu kulipwa haki zetu kila mmoja sawa na matendo yake.

Mbaya zaidi ni pale hata wale ambao wameokoka nao pia wamekosa utiifu mbele za Mungu na matokeo yake wameanza kuipenda na kufuatisha namna ya dunia hii na kwa sehemu inafika mahali hakuna tena tofauti kati ya aliyeokoka na asiyeokoka. Sasa kwa nini mara nyingi tunashindwa kuwa watiifu katika maagizo ya Mungu?
 Naomba tusiwe wepesi kumlaumu Adam na Eva pale bustanini, au Samson kwa Delila au Kuhani Eli au Mfalme Daudi. Biblia katika kitabu cha Isaya 57:11 inasema “Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuwekwa hayo moyoni? Je, mimi sikunyamaza tangu zamani hata huniogopi Ukisoma vizuri huo mstari utaona kuna sababu kubwa tatu ambazo ni :

*Hofu na woga kwa wanadamu wengine .
 Katika kizazi cha leo imefika mahali kwa wakristo wengi nafasi ya Mungu kwa hao wakristo wamechukua wanadamu. Mungu anaweza akamwagiza mtu wake fanya hiki, lakini mtu kwa sababu ya kuogopa je, watu watanielewaje?, au fulani ndiye anayenitunza nikifanya hili je, ataendelea kunitunza nk. Hofu kwa wanadamu na si Mungu imepelekea watu wengi sana kukosa utiifu mbele za Mungu na hivyo kuharibu mahusiano kati ya hao watu wa Mungu wao .

*Kumsahau Mungu
 Dunia hii ya sasa imetengeneza mazingira ambayo kama wakristo hawatakuwa makini watajikuta imefika mahali wazo la kwamba Mungu yupo, halipo tena katika fahamu zao. Shetani amemwaga roho ya kujisahau na kumsahau Mungu kwa Wakristo wengi na kwa sababu hawaoni tena kwamba Mungu yupo, inakuwa rahisi kwao kukosa utiifu mbele za Mungu

*Kutokuweka sheria ya Mungu ndani yako.
Mwimbaji wa Zaburi anasema katika Zaburi 119:11 “Moyoni mwangu nimeliweka neon lako, nisije nikakutenda dhambi” na pia katika Mstari wa 105 anasema “Neno la taa ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu” Sasa kwa sababu wapendwa wengi hawatumii muda mwingi kutafakari neno la Mungu ili likae ndani mwao kama taa katika miguu yao na shetani anatumia hiyo fursa kuwafanya wakose utiifu mbele za Mungu.

Neema ya Kristo iwe nawe siku zote.

MAKOSA WANAYOFANYA VIJANA KATIKA KUTAFUTA MWENZI WA MAISHA.

August 17, 2007

KWA NINI VIJANA WENGI WANAKOSEA KATIKA KUTAFUTA MWENZI WA MAISHA?

Maamuzi ya kuoa au kuolewa, si maamuzi madogo, ni moja ya maamuzi makubwa ambayo vijana wengi wa kike na wa kiume wana kutana nayo kila siku. Sasa katika kufanya maamuzi haya ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya vijana mpaka wafike mahali pa kumpata kijana au binti wa kusema huyu ndiye haswa wa kutoka kwa Bwana, basi ujue tayari wengi wanakuwa walishakosea mara nyingi mpaka kufikia hapo. Wapo ambao wakikosea husema, yule wa kwanza hakuwa chaguo la Bwana, au haukua ufunuo wa Mungu mwenyewe bali malaika, au utasikia mwingine akisema Bwana amemchukia Esau akampenda Yakobo au amehamishia upako wa Sauli kwa Daudi kwa maana ya kwamba upako umehama kutoka binti wa kwanza hadi kwa mwingine. Mimi sina uhakika sana na hizi kauli.
Je hivi kweli hayo ndiyo yalivyo au ni ujanja ujanja tu wa vijana tena hasa wa kiume ndio wenye kauli kama hizi. Lengo la waraka huu mfupi kwako kijana mwenzangu ni kutaka kukueleza sababu kadhaa ambazo kupelekea vijana wengi kufanya makosa katika kutafuta mwenzi wa maisha.

*Wengi wanakuwa tayari wameshafanya maamuzi ya nani ataishi naye.
Vijana wengi huwa wanaomba Mungu awape mtu sahihi wa kuishi naye na wakati huohuo tayari kwenye nafsi yake anakuwa na mtu wake kwamba lazima huyu tu ndiye nitaishi naye. Na kwa sababu hiyo ina kuwa ni vigumu kwao kumpata mtu wa mapenzi ya Mungu na pia ina muwia kazi Mungu kukuonyesha mke au mme wa kusudi lake kwani tayari umeshafanya maamzi ndani yako, je Mungu afanye nini kama sio kunyamaza.

*Sababu za kipepo
Hapa nitaelezea mambo mawili kwa wakati mmoja, la kwanza ni hili kuna vijana huenda wao wenyewe au ndugu zake, wazazi wake walishawahi kumtoa huyo mototo kama dhabihu kwa mapepo kwa sababu ya mila zao au pia alipatikana kwa njia za kipepo. Siri moja ni hii kuna baadhi ya mapepo huwa hayapendi kushare sex na mtu mwingine, hivyo ni lazima yalete kila namna ya upinzani ili mtu asiolewe na wala kuoa. Na mwingine hata kama hakutolewa kama dhabihu lakini huenda pepo wameshawahi kufanya mapenzi na huyo mtu na kama yatampenda basi ujue hayatakubali aolewe au kuoa, hivyo yatamletea kila namna ya upinzani katika kuolewa au kuoa kwake. Mengine hufika mahali hata pa kumwachia kijana wa watu harufu mbaya ili mwingine asimpende.

*Maneno ya kujitamkia
Kuna baadhi na hasa hapa ni akina dada kwa sababu mbalimbali kama vile kubakwa, kujeruhiwa katika nafsi kwa sababu ya kuachwa na mchumba wake hufikia mahali wakasema mimi sitaki tena kuolewa. Sasa inpofika muda umepita na wanataka tena kuolewa wananaza kuomba Mungu awape mume, wakati huo wamesahau kwamba walishatamka kwamba hawataki tena kuolewa. Nisikilize ukisema hutaki kuolewa au kuoa tena, maana yake unaifunga nafsi yako hapo kwamba hutaoa kuolewa, na Biblia inasema mtu atashiba matunda ya kinywa chake. Na wakati huo shetani ni mwepesi kufuatilia maneno ambayo ni ya athari kwako. Sasa bila kufuta kwa Damu ya Yesu ndugu utakesha hapo.

*Dhambi.
Sikiliza Biblia inasema afichaye dhambi zake hatafanikiwa, (Mithali 28:13a). Kuna baadhi ya vijana huwa wanakuwa awali kuna baadhi ya dhambi wamezifanya na hawajazitubia, na bado wana taka mtu awaoe au wa kumwoa. Biblia iko very clear kama kuna dhambi umeficha hutafanikiwa, sasa inategemeana, lakini pia inahusiana sana na kutofanikiwa kwako pia kumpata hata mwenzi tu. Nikupe mfano mara nyingi watu wanatoa mimba, au watoto wanaozaa, nao pia kupata mume au mke huwa inakuwa kazi kweli kweli.

*Kutokuenenda kwa Roho.
Paulo anasema, “Basi nasema enendeni kwa roho wala hamtatimiza kamwe tama za mwili” (Wagalatia 5: 16). Kuenenda wa Roho maana yake ni kuongozwa na Roho Mtakatifu, hii ni pamoja na zoezi zima la kutafuta mke au mme. Sasa kwa sababu wewe unaenda kwa mwili, mara eti nataka mtoto portable, mguu wa chupa, mweupeee, nk. Hivyo vitu unavyotaka wewe kuna wengine pia wanataka hivyohivyo na matokeo yake mnaanza kugombaniana msichana au mvulana kwa sababu tamaa za miili yetu zinawaongoza huko.

*Kuwa na vigezo binafsi.
 Vijana wengi sana katika suala zima la kupata mke ua mme, ukweli wengi wao wana vigezo vingi sana ambavyo kila mmoja angependa huyo mchumba wake awe navyo. Utasikia lazima awe wa kabila ya kwangu, awe portable, mweupee, mrefu ndio mzuri, ajue kutabasamu na kisha awe ana ulamba. Sawa mi sikatai hivyo vigezo, lakini nikuulize swali Je! Unayajua mawazo ya Mungu kuhusu wewe kwa habari ya mkeo au mmeo? Je kibiblia hivyo vigezo vyako vinakubalika/ na je mke/mme mtu huchagua mwenyewe au hupewa na Bwana?
 Najua utaniambia mimi nitaomba Mungu anipe mke/mme mwenye sifa hizo. Ok. Ukiniambia hivyo na mimi nitakuambia kumuomba Mungu kwa muundo huo ni nzuri kabisa, wala sio dhambi lakini kumbuka maandalio ya moyo ni ya mwanadamu lakini jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana. Na hapo ndipo patamu, wengi huwa wanaomba kwa vigezo vyao, na mara nyingi Mungu anapojibu inakuwa tofauti na vigezo vyao, na hapo wengine wanakataa hata chaguo la Bwana wanabakia kuteseka. Jua kwamba wewe unapoweka vigezo vya mwenzi wako na Mungu naye ana vigezo vya aina ya mwenzi anayekufaa.

* Kufanya maamuzi kabla ya wakati.
Biblia inasema katika Mhubiri 3:1 “kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu”.Hili ni jambo la kawaida, hata wakati wa uchaguzi kura mtu harusiwi kupiga kama hajafikisha miaka kumi na nane kwa nchi nyingi. Vivyo hivyo hata suala la kutafuta mke au mume lina wakati wake maalumu. Ukitaka kulifanya nje ya kipindi ambacho Mungu amekipanga kwa ajili yako utateseka hadi uchoke. Kumbuka kila mtu ana muda wake, hivyo basi hakuna muda maalumu wa kila mtu kuanza kutafuta mke au mme, bali kila mtu ana muda wake na mara tu unapowadia Mungu humjulisha mtu wake.

Nisikilize ukiulekeza moyo wako upate kujua haya nisemayo na ukajizuia kufanya makosa kama haya, basi nataka nikuhakikishe suala la kupata mke au mme wa kutoka kwa Bwana litakuwa ni jepesi sana,ni sawa sawa na kuombea chakula na ukishafumbua macho ukaanza kula moja kwa moja ukiwa na uhakika kimeponywa na kubarikiwa.

Ndimi katika huduma hii,
Sanga P.S.

 

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOFANYA HUDUMA.

August 17, 2007

Na:Patrick Sanga

Kama Mungu amekuita umtumikie kwa kusudi fulani hapa chini ya jua, na pia amekupa huduma ambayo ina kulazimu uwe ni mtu wa kuingiliana na watu kwa maana ya kuwafundisha na kuwashauri. Na pia kama wewe ni mchungaji, au ni kiongozi katika kundi lolote lile la kiroho basi yapo mambo machache ambayo napenda nikutahadharishe wakati wa kutekelezeza wajibu wako kama kiongozi na mtumishi wa Mungu katika kundi lako.
Labda niseme maadamu wewe ni kiongozi, huwezi kukwepa kuishi bila kuingiliana, kuhusiana na kushirikiana na makundi ya watu wengine kama ni kanisani, shuleni, kazini. Sasa kwako wewe kiongozi, mchungaji, au mtumishi nk, uliyeokokoka yafuatayo ni mambo ya msingi kuzingatia wakati unapoishi kwenye jamii au kundi la watu unaowaongoza.

*Nafasi unayowapa watu wengine katika maisha yako.
Jifunze kuangalia Je, ni nafasi gani na ya aina gani? Unayowapa wale unaowaongoza kila siku. Hili jambo limepelekea wengi kufanikiwa katika huduma zao na wengine kuangamia kabisa. Ninapozungumzia nafasi namaanisha hao watu wana sehemu gani kwako, unawahesabu kama kina nani? nk. Je katika moyo wako wana nafasi ipi kwako na wewe una nafasi ipi ndani yao?.
Na je, Mungu pia ana nafasi gani kwako na kwao. Nisikilize mtumishi mwenzangu, nafasi ya Mungu ndani yako ikichukuliwa na wao na ndani yao ikichukuliwa na wewe, ni rahisi sana kwako kuanguka na hao washirika wako au na yule ambaye itamtokea hali hiyo.

*Tafsiri uliyo nayo juu ya watu wengine.
Pili je ni mahusiano gani uliyoyajenga baina yako na hao washirika wote kwa ujumla au mmoja mmoja. Mahusiano unayojenga ndiyo yanayokujengea pia tafsiri yako kwao na tafsiri yao kwako. Jihadhari tafsiri hiyo isipelekee ninyi kupotea. Ninapozungumzia tafsiri nina maana je wao wanakuhesabu vipi, wanakuita na kukuona wewe kama nani?, rafiki yao, mchungaji au kiongozi kwao, mshikaji wao, mpenzi, mchumba wao? nk. (Haya yapo kwa baadhi ya watumishi).

*Muda unaowapa hao watu wengine.
Je, mara kwa mara muda wako unautumiaje na watu wako au baadhi ya washirika wako. Mtu yoyote unayempa muda wako mwingi jua kabisa kati yenu kuna aina fulani ya mahusiano yanajengeka. Sasa uwe makini na muda na hayo mahusiano yatakayoanzishwa hapo kwani huenda yakazaa mafanikio kihuduma au kifo chako kiroho na kihuduma. jifunze kutumia muda vema ili uweze kuhudumia washirika wote na pia uwajue vizuri.

*Uhuru/mipaka unayoijenga kwa hao unaowaongoza.
Je unapokuwa na washirika au mshirika wako, ni mipaka gani au ni uhuru gani umeujenga baina yenu wakati unawaombea, unawafundisha, unawashauri nk. Je huwa unakuwa mazingira gani wakati unafanya huduma kama hizo, Je wana uhuru wa kukutania wanavyotaka?. Na je nje ya huduma ni habari gani huwa mnazungumzia mara kwa mara, Je kuna baadhi yao huwa unatoka nao out kupata chakula au la. Uwe makini ndugu shetani in mwerevu kuliko unavyofikiri. Lazima ujifunze kuweka mipaka/kanuni/taratibu zitakazokuongoza katika huduma yako.

*Upendo unaowaonyesha hao unaowaongoza.
Zipo aina nyingi za upendo au mapenzi unazoweza kama kiongozi kuonyesha kwa watu wako. Je ni upendo gani huwa unawaonyesha na upendo/mapenzi gani unayapata kutoka kwao. Je mnapendana kama ndugu katika Kristo au mnapendana kama wapenzi wa kidunia.  Na hapa matendo yenu ndiyo yatakayothibisha hili. Ukiona aina ya mapenzi yanayoendelea kwako ni ya kidunia tambua kwamba kumekucha, vaa silaha mwanangu ili nafsi yako isije ikaangamizwa.

Hapa nimeandika kwa kifupi sana, lakini nakusihi mtumishi mwenzangu, mambo haya tunayoona madogo ndiyo yamewangamiza kiroho viongozi na watumishi wengi sana. Ukitaka kuthibitisha chunguza mwenyewe katika eneo lako watumishi walionaguka katika dhambi yoyote ile na si uzinzi tu chanzo chake nini, kama si hayo hapo juu. Hivyo  inapofika suala la mahusinao ya kiongozi na wanachama mipaka kimahusiano ni muhimu.

Naamini mambo haya machache yatakusaidia katika utumishi wako.

Neema ya Bwana Yesu na iwe nawe siku zote.