Archive for February 2007

JINSI YA KUENENDA KWA ROHO.

February 6, 2007


Patrick akifundisha
 

Na; Patrick Samson sanga.Wagalatia 5:16 “Basi, nasema enendeni kwa Roho, wala hamtatimiza kamwe tamaa za mwili”Hapa tunaona Paulo anawaagiza wagalatia kwamba waenende kwa Roho na lengo kubwa ni ili wasizitimize tama za mwili.

Lengo la waraka huu mfupi ni kukueleza namna unavyoweza kuenenda kwa Roho, na hii ni kwa sababu Yesu  mwenyewe alisema ni heri mimi niondokeili aje mwingine msaidizi huyo Roho wa kweli. Na
kama tunaye Roho mtakatifu ni lazima tujue ni kwa namna gani tutaenenda kwa roho?Neno la Mungu/ Mungu anaposema, enendeni kwa Roho ana maana hii:- 

(a)            Kila unalolizungumza, lizungumze chini ya uongozi wa Roho mtakatifu. Yohana 12:49-50. Yesu mwenyewe hakunena neno lolote kwa shauri lake, bali kila ambalo baba alimwambia kupitia Roho mtakatifu. Hivyo hata wewe
kama unafundisha, unahubiri, unaonya hakikisha unachokisema Roho mtakatifu ndiye amekuruhusu ukiseme. Usiseme kitu cha kwako halafu ukasema Roho mtakatifu amekuongoza.

(b)            Tii uongozi wake .Yohana 16:13 “ lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli; atawaongoza awatie kwenye kweli yote…….” Moja ya kazi za Roho mtakatifu ni kutuongoza na kututia kwenye kweli yote. Hivyo kuenenda kwa Roho maana yake ni kutii katika yale anayotuambia maana hata yeye haneni kwa ridhaa yake isipokuwa yale anayoyasikia kutoka kwa Mungu. 

(c)             Jifunze kuyafikiri mambo ya Roho wa Mungu. Warumi 8:5b “
Bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho”Kuenenda kwa roho kunajumuisha kukaa chini na kuanza kutafakari mambo/kazi za Roho mtakatifu. Vile jinsi utendaji wake ulivyo, karama zake, vipawa, tunda la Roho na vile jinsi anavyofanyika msaidizi katika maisha yako.

(d) Kuliishi tunda la Roho.Wagalatia 5:22 “lakini tunda la Roho ni upendo, Furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi………”Sikiliza ukijifunza au kadri unavyoishi maisha yaliyojaa upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi ndivyo unavyokuwa umejiweka kwenye mkao wa kuongozwa na Roho au ndiko kunaitwa kuenenda kwa Roho. 

 (e) Kwa kuyakataa na kuyafisha/vunja matendo ya mwili katika maisha yako. Wagalatia 4:28-31 ule mstari wa 30 unasema” Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa muungwana”Biblia inapozungumzia kumfukuza mjakazi pamoja na mwanawe ina maana ya kuyafukuza, kuyapinga, kuyaondoa, kuyafisha, kuyaharibu matendo ya mwili katika maisha yako ambayo yametajwa katika. Wagalatia 5:19-21 ikiwa ni pamoja na uasherati, ulevi, husuda, uadui, ugomvi, uchafu, ufisadi nk.Naamini baada ya ujumbe huu utaanza kuenenda kwa Roho na kuomba msaada wa Mungu katika maisha yako kwenye eneo hili..

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nawe.

KWA NINI UNATAKIWA KULITAFAKARI NENO LA MUNGU USIKU NA MCHANA?

February 6, 2007

 

Vjana wakijadiliana. 

  Na; Patrck samson Sanga.

Yoshua 1:8 “kitabu hiki cha Torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo……..)

Hapa tunaona jinsi Mungu alivyomtisitiza Joshua kwa habari ya kulitafakari neno la Mungu usiku na mchana .

Lengo la waraka huu mfupi kwako mpendwa msomaji ni kukueleza sababu za msingi kwa nini ni lazima na sio ombi kwamba usome na kulitafakari Neno la Mungu usiku na mchana.Kabla sijakueleza sababu nikupe tafasiri ya Neno la Mungu kwa ufupi, neno la Mungu ni jumla ya mawazo ya Mungu juu ya mwanadamu.

Ndani ya Neno kuna maamuzi (hukumu), sheria, maagizo na njia za Mungu za kumtoa mwanadamu katika shida aliyonayo, kumfanikisha katika mambo yote na kumsaidia, kuishi kwa kulishika shauri (kusudi) la Bwana.

Sababu hizo ni ;

(a) uweze kuelewa nini mawazo ya Mungu juu yako .
Katika kitabu cha Yeremia 29:11 Mungu anasema nayajua mawazo ninayokuwazi si mawazo mabaya ………, sasa ili uweze kuelewa Mungu anakuwazia nini ni lazima usome kwa kulitafakari neno lake ili upate anachokueleza kuhusu maisha yako, huduma, kazi, biashara nk.

(b) upate kuifanikisha njia yako.
Yoshua 1:8b. Mungu anasema nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea ………….( Zaburi 32:8), kumbuka kila mmoja ana njia yake ya kupita ili kilitumikia shauri la Bwana. Sasa ili uweze kufanikiwa katika njia yako ni lazima usome na kulitafakari Neno la Mungu maana ni taa ya miguu yako. Zaburi 119:105.

(c) usimtende Mungu dhambi .
Zaburi 119:11. mwimbaji wa zaburi anasema, moyoni mwangu nimeliweka neno lako ili nisikutende dhambi. Neno linawekwa moyoni kwa kulitafakari. Kadri unavyolitafakari kimapana ndivyo linavyokusaidia na kukulinda na dhambi. Litakuonyesha hila na mitego ya dhambi ya shetani, na litakupa ushindi kwa kila ushawishi wa adui.

(d)Ili uongezeke kiimani.
 warumi 10:17. Ikiwa chanzo cha Imani ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la kristo, maana yake kadri unavyolisoma na kulitafakari Neno la kristo mara kwa mara, kisha ukajitamkia mwenyewe ili ulisikie hii ina maana lazima imani yako itaongezeka tu.

(e)Neno limebeba jibu la mahitaji yako.
 Zaburi 107:20. kwa kuwa ndani ya neno kuna mawazo na njia (mikakati) ya kukufanikisha kimaisha, hii ina maana, unapolitafakari licha ya kuelewa mipango ya Mungu juu yako, pia utaelewa na njia za Mungu za kukuondoa katika shida uliyo nayo kiroho, kimwili, kindoa , kibiashara nk.

(f)uweze kustawi sana .
Yoshua 1:8b, Biblia inapozungumzia kustawi ina maana ya kutawala na kumiliki vema, kimapana yale ambayo Mungu ameyaweka chini yako .Mtu ambaye ndani yake amejaa Neno la Mungu kwa wingi huyo ana uwezo mkubwa sana wa kutawala na kuongoza watu pia.

(g)Litakupa miaka mingi duniani . Mithali 3:1. Ukilitafakari Neno la Mungu katika maisha yako.Neno litakupa miaka mingi ya amani (mafanikio) hapa duniani na kila ulifanyalo litafanikiwa.

(h)uwafundishe wengine kumjua Mungu.
 kumbukumbu 6:1-10. Mungu anataka watu wamjue yeye, kwa hiyo pindi unapotafakari anajifunua kwako, akajifunua kwako anataka uwaambie na wengine jinsi alivyo na ukuu wake ili wasimsahau yeye

Naamini baada ya kuwa umejua umuhimu wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu usiku na mchana, utaamua kuanza pia kulisoma na kulitafakari usiku na mchana.

KWA NINI TATIZO LA FEDHA LIMEKUWA SEHEMU YA MAISHA YA WAKRISTO?

February 6, 2007

Na: Patrick Samson Sanga. 

Biblia imeshaweka wazi katika Yerema 29:11 na 3 yohana 1:2 kwamba mawazo aliyonayo Mungu juu yetu ni mawazo/mipango ya kutufanikisha, si hivyo tu bali anataka tufanikiwe katika mambo yote. Pia tunajua kwamba fedha na dhahabu ni mali ya Bwana si hivyo tu bali sehemu kubwa ya Biblia imejaa ahadi za Mungu za kutufanikisha kifedha na mafundisho mengi ya pesa.

Sasa licha ya haya yote na ukweli kwamba tumemwamini huyu Yesu lakini bado maisha ya mkristo mmoja mmoja, wakristo wengi, kanisa kwa ujumla, kwaya, makundi ya kiroho na huduma mbalimbali hali yake ya kifedha ni ngumu. Kila mtu analalamika juu ya pesa, mpaka imefika mahali tatizo la fedha limekuwa sehemu ya maisha.

Mikutano, semina tumeshindwa kufanya kisa fedha, vijana wameshindwa kuoa kisa pesa, kwaya hazirekodi kisa fedha. Kitu gani kimetokea kwa wakristo. Wazungu wanasema “Something must be wrong some where” maana yake lazima kuna kitu hakijakaa sawasawa mahali fulani.

Kusudi la waraka huu mfupi ni kukuelezea sababu ambazo zimepelekea tatizo la fedha kuwa sugu na kwa sehemu ya maisha kwa wakristo wengi. Sababu hizo ni ;

Moja, kukosa maarifa (mafundisho) ya kutumia fedha ki-Mungu.
 Hosea 4:6a Fedha ina kanuni zake za matumizi. Hivyo kushindwa kujua kanuni hizo na namna ya kuzitumia hizo fedha ki-mungu basi tatizo litaendelea kuwapo.

Mbili, matumizi ya fedha ya Mungu nje ya kusudi lake.

Hagai 2:8, Sikiliza fedha ni mali ya Bwana, hata ikiwa mikononi mwako bado ni ya Bwana, hivyo ni lazima itumike kwa mapenzi yake, maana kila pesa anayokupa ndani ina kusudi fulani au anakupa kwa lengo fulani.

Tatu, Roho ya mpinga kristo inafanya kazi ndani ya fedha.
 2 wathesalonike 2:7, sikiliza, shetani anajua ukiwa na fedha yeye atakuwa na hali ngumu sana maana utaituma hiyo fedha kuimarisha agano la Bwana, hivyo ameweka Roho ya mpinga kristo ndani ya fedha ila kupinga  fedha isiende kwa watu wa Mungu ili washindwe kumtumikia Mungu.

Nne, kukosa nidhamu katika matumizi ya fedha.

Tito 3:14 Watu wengi hasa waliokoka, hawana nidhamu katika matumizi ya fedha pindi inapofika katika mikono yao. Hawana malengo mazuri katika mtumizi ya fedha na kwa sababu hiyo wanajikuta fedha wanayoipata inatumika kienyeji na kwa sababu hiyo tatizo la fedha lina baki palepale.

Tano,Ufahamu mdogo wa Neno la Mungu kuhusu fedha.
 Wakristo wengi sana wanayo mistari mingi sana inayozungumza uponyaji na kutoa mapepo, na hata imani yao imeongezeka kwenye maeneo hayo. Lakini kwenye eneo la pesa ufahamu wao ni mdogo sana, si wengi wanaopata mafundisho katika nyanja ya fedha ya kutosha.

Sita, Kuwategemea wanadamu na si Mungu .
Katika Yeremia 17:5 Mungu ametoa ole kwa wale wanaowategemea wanadamu.Hii pia imekuwa sababu kubwa sana ya tatizo la pesa kuwa sugu. Ni kweli watu wanamuomba Mungu awabariki, lakini mioyo yao inawategemea wanadamu na tayari ole imeshatiliwa kwa mtu anayemtegemea mwanadamu ki-mafanikio.

Mwisho, ni vifungo na laana za kifamilia, kiuokoo, kitaifa nk.

 Kwenye eneo la pesa, kuna baadhi ya watu wamefungwa wasifanikiwe kifedha katika ulimwengu wa kiroho. Hili ni tatizo la kiroho zaidi na pia wengine ni laana zinazotokana na kushindwa kulijua neno la Mungu. Soma kumbukumbu 28:15-60.

Ni maombi yangu kwamba Mungu akusaidie kuwa na mahusiano mazuri na yeye hasa kwenye eneo la fedha ili uone baraka zake.

NAMNA IMANI INAVYOWEZA KUFANYIKA MSAADA KATIKA MAISHA YAKO.

February 6, 2007

  Na; Patrick Samson Sanga.

Waraka wa Februari. Siku zote neno la Mungu linasema katika 2Petro 5:7 kwamba siku zote Mungu anajishughulisha na mambo yetu/mahitaji yetu ya kila siku. Yapo mahitaji mbalimbali ya kiroho, kiuchumi, kindoa, kimahusiano nk. Ambayo tunahitaji kuona tunafanikiwa vema. Katika kujishughulisha na mahitaji yetu, Mungu ametupa imani ili itusaidie kuunganisha/kutengeneza njia kati ya haja tulizonazo na msaada wa Mungu.

Lengo la ujumbe huu mfupi ni kukuelezea tafsiri fupi ya Imani, makundi matatu ya imani na kisha namna hiyo imani inavyoweza kufanyika msaada katika maisha yako. Katika kile kitabu cha Waebrenia 11:1 Biblia inasema, Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Katika hii tafsiri kuna mambo makubwa mawili kama siyo matatu yamezungumziwa kwanza ni kuwa na hakika, na pili ni ya mambo yatarajiwayo; katika haya yatarijiwayo yapo yasiyoonekana
 Makundi ya imani

(a)Imani katika yale ambayo Mungu amekueleza au amekuagiza.


Hili ni kundi la kwanza la Imani; na imani hii inakuja kwa kuamini yale ambayo Mungu anakuagiza kuyafanya. Mfano Ibrahimu alipoambiwa aende nchi ya ugenini. Mwanzo: 12 yote na pia Nuhu alipoagizwa aitengeneza safina.

(b) Imani unayojiumba/unayoiumba ndani yako kutokana na ahadi za Mungu juu yako.


Imani hii inakuja kwa wewe kuwa na ufahamu fulani kuhusu ahadi za Mungu na kwa sababu umezisikia hivyo ndani yako unatengeneza Imani yenye matendo itakayokupa kila kilichobebwa ndani ya ahadi. Eg. Mfano wa mwanamke mwenye kutoka damu. Marko 5

(c)Imani katika ahadi za Mungu .


Imani hii inakuja kwa wewe kuamini tu kile ambacho Mungu amekisema katika Neno lake kama ahadi kwako. Mfano Imani ya sara, kwamba atapata mwana hata katika uzee wake .

Namna Imani inavyofanyika msaada:

Imani yoyote ile siku zote ina matendo yake, na si hivyo tu bali imani hufanya kazi kwa kushirikiana na matendo yake. Chanzo cha Imani yoyote ile ni kusikia, sasa Imani katika Kristo inakuja kwa kusikia habari za kristo, Imani katika Jina la Yesu, Damu ya Yesu, Roho mtakatifu nk. Inakuja kwa kusikia habari za kristo, Imani katika Jina la Yesu, Damu ya Yesu, Roho mtakatifu nk inakuja kwa kusikia habari za jina la yesu, Damu ya Yesu, Roho Mtakatifu nk.

Hivyo kwanza ili uone imani ikikusaidia jifunze kujisemea kile unachokisoma  ili usikie neno la Mungu linalozungumza eneo unalohitaji msaada Mfano, Biashara, ndoa, Huduma nk. Imani inaumbwa kwa wewe kujisemea kile unachoamini.
Hivyo uzao wa Imani ni sawasawa na kile ulichosema (ulichoamini) + matendo yake .

 Ukitenda tendo au matendo kinyume na kile ulichoamini au kusema bali imani hiyo haiwezi kuzaa. Isipozaa basi ujue huenda imani hiyo imepungua au matendo uliyoyatenda ni kinyume na ulichoamini, yaani umekosea kwenye matendo. Una imani nzuri lakini matendo ya hiyo imani hayasaidii kuzaliwa kwa kile ulichokisema.

Naamini sehemu hii ya kwanza kuhusu imani itakusaidia kujua namna imani inavyofanyika msaada katika maisha yako ya kila siku.

Ubarikiwe.

JE, MAAMUZI YA NANI ATAKUWA MWENZI WAKO WA MAISHA NI YA MUNGU AU YA KWAKO?

February 6, 2007

 Na: Patrick Samson Sanga.

 Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; bali mke mwenye busara mtu hupewa na Bwana”.

Ni matumaini yangu kwamba u-mzima kijana mwenzangu na una maendeleo mazuri kiroho na kimwili. Katika waraka huu mfupi kwa vijana nataka kujibu swali hili ambalo vijana wengi wamekuwa wakijiuliza. Wengine kutokana na kutojua ukweli wake wamejikuta wakifanya maamuzi ambayo hadi leo wanayajutia .

Kibiblia, tunajua kabisa ni mpango wa Mungu tuweze kuoa au kuolewa. Sasa swali linakuja, je ni lazima Mungu anionyeshe, anipe mke au mume wa maisha yangu? Kwani mimi kijana sina uwezo wa kuangalia mtu kisha nikaomba Mungu na mwisho nikajichagulia mwenyewe? Au kifupi maamuzi ya nani atakua mume/mke wangu ni ya nani?

Hili ni swali ambalo vijana wengi limekuwa likiwachanganya. Wengine wanaamini maamuzi hayo ni ya Mungu kunipa mke/mume na wengine wanaamini Mungu hahusiki, bali wao ndio wenye nafasi na wanaohusika. Sasa hayo ni mawazo yao wala mimi sitaki kuyapinga lakini ngoja nikuonyeshe Biblia inasema nini halafu utajua ukweli ni upi:-

Kwenye kitabu cha Mithali 19:14 , Mungu anasema suala la nyumba, mashamba, maduka na vyote vifafanavyo na hivi nimewapa uwezo na ruhusa wazazi wako baba & mama) wa mwili wakupe lakini suala la mke au mume mwenye busara mimi pekee ndiye ninaye wajibika kukupa .Sikiliza kama unataka mke/mume kwa ajili ya kulitumikia kusudi la Mungu alilokuumbia basi huna budi ni lazima upige goti kuomba na kisha ungoje Mungu akuonyeshe/ akupe mke/mume wa kusudi lake.

Vijana wengi wanafikiri eti kwa sababu wameokoka, na wamejzwa roho mtakatifu basi wanao – uwezo wa kujichagulia mke/mume wa kuishi nao. Sikiliza kama una amini umeumbwa kwa kusudi la Mungu na unataka kutembea katika njia yake basi mruhusu Mungu akupe mke/mume mwenye busara ya kukaa na wewe.

Mke au mume ana sehemu kubwa katika maisha yako. Anaweza akabadilisha maisha yako, ya kiroho, kiuchumi, kimwili, kihuduma na kima husiano na watu wengine.Hivyo kibiblia maamuzi ya nani atakuwa mkeo au mumeo ni ya Mungu na si ya kwako. Hii ina maana ukimuomba Mungu hakika atakuletea mtu halisi wa kukaa na wewe. Lakini maamuzi ya kumkubali au kumkataa ni ya kwako na si ya Mungu. Ukikubali shauri la Bwana litatumikiwa, ukimkataa, umejikaribishia laana.

Zifuatazo ni sababu za msingi zinazomfanya Mungu akuchagulie/akupe mke/mume na sio kukuruhusu wewe/wazazi/ukoo wako/mchungaji wako kukuchagulia mke.

(a)Kusudi la uumbaji (kuwaunganisha) .
Sikiliza hakuna mtu aliyeumbwa kwa bahati mbaya, Mungu ndiyo aliyekuchagua na siyo wewe uliyemchagua na akakuweka duniani ili umtumikie sasa yeye ndiye anayejua nikimuunganisha huyu kaka na yule dada watalitumikia kusudi langu.  Warumi 8:28-29.  Mungu anapofanya maamuzi anafanya kwa kuangalia kusudi lake na muda na wahusika wa hilo kusudi. Yeye ni Mungu na anafanya kwa utikufu jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie na si ya kwako.

(b) Mungu ndiye ana-fahamu nani mwenye busara ya kukaa na wewe.
Mithali 19:14b Busara ni uwezo uliomo ndani ya mtu (mke/mume) unaomsaidia kujizuia kufanya jambo ambalo liko nje ya mpango/mapenzi ya Mungu kwa kufanya lile lilio katika mapenzi ya Mungu.Hivyo Mungu pekee ndiye anaye mjua mke/mume mwenye busara ya kukaa na wewe, kamwe wewe hutaweza mjua bila uongozi wa Mungu.

(c) Sababu za ki-Agano.
Zaburi: 32:8 Siku uliyofanya maamuzi ya kuokoka maana yake uliyakabidhi maisha yako kwa Yesu, ukamwambia nafungua moyo wangu uingie uyatawale na kuyaongoza maisha yangu sasa hilo ni Agano lako kwa Mungu. Kwa sababu hiyo Yesu anawajibika kwako kukufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, hii ikiwa ni pamoja na kukupa mke/mume wa kukufaa.

(d)Mawazo yake, si mawazo yako.
Isaya 55:8 Sikiliza Mungu anayo mawazo (mipango) na njia (mikakati) ya kukufanikisha kimaisha. Sasa katika kutekeleza mipango yake kwako na kupitia wewe lazima atumie mikakati yake ili kutekeleza mawazo yake. Sasa moja ya mikakati yake ni kukupa mke au mume wa kusudi lake .
Sasa, sikatai huenda kwa jinsi ya mwili ni kweli huyo mtu anayekupa Mungu ana upungufu fulani. Huenda umbile lake, sura yake, kabila lake, rangi yake, dhehebu lake, haliko
 kama ulivyo kuwa unavyotaka wewe. Mungu anakupa mke au mume kutokana na sababu hizo ambazo nimekuekezea hapo juu na ninakuhakikishia ukimkubali atakupa neema ya kukaa naye huyo mtu na kukufanya uridhike naye na kumpenda huyo mwenzako .

Nakutakia uongozi wa Mungu katika eneo la maamuzi ya nani atakua mumeo au mkeo .