Archive for November 2006

JINSI YA KUJUA MAWAZO YA MUNGU YA KUKUONDOA KWENYE SHIDA ULIYO NAYO.

November 27, 2006

Na: Patrick Sanga.

Kile kitabu cha Yoshua 1:8 Biblia inasema” kitabu hiki cha Torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo, maana ndipo utakapoifanikisha njia yako; kisha ndipo utakapostawi sana 

Kwenye kile kitabu cha Yeremia  29:12, tumeona mawazo ya Mungu kwetu ni mawazo ya amani (kutufanikisha) tena ni yenye kutupa tumaini siku zetu za mwisho. Siku zote mawazo ya Mungu juu yako familia yako, kazi yako, kanisa lako, nchi yako, Biashara yako, ni  mazuri, anawaza kukufanikisha. Tatizo kubwa linalowakabili watu wengi ni kwamba moja hawaelewi nini mawazo ya Mungu juu
yao na hata 
kama wanajua kugundua mikakati ya kutekeleza hiyo mipango ni shida.  Mawazo ya Mungu ya kukufanikisha na njia zake pia yamo ndani ya neno lake. Musa alipokufa Mungu alikuwa amemuandaa Joshua ili kutekeleza Neno lake/kusudi lake la kuwafikisha wana wa
Israel kwani tunaona katika ile Joshua 1:8, Mungu anamsisitiza Joshua kwa habari kuhakikisha kila siku Joshua anasoma ile Torati, anatafakari anachosoma na kukitendea kazi ndipo atakapofanikiwa na kustawi
sana. 

Kwa lugha nyepesi Mungu alimwambia Yoshua kufanikiwa kwako na kustawi kwako katika njia unayoindea kunategemea
sana bidii yako katika kulitafakari na kulitenda neno langu usiku na mchana. Tumeona kwamba Mungu ndiye mwenye mawazo ya kutufanikisha na kutuondoa kwenye shida tulizo nazo. Sasa kwa namna gani tutaelewa hayo mawazo, ni kwa njia zifuatazo. Moja: kwa kulisoma, kulitafakari na kulitenda neno la Mungu kila iitwapo leo. Sikiliza, Biblia ni kitabu kilichokamilika ndani yake kimebeba kila namna ya mawazo na njia za Mungu za kukufanikisha, ndani yake kuna mawazo ya kibiashara, kisiasa, kiuchumi (kifedha), kimahesabu, kimahusiano, kiroho, kindoa, kikanisa n.k. kwa lugha nyepesi hakuna shida, tatizo litakalokukabili wewe ambalo jibu lake halipo kwenye Biblia au tunaweza kusema Jibu la kila shida ulionayo lipo kwenye neno la Mungu (Biblia). Sasa ni jukumu lako wewe kutafakari kila siku na kuhakikisha unajifunza neno

lake
na kuyaweka kwenye matendo yale unayojifunza. Mfano: kama wewe ni mwanasiasa na unataka kufanikiwa kisiasa basi ndani ya Biblia kuna ahadi nyingi na mistari mingi inayozungumizia mambo ya siasa, soma tafakari weka kwenye matendo nakuambia utakuwa mwanasiasa wa aina yake, yamkini wewe ni mfanya biashara nakuambia ndani ya Biblia kuna mistari mingi sana inayozungumzia mambo ya biashara, jukumu lako ni kuomba uongozi wa Roho mtakatifu katika kusoma na ktafakari neno lake. Kwa hiyo Mungu anakushirikisha mawazo yake kwa njia ya neno lake. 

Nimalizie kwa mfano huu huenda wewe ni mchungaji mwalimu au kiongozi wa kikundi fulani cha kidini, sikiliza ndani ya Biblia kuna mipango mingi na njia nyingi
sana za namna ya kuchunga au kuongoza hao watu, namna ambavyo kanisa au kundi lako linaweza likaongezeka kiroho, na kiidadi pia. Namna kanisa lako linaweza kufanyika baraka pale ulipo na uchaotakiwa kufanya ni kusoma hiyo Biblia yako kwa jicho la  kutafakari unachokisoma na kuweka kwenye matendo misitari unayoipata. Jifunze kanisa la kwanza lilifanya nini. Pili: unaweza ukaelewa mawazo ya Mungu kwa kusoma vitabu mbalimbali vya watunzi mbalimbali vinavyozungumza habari za yale yanayokutatiza. Lakini viwe katika mpango wa Mungu, yaani mawazo yake mle ndani yawe ni mazuri, sio yawe ya kukuongoza utumikie njia ambazo unajua hazimbariki Mungu. Wewe kama ni mfanyabiashara jifunze mfumo wa uchumi wa sasa, usome njia na mazingira ya kiuchumi tendea kazi, soma vitabu vya aina zote maadamu mawazo ya mle ndani yanakuongoza katika njia bora za kutekeleza; kwa hiyo njia ya pili ni vitabu vya aina mbalimbali. 

Tatu: unaweza kupata mawazo ya ki-Mungu ya kukuondoa kwenye shida ulionayo kupitia watu wengine ambao unajua wamefanikiwa katika eneo ambalo wewe linakusumbua; tafuta mtu unayejua amefanikiwa katika eneo  ambalo unataka kufanikiwa si lazima awe ameokoka japo kuna baadhi ya shida ni lazima uwaone watu waliookoka hasa zinazohusiana na mambo ya kiroho. 

Nne: kupitia semina, mikutano na mafundisho mbalimbali yanayofanyika katika eneo ulilopo au nje ya eneo ulilopo. Zipo semina mbalimbali nyingine ni za kiserikali zinalenga wafanyabiashara, wakulima, viongozi, wanafunzi pia zipo za kidini (kiroho) zinazolenga watu wote, wanandoa, cha kufanya nenda huko kajifunze mawazo ya Mungu ya kukufanikisha si unajua serikali inavyokuwa madarakani imewekwa na Mungu na hivyo wao pia watumishi wa Mungu, hivyo nenda huko jifunze kupitia wao. 

Tano: kupitia vyombo mbalimbali vya habari,
kama redio, Tv na computer (internet), magazeti. Vipo vipindi na ratiba mbalimbali vya kidini kwenye Tv vya watumishi wa ndani na nje ya nchi pia, fuatilia, kutoka kwao nunua kanda zenye mafundisho katika eneo unalolihitaji wewe kufanikiwa, sikiliza, tazama, yatendee kazi hayo mawazo. Hivyo ndivyo Mungu pia anavyowashirikisha watu wake mawazo yake. 

Njia ya mwisho ni kujifunza kupitia sauti ya Mungu na kuyatekeleza mawazo na maagizo anayokuletea. Unajua Mungu anazo njia mbalimbali anazoweza kutumia ili kukushirikisha mawazo yake, anaweza  akakuletea wazo fulani la kibiashara, kiuchumi kindoa nk. Chakufanya hakikisha unatekeleza, anaweza akasema nawe kwa njia ya ndoto, maono, kwa sauti yate nk. Zaidi jifunze kutii na kutekeleza kile unachojifunza kwa kusoma, kusikia au kuona. Usipuuze unachojifunza utafanikiwa
sana. Mtegemee Mungu na sio akili zako. 

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na ikae nanyi siku zote. 

KWA NINI MUNGU ANATAKA WATU WAKE WAWE MATAJIRI?

November 27, 2006

Na; Patrick Samson Sanga.

Ile mwanzo 12:2 neno inasema “nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka”. Na Mwanzo 13:2 inasema“Naye Abramu alikuwa ni tajiri  kwa mifugo, na kwa dhahabu”.

Hapa tunaona jinsi Mungu anavyoweka ahadi ya kumbariki Abramu na kumfanya kuwa taifa kubwa. Kwenye sura ya 13 tunaona tayari Mungu ameshaanza kumbariki inasema alikuwa tajiri kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Bado katika 3Yohana 1:2 Mungu anasema “mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo .

Mpaka hapa tunaona kabisa ni mpango wa Mungu kutufanikisha katika mambo yote, hii ni pamoja na mafanikio ya kifedha. Na utajiri ambao Mungu anataka tuwe nao sio utajiri mdogo .

Sasa swali ni kwamba kwa nini Mungu anataka tuwe matajiri? Maana kuwa tajiri bila kujua sababu za kuwa na huo utajiri utashindwa kujizuia kwenye matumizi mabovu ya huo utajiri (Fedha). Huenda zipo sababu nyingi, lakini mimi nataka nikuonyeshe sababu tatu za kibibilia.

Sababu ya kwanza , kulinda mawazo na mikakati ya Mungu kwa watu wake.

 Yeremia 29:11. Mhubiri 7:12 “Kwa maana hekima ni ulinzi kama vile fedha ilivyo ulinzi na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliyo nayo” Mithali 18:11 “ Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake .

Kwenye kitabu cha Yeremia 29:11 Mungu anasema nayajua mawazo ninayowawazia, si mawazo mabaya, ni mawazo ya amani ………..Sasa ukiunganisha mawazo ya mhubiri 7:12 na mithali 18:11 utupata sentensi hii. Mungu anapokupa utajiri (fedha), anakutajirisha ili kulinda mawazo (mipango) na mikakati ya Mungu ambayo anakupa kabla ya kukupa hizo pesa kwa watu wake. Fedha yoyote ambayo Mungu anaileta mikononi kwako kumbe ina makusudi, mipango ya Mungu ndani yake.

Mungu anayo mipango na njia za kuwafanikisha watu wake kiuchumi, kimwili, kibiashara, kimaisha  n.k. sasa hii mipango inalindwa na nguvu ya fedha. Maana kama watu wake watakuwa masikini basi mipango aliyo nayo juu ya kanisa, familia, nchi n.k. basi si tu haitatekelezeka vizuri bali pia itanunuliwa na shetani kwa fedha yake. Hii ina maana Mungu anataka tuwe na nguvu ya kimaamuzi na ya utawala kwa yale anayotuagiza Mungu kwa sababu kwa fedha.

Sababu ya pili , Ili kuliimarisha agano lake.

kumbukumbu 8:18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri, ili ALIFANYE imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.

Hapa tunaona wazi kabisa kwamba Mungu anasema ninakupa huo utajiri ili kulifanya agano lake kuwa Imara. Je agano hili ni lipi? Yeremia 31:31 inasema “Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, …. Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaindika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu.

Agano ambalo Mungu anataka uimarishe kwa fedha anayokupa ni la yeye kukaa na watu wake. Maana yake tumia fedha anayokupa kujenga na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Yesu na watu wake.Uhusiano wa Yesu kama mwokozi, Rafiki, mpanyaji, Bwana n.k kwa watu wake maana yake ni hii, tumia fedha kufanya jambo lolote maadamu una hakika litapelekea uhusiano wa mtu (watu) na Yesu kuimarika na jina la Yesu kutukuzwa. Na kwa sababu hiyo utukufu wa mwisho wa nyumba hii/agano hili utakuwa ni mkuu kuliko ule wa kwanza, Hagai 2:8

Sababu ya tatu, ili tukopeshe na sio kukopa .

Kumbukumbu la Torati 28:12 inasema Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri … Nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe .Sikiliza tumeshaona katika mithali 18:11 kwamba mali ya mtu tajiri ni mji wake wenye nguvu… kwa lugha nyepesi maana yake fedha ya mtu tajiri ni nguvu ya huyo mtu kwenye mji aliopo/ au ambao yupo. Kwa kuwa akopaye ni mtumwa wake akopeshaye, hivyo utakapokopesha maana yeke utakuwa na nguvu juu ya maamuzi na hisia za huyo au hao watu uliowakopesha.

kama tukibakia kukopa tutakuwa watumwa na kwa sababu hiyo ndiyo maana Mungu anatupa utajiri kwa mtu mmoja, familia, kanisa, nchi n.k

Naamini sehemu ya kwanza ya somo hili litakusaidia katika matumizi ya utajiri ambao Bwana Mungu amekupa.

Ubarikiwe.

NINI MATARAJIO YA MUNGU KWA VIJANA?

November 27, 2006

Na: Patrick Samson Sanga.

 1yohana 2:14 “…. Nimewaandikia ninyi,vijana kwa sababu mna nguvu,na neno la Mungu linakaa ndani yenu ,nanyi mmeshinda yule mwovu.”Mungu anao mtazamo wake binafsi juu ya kila kundi la watu chini ya jua,.Na kila kundi mfano wa wamama,wajane,watoto,vijana kuna mambo fulani ambayo Mungu anatarajia kila kundi litatekekleza. Mungu anazungumza na vijana na kusema nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu moja mna nguvu,mbili neno la Mungu linakaa ndani yenu, na tatu mmemshinda yule mwovu.

Nguvu zinazozungumziwa hapa ni nguvu,uweza wa Mungu wa kukusaidia kutekeleza maagizo yake. Na kwa sababu hiyo basi kuna matarajio ya Mungu kwa hao vijana. Sasa lengo la ujumbe huu mfupi ni kukueleza nini Mungu anatarajia/anategemea kwamba utafanya sawasawa na nafasi aliyokupa mbele zake na uwezo aliokupa. Matarajio ya Mungu kwa vijana ni kama ifuatavyo:

*Moja, Vijana wauteke ufalme wake.

Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu,nao wenye nguvu wauteka”. Biblia inapozungumzia ufalme wa Mungu inazungumzia habari za utawala wa Mungu . Hivyo ni matarajio ya Mungu kwamba popote pale vijana walipo basi watatengeneza mzazingira ya Mungu kutawala katika maeneno waliyopo iwe darasani, Chuoni, Kazini, Kanisani nk na hii ni kwa sababu wana nguvu.Sikiliza vijana wana nguvu na ufalme unapatikana kwa nguvu,maana yake Mungu anatarajia vijana watumie nguvu zao kuuteka ufalme wake na kuurusu uchukue utawala duniani.

*Mbili,Vijana warejeshe urithi na mali za wana wa Mungu zilizotekwa.

Mwanzo 14:13-16. “…Akawapa silaha vijana wake,walozaliwa katika nyumba yake,watu mia tatu na kumi na nane,akawafuata mpaka Dani”. Hizi ni habari za Ibrahamu aliyeenda kumuokoa nduguye Lutu baada ya kuwa ametekwa.Ili kurejesha urithi wao na mali zao ilimbidi Ibrahimu atumie nguvu kazi ya vijana. Na hivyo hata leo Mungu anatarajia kwamba vijana wasimame kwenye nafasi zao na kupambana kwa ajili ya afya,ulinzi, uchumi,uponyaji,mafanikio ya watu wake. Hebu jipe dakika moja halafu tazama jinsi shetani anavyotesa watu na kudhulumu afya zao, ujana wao, ndoa zao ,uchumi wao nk.Ni nani watakaorejesha hali nzuri, urithi huu kwa wana wa Mungu , ni Mungu kupitia Vijana.

*Tatu, Vijana wasikosee katika kufanya maamuzi ya kuoa au kuolewa.

Mithali 5:18 “Chemichemi yako ibarikiwe;nawe umfurahie mke wa ujana wako”.Sikiliza Mungu anataka ndoa yako iwe ni ndoa ya mafanikio na ya furaha, maana yake ni ndoa ambayo hautaijutia kwamba kwa nini nilimuoa au kuolewa na huyu mtu.Sasa ili ndoa yako iwe ni ya furaha na amani, ni lazima huyo mwenzi wako umpate kwa uongozi wa Mungu mwenyewe. Sasa mtazamo wa Mungu kwa vijana ni huu vijana hawatakosea kufanya haya maamuzi kwa sababu tayari Neno la Kristo limejaa kwa wingi ndani yao.Kumbuka neno la Kristo ni taa ya miguu yangu.

*Nne, vijana wawe wasuluhishi wa matatizo katika jamii na taifa.

 Mithali 1:4 “Kuwapa wajinga werevu,na kijana maarifa na hadhari”. Leo ndani ya kanisa, jamii tunayoishi na katika taifa kwa ujumla yapo matatizo mbalimbali ya kiroho,kiuchumi,kijamii,kiafya,kimwili,kibiashara,kindoa nk. Sasa Mungu anatarajia vijana ndio watumike kusuluhisha matatizo haya mbalimbali katika jamii kwa sababu ya wingi wa neno la Kristo ndani yao. Hii ina maana mtu mwenye neno la Kristo kwa wingi ndani yake basi maana yake ana upeo mkubwa wa kuelewa mipango na njia za Mungu za kuwatoa watu wake kwenye matatizo yanayowakabili. Hivyo tumia fursa hiyo kutatua matatizo hayo na kusuluhisha kwa sababu ya Kujua mawazo na njia za Mungu za kuwatoa watu wake kwenye shida walizonazo.

*Tano, vijana walitumikie kusudi lake la kuhubiri habari njema.

 Mathayo 28:19 “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,mkiwabatiza kwa jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu”. Sikiliza kwa sababu ya nguvu ambayo Mungu amewekeza kwa vijana basi ni matarajio yake kwamba wewe kama kijana utatumika kuwaeleza watu wengine habari njema za Yesu Kristo ziletazo amani. Ni matarajio yake kwamba vijana watapita nyumba kwa nyumba , mtaa hadi mtaa wawaambie wengine kuhusu huyu Yesu, wakiwafungua waliofungwa na kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika. Naamini haya matarajio matano ya Mungu kwako kama kijana mwenzangu basi yatakusaidi sasa kukaa kwenye nafasi yako ili Mungu ajivunie kuwa na kijana kma wewe.

Amani ya Kristo na iwe pamoja nanyi.

 Ndimi katika utumishi huu Patrick Sanga.

ENYI WANAWAKE MSINILILIE MIMI.

November 27, 2006

 Na; Patrick Samson Sanga.

Kwa nini Yesu aliwaambia akinamama jililieni nafsi zenu na watoto wenu ?
Luka 23:27-28 “Na mkutano mkubwa wa watu wakamfuata na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea, Yesu akawageukia,akasema,Enyi binti za Yerusalemu ,msinililie mimi,bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu”.

Hapa Bwana wetu Yesu alikuwa njiani kuelekea Golgotha kusulubiwa, akina mama na binti za Yerusalemu wakawa wanamlilia na kumwombolezea Yesu kwa uchungu sana.

Sasa kwa kawaida mtu anapokuwa anapita kwenye hali ngumu au matatizo au msiba au janga lolote zito kwa kawaida tunapenda watu wengine watufariji na waomboleze pamoja na sisi na ndiyo maana hata Paulo alisema lieni pamoja na wanao lia nk

Lakini jambo hili halikuwa hivyo kwa Yesu ,kile kilio cha wale akina mama kilimfanya Yesu awageukie na kutoa ujumbe wa ajabu kwa wale akina mama na ndipo akasema msinililie mimi,bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu .

Nimeandika ujumbe huu mfupi ili kujibu maswali mawili ambayo tunayapata kutoka katika sentensi ya Bwana wetu Yesu kwa hawa wamama nayo ni;
Moja, kwa nini Yesu aliwaambia msinililie mimi ? mbili kwa nini Yesu aliwaambia jililieni nafsi zenu na watoto wenu?. Yesu aliwaambia msinililie mimi kuu mbili nazo ni;

{a}Ili neno liweze kutimia.Yohana 3:16. Mapatano ya Yesu na baba kule mbinguni ilikuwa Yesu aje na afe  kwa ajili ya watu wake. Ili mlazimu Yesu kupita kwenye hiyo njia, hata kama wangeombolezaje kilio chao kisingeweza zuia kifo cha Bwana Yesu.

Kumbuka kule Gethsemane Ysu mwenyewe aliomba akasema Baba, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke, Lakini tunaona Mungu alituma malaika kumfariji na kumtia moyo na Yesu mwenyewe alikuwa tayari mapenzi ya Mungu yatimizwe.

{b} Kilio chao kingemhuzunisha na kumvunja moyo zaidi. Matendo ya Mitume 21:9-14.Hapa ulikuwa umetolewa unabii wa jinsi vile Paulo atakavyouawa kule Yerusalemu. Na watu wa nyumba ile wakaanza kulia na kumsihi Paulo asipande kwenda Yerusalemu, Ndipo Paulo akawaambia mnafanya nnini, kulia na kunivunja moyo?. Kwa hiyo hata Yesu angekutana na hali ka,a ya Paulo.

Swali la pili; Kwa nini Yesu aliwaambia wamama bali jililieni nafsi zenu na wato wenu na Je alikuwa ana maana gain kuwaambia hivyo?
 Kabla sijakuambia hizo sababu, ngoja kwa kifupi nikuambie habari za nafsi. Kwa kiyunani inaitwa (psuche).Nafsi inahusika kuelekea ndani ya mtu.Ndani ya nafsi ndiko kwenye hisia,akili na maamuzi ya mtu.Hivyo nafsi ya mtu inahusika na maauzi, hisia na nia za mtu binafsi. Nafsi inatabia ya kuugua,kuinama, na na kuumia pale inapojeruhiwa.

Siku zote nafsi inagojea mwongozo wa roho au mwili wa mtu. Mtu akiwa ni wa rohoni nafsi itakaa mkao wa rohoni na mtu akiwa ni wa mwilini na nafsi yake itakaa mkao wa mwilini.Nafsi inaishi sasa kwa kutegemea maneneo unayojisemea au kusemewa na wengine sasa au wakati uliopita.Hivyo Yesu alipowaambia wale kinamama msinililie mimi alikuwa na maana hii na sababu hizi;

*Moja, Yesu alijua akinamama wengi ni watu ambao nafsi zao ni rahisi kujeruhika na kuinama pindi wanapokutana na matatizo mbalimbali na zaidi kina mama wengi ni watu ambao ni wepesi sana kuijtamkia maneno ambayo kwa namna moja au nyingine yanajeruhi nafsi na kuharibu future yao wenyewe.

Kwa Kujua kwamba akina mama wengi mara nyingi huwa wanajitamkia maneno ambayo yanaathari kwao wenyewe, watoto wao, familia zao, kanisa lao na hata nchi nk ndio maana Yesu alisema jililieni nafsi zenu.
 Alikuwa akimaanisha nini?

Yesu alikuwa anawaambia wale wamama wajitunze nafsi zao na za watoto wao kwa kuhakikisha ndani wanweka neno la Mungu linalozungumzia maisha yao ya baadae (future).

Hili neno litazifanya hisia zao, na akili zao na maamuzi yawe yatawaliwe na ahadi za Mungu na hii itawasaidia nafsi kutokuinama wala kujeruhika pindi wanapokutana na matatizo mbalimbali. Neno hili litawapa jibu la kukabiliana na mazingira ya kila nmana kwa sababu hiyo Jehanamu itakosa watu .

*Mbili ni kwa sababu ya nafasi na wajibu ambao Mungu amewapa akinamama kama walinzi wa kusudi lake popote pale walipo.

Nisikilize mwanamke Mungu amekuheshimu sana kukupa wajibu wa kulinda agano na kusudi lake duniani.Shetani anapotaka kuvuruga na kuharibu kusudi la Mungu mahali popote pale, uwe na uhakika lazima tu ataanza kutafuta njia na mpenyo kwa mwanamke.Shetani akitaka kuleta vurugu kwenye ndoa,kanisa,familia uwe na uhakika atafanya kila analoweza apitie kwa mwanamke.

Hebu chukua dakika moja tafakari vile shetani anavyovuruga vijana wa kike na wa kiume, kwa kuwafanya mabinti watoe mimba na kuua bila hata hofu kwa Mungu, Wazazi kufanya tendo la ndoa na wanao, ndugu kwa ndugu, Yesu aliona huzuni na kilio kikubwa ambacho kwanza kitawapata kinamama hapahapa duniani na baadaye katika dhiki kuu na mwisho katika Jehnamu ya moto na ndiyo maana alisema watasema heri wa matumbo yasiyozaa na matiti yasiyonyonyesha.

Mwanamke hakikisha uniombolozea nafsi na kuiambia nafsi yangu mtii Mungu, nafsi yangu usiiname kwa yale unayoaona, hawa watoto wangu si ya dunia, iambie nafsi yako kwamba hawa watoto, hii ndoa, kanisa, vijana,nchi nk ni ya Bwana .

Hakuna hata mmoja wa watoto wangu watakaokwenda Jehnamu , sizai watoto wa kwenda Jehanamu nk.Hakikisha ndani yako ahadi za Mungu zinajaa kwa wingi ili nafsi isitekwe na hivyo ukawa umemruhusu shetani kuvuruga na kuharibu kusudi la Mungu kupitia wewe .

Naamini ujumbe huu utawasidia wamama wengi Kujua namna ya kushughulika na nafsi zao na kuhakikihsa haziwafanyi kutoka kwenye kusudi la Mungu.

Neema ya Kristo na iwe nawe.

NJIA KUMI ZA KIBIBLIA ZA KUMPATA MWENZI WA MAISHA.

November 3, 2006

Na: Patrick Samson Sanga.

Mpenzi msomaji hizi ni dondoo tu zilizomo ndani ya kitabu hiki ndani ya kitabu cha kwanza, nimeona ni vema walau kwa sehemu nikueleze yaliyomo ndani.
Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kutoka kwa babaye bali mke mwenye busara mtu hupewa na Bwana’.Nianze kwa kusema kuoa au kuolewa ni mpango kamili wa Mungu. Zipo sababu nyingi za kwa nini unahitaji mke au mume Moja unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana, mbili ni kwa sababu zinaa (1 Wakorintho 7:20) na tatu unapopata mke unakuwa umepata msaidizi na mlinzi.

Kibiblia mke /mme mwenye busara mtu hupata kutoka kwa Bwana, maana yake Mungu ndiye anayehusika na kumpa mtu mke/mme. Mungu pekee ndiye anayejua nani ana busara ya kukaa na fulani halafu ndiyo anayekupa huyo mtu. Suala la kumpata mwenzi ambaye hakika ni wa mapenzi ya Mungu kwa mtu husika, imekuwa ni changamoto kubwa hasa kwa vijana na pia wale ambao bado hawajaoa au kuolewa.

Lengo la kitabu hiki ni ;

*kuwasaidia vijana wengi ambao bado hawajaoa au kuolewa kufanya maamuzi sahihi.

*Kuwapa maarifa wale ambao wanafuatwa na vijana wengi kwa lengo la kutaka kuwaoa, nini wafanye pindi wanapofuatwa na vijana wengi.

*Kuwapa uhakika / uthibitisho wale ambao tayari wameshafanya maamuzi haya na tayari wana wachumba kwamba wachumba hao wanatokana na Mungu au la.

*Kuwafariji na kutoa mwongozo kwa wale ambao huenda hamna anayejitokeza kutaka kuwaoa, wanaokataliwa na wale ambao wamechelewa kuolewa halafu wao wanafikiri ni laana.

*Kutoa mwongozo kwa wazazi, wachungaji, walezi, viongozi wa makundi ya kidini kuwasaidia vijana wao katika kufanya maamuzi haya makubwa .

*Kukusaidia kuzipinga hila zote za shetani katika safari hii ya maamuzi.

Kabla ya kuzitaja njia, ndani ya kitabu hicho nimetaja kwanza misingi unayotakiwa kuijua kabla ya kuzijua hizo njia nayo ni;

*Kwa kila jambo kuna majira yake hivyo hata wewe kuoa au kuolewa kwako kuna wakati wako maalumu.

*Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kukujulisha wewe mwenzi wako.

*Mungu anavyo vigezo vya kwake ya kukupa mke au mme ambavyo si lazima viendane na vigezo vya kwako.

*Si kila mke au mme hutoka kwa Mungu.

*Mungu anapoamua kukupa wewe mke au mme anakuwa ameangalia mbali kuliko wewe unavyofikiria.

*Usimuombe Mungu akujulishe mke au mme wako wakati ndani yako umeshajichagulia wa kwako.

*Ni vema uwe umekomaa na umekua kiakili, kiufahamu, na kiroho kwanza kabla ya kufanya maamuzi kama haya na hujaokoka fanya maamuzi ya kuokoka maana ni kwa faida yako mwenyewe.

*Ni vema ukatambua ya kuwa mwenzi wako si lazima atoke kanisa lako, shule au chuo ulichosoma au kazini kwako nk.

Zifuatazo ni njia za kibiblia, ambazo hakika zimewasaidia wengi kuwajua na kuwapata wenzi wao wa maisha;

*Kwa kumcha Mungu, ( kumtii Mungu ).

*Kwa sauti ya Mungu mwenyewe.

*Amani ya Kristo.

*Upendo wa ki –Mungu ( wa Dhati ).

*Mafunuo ya ki-Mungu.

*Kwa kuyatenda mapenzi ya Mungu.

*Kulijua kusudi la Mungu katika maisha yako.

*Kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu.

*Wazazi /walezi/wachungaji/kiongozi wako katika kundi lenu.

*Dhamiri za watu wengine au ushuhuda wa watu wengine.

Mpenzi msomaji hapa nimetaja tu hiyo misingi na njia husika. Lakini ndani ya kitabu nimefafanua kila msingi na njia kimapana maana isingekuwa rahisi kuziweka kurasa zote za kitabu hiki humu ndani.

Kama huna kitabu na ungependa kupata kitabu au hata kumchukulia mtu mwingine nenda katika Category ya vitabu utapata maelekezo huko.

Bwana Mungu akubariki na akutangulie katika safari hii ya maamuzi makubwa katika maisha yako.