Archive for September 2006

JIFUNZE KUMILIKI MAJIBU YA MAOMBI YAKO

September 19, 2006

 Waraka wa Septemba

 

Yoshua 13:1-7

Utangulizi,

Katika dunia ya leo  watu wengi sana wamekuwa wakitumia muda wao mwingi ikiwa ni pamoja na kufanya maombi ya kufunga na kuomba ili kumuomba Mungu awabariki, awaponye, awalinde kwa kifupi awajibu mahitaji yao waliyonayo mbele zake siku zote. Wapo waliokuwa hawazai wamezaa, vipofu wameona, wasioajiliwa wameajiliwa, biashara za wengi zimefanikiwa, ndoa nyingi Mungu ameziponya, wapo waliotaka kuolewa au kuoa na Mungu amewapa waume na wake wazuri. 

 

   Sasa hao hao watu ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi katika kuomba Mungu awatendee miujiza katika maisha yao, imefika mahali wanaona yale ambayo yalikuwa ni majibu ya Moambi yao shetani ameyavamia na kuleta balaa zaidi na limekuwa pigo kubwa sana  kwa wana wa Mungu. Na kwa sababu hiyo wamejikuta wakimlalamikia Mungu kama vile wana wa Israeli na imefika mahali  pa wengine  kuona kama Mungu  hawezi na hivyo kumuacha.

Tatizo  la haya yote ni kwamba wakristo wengi hawana tabia ya au mazoea ya kumiliki mujibu ya maombi yao toka kwa Mungu. Huenda ulikuwa huna mtoto na Mungu amekupa kuzaa mtoto, sasa  huyo mtoto ndiyo jibu lenyewe kutoka kwa Mungu. Sasa ni lazima ujifunze kumiliki  huo muujiza wa mtoto, sasa si mtoto tu bali ni pamoja na ajira, ndoa, uponyaji, kanisa, Nchi, Biashara nk. 

 

  Kusudi la waraka huu mfupi ni kukufundisha njia zitakazokusaidia kumiliki majibu ya maombi yako na kukupa maarifa yatakayokusaidia kuwa makini na majibu ya Mungu katika maisha yako.Tafsiri ya Kumiliki, Neno kumiliki linapozungumziwa kibiblia lina maana ya kukiweka kitu au jambo fulani chini ya utawala wako, maana yake unakuwa na nguvu au umri juu ya hicho kitu. Una hakikisha  hakiwezi kutoka kwako. Kumiliki siku zote kunahusisha mapambano makali Sasa mimi sijui Mungu amekutendea nini? Ila ninachojua kwa namna moja au nyingine lazima kuna mambo ulikuwa unamuomba Mungu  akufanyie na mengine tayari ameshakufanyia na mengine ndiyo anayafanya na bado kuna mengi atafanya.sasa katika hayo aliyokwisha kufanya huenda amekupa mke au mme mtarajiwa, huenda ameiponya ndoa yako, nafsi yako, mwili wako, Afya yako, Huenda amekupa mtaji, amekupandisha cheo, amekupa mtoto, amepanua  mipaka ya huduma yako  nk.

 

    Katika lolote ambalo amekufanyia unatakiwa kulimiliki kwa maombi. Kama shetani alikuwa hataki uzae usidhani atamfurahia mtoto uliyemzaa. Kama alishindwa kumzuia asizaliwe usidhani atakubali aendelee kuishi. Shetani atafanya kila  analoweza kuua huyo mtoto au kuharibu chochote kile ambacho Mungu amekutendea kama jibu. Sasa kwa sababu hiyo ni lazima uzijue njia za Kibiblia zitakazokusaidia kumiliki hayo majibu ya maombi yako kutoka kwa Mungu.

 

 Huenda zipo njia nyingi zifuatazo ni sehemu na ni za msingi kati ya hizo nyingi.

 

Njia ya kwanza, kumiliki kwa kuupigania na kuujenga huo muujiza au jibu lako toka kwa Mungu.

Yoshua 13:1-7, 2 Samwel 2:1-7.Ule mstari wa kwanza wa kitabu cha Yoshua katika kitabu Yoshua 13 unasema “Basi Yoshua alipokuwa mzee na kuendelea sana miaka yake BWANA akamwambia wewe umekuwa mzee na kuendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi  nyingi sana bado kumilikiwa” Kumbuka katika ile sura ya kwanza  ya kitabu cha Yoshua Mungu anamwambia Yoshua uwe Hodari na moyo wa ushujaa maana ni wewe utakayewarithisha watu wa nchi hii. Na ukisoma vizuri kitabu chote cha Yoshua unaona kabisa Yoshua alitekeleza agizo la kuwarithisha wana wa Israel nchi ya ahadi.

 

 Wakati Mungu anamwambia Yoshua bado inabaki nchi yaani maeneo mengi sana ambayo bado hayajamilikiwa tayari Yoshua alikuwa ameshapiga zaidi ya wafalme 32 na kuiteka miji yao, lakini bado Mungu anamwambia bado nchi nyingi inasalia. Kitu gani Mungu anataka tujifunze hapa? Sikiliza Yoshua alipewa kuwarithisha wana wa Israel nchi hii lakini sio kuwamilikisha. Suala la kumiliki lilikuwa kwa yule aliyekabidhiwa nchi  au mji lakini sio kwa Yoshua. Sasa ndiyo maana Mungu akamwambia Yoshua kwa sababu wewe  ni mzee igawanye  hiyo nchi kwa wana wa Israeli kwa kufuata kabila zao ili waweze kumiliki. Maana yake waingie kwenye mapambano ya kile ambacho Mungu amewapa kupitia Yoshua.

 Niseme hivi chochote unachokipata kwa njia ya maombi kinamilikiwa kwa njia ya maombi, jifunze kukipigania na kukijenga yaani kuendelea kukiri uwepo wa hicho kitu siku zote. Mfano kama uliomba mke au mme na Mungu amekupa usipunguze kuomba maana shetani usidhani anafurahia ndoa au uhusiano wenu. Ukiendelea  kusoma zile  sura zinazofuata za kitabu cha Yoshua ndipo utakapoona makabila yalivyopambana ili kumiliki jibu lao toka kwa Mungu la nchi. 

 

Njia ya Pili; Miliki majibu yako kwa kutafuta maarifa zaidi ya kutunza huo muujiza.

 Hosea 4:6a inasema “Watu wangu wanaangamizwa  kwa kukosa maarifa”.Sikiliza  muujiza au jibu lolote lile ambalo Mungu amekujibu au amekutendea una maarifa yake ya kuutunza. Maarifa hayo yanaweza kuwa ndani ya Biblia na hata katika vitabu vingine nje ya Biblia. Mfano umemwomba Mungu akupe mtaji uanze biashara na Mungu amekupa, sasa huo mtaji una namna zake za kuuendesha ili uweze kuzaa kwa faida. Kuna namna fulani ambayo ukiwekeza utapata faida nzuri. Sasa maarifa hayo ya kuwekeza yapo mengine kwenye Biblia lakini mengine ni kupitia watu wenye uzoefu katika hilo eneo, vyombo vya habari, kuna semina za kiserikali kuhusu biashara nenda huko ufuatilie ili  ujue zaidi, maana apendaye mafundisho hupenda maarifa. Huenda ulikuwa hujaoa au kuolewa na sasa uko kwenye ndoa. Hudhuria semina za ndoa na kusoma vitabu husika ili upate maarifa yatakauokusaidia kuishi katika ndoa vizuri.

Umezaa watoto wengi wanakufa kwa malaria halafu watu wanasema ni shetani tu wakati mwingine si shetani  ila ni wewe ulimweka mwanao katika mazingira  ya  kuumwa  na mbu vizuri ndio maana akafa. Soma habari za matumizi ya ngao, chandarua yanayotolewa na serikali hujui kwamba serikali yoyote ile imewekwa na Mungu. Kwa kifupi muujiza wowote amabo Mungu amekutendea una maarifa yake ya kuutunza na chanzo kikubwa cha maarifa ni neno la Mungu. Hivyo lisome likae kwa wingi ndani yako.

 

 Njia ya Tatu; Miliki majibu yako kupitia shukrani, sadaka au utoaji wa aina  yoyote ile.

 2Wafalme 5:17”Naamani akasema kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili, kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA. 

Hizi  ni  habari za Namani Jemedari  wa jeshi la shamu alikuwa na Ukoma. Alipokwenda Istraeli  kwa nabii Elisha ili aombewe kuhusu tatizo la ugonjwa wake Elisha alimpa maagizo ya kutekeleza kuwa akajichovye / akajizamishe ndani ya mto Yordani mara saba na ndipo atapona. Baada ya Namani kutii maagizo Biblia inasema alipona na ngozi yake ikatakasika ikawa kama ya mtoto mchanga.Baada ya jibu  hilo kwanza Namani alimshukuru Mungu wa Elisha na kisha akasema tangu siku ile hatatoa tena sadaka kwa miungu yao kule shamu isipokuwa kwa Mungu wa Elisha pekee.

Unapomshukuru Mungu kwa lile alilokutendea ni ishara ya kupokea kwa kuonyesha kujua nani aliyekutendea hilo jambo na  hivyo kumrudishia yeye utukufu. Pia unaweza kumiliki majibu ya maombi yako kwa njia ya kutoa sadaka kwa yatima, wajane na pia unaweza kumshukuru Mungu kwa kushuhudia kwa wengine nini Mungu kakutendea au kutoa sadaka ya shukrani au utoaji kwa makundi mengine yasiyojiweza  katika jamii.

 

 Njia ya nne: Kumiliki muujiza kwa kuwatunza watumishi wa Mungu na kuchangia huduma mbalimbali.

Yoshua 12:1-3 kwenye ule mstari wa pili Biblia inasema “Basi wakamwandalia karamu huko naye Martha akamtumikia na Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja nao. 

Hii pia ni habari nyingine inamhusu Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua baada ya kuwa amekufa kwa siku nne. Sasa Lazaro aliumiliki muujiza wake wa kufufuliwa kwa kumtunza Yesu pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Hii ina maana Lazaro pamoja  na dada zake waliingia gharama kwa ajili ya kuwatunza Yesu pamoja na  wanafunzi wake, Kwa siku zote ambazo Yesu alikaa kwa Lazaro, Lazaro alihakikisha hawalali njaa, anawapa mahali pa kulala nk.

Sasa unaweza kumiliki muujiza wako kwa kuruhusu watumishi wa Mungu wakae nyumbani kwako. Huenda wamekuja kwenye mkutano au semina kwa wiki moja au mbili itoe nyumba yako itumike, kufanya hivyo ni kumfanya Mungu aendelee kukulinda wewe na yale aliyokupa maana anajua hutamnyima siku moja atakapohitaji kuvitumia. Wapo wengine wanaomiliki kwa kutoa magari yatumike kipindi chote cha mikutano, unaweza pia  kumiliki kwa kuchangia gharama za mikutano  si lazima pesa lakini hata kufanya kazi mbalimbali katika mkutano huo, huenda  ni  usafi,  kubeba vyombo, kufanya usafi walikofika watumishi, kuombea huo mkutano au semina nk. Nakuambia unaweza ukaona kama ni vitu vidogo lakini ndivyo mujibu ya maombi yanavyomilikiwa bila kujali Mungu amekutendea nini.

 

 

 Nija ya tano: Kumiliki muujiza kwa kufanya  maamuzi ya kuokoka endapo Mungu alikufanyia huo muujiza kabla hujaokoka, na kuwaambia wengine habari ya Yesu aliyekuponya. 

 Ukisoma ile sura nzima ya 9 ya kitabu cha Yohana utakutana na habari ya kipofu mmoja tangu kuzaliwa kwake  ambaye Yesu alikuwa amemponya. Ule mstari wa 39 unasema “akasema,Naamini, Bwana akamsujudia” Ukisoma vizuri habari hii utagundua baada ya mahojiano marefu kati ya mafarisayo na yule kijana kuhusu uponyaji wake ndipo Yesu akamwuuliza je unamwamini mwana wa Mungu? Yule kijana akamwuliza ni nani huyo nipate kumwamini? Kwa kifupi Yesu akamjibu unayezungumza naye. Ndipo yule kijana  akasema, naamini Bwana akamsujudia.

Mtu mwingine ni Naamani ambaye tumekwisha ona habari zake, kitendo cha yeye kusema toka leo sitatoa sadaka kwa miungu  ya shamu ila kwa Bwana  ni dalili  ya kuonyesha kumwamini Mungu wa Israel. Hivyo hata leo wapo ambao Mungu anawatendea mambo mengi hata kabla hawajaokoka sasa ili kumiliki  hayo ambayo Mungu amekufanyia mwamini Yesu ndio huo muujiza utadumu. Wapo watu leo wanafunguliwa kwenye nguvu za mapepo huo ni  uponyaji. Sasa badala ya kuwasaidia watu wamwamini Yesu tunawaacha, nakuambia pepo watarudi kwa huyo mtu wenye nguvu zaidi kuliko yule wa kwanza. 

 

  Pia ukisoma vizuri habari hiyo hiyo utagundua kwamba huyu jamaa alimiliki uponyaji wake kwa kuwaambia wengine habari za Yesu na kukiri kwamba  mponyaji ni Yesu na si mtu mwingine, nakuambia  kufanya  hivyo ni kujihakikishia kudumu kwa huo muujiza na Mungu ataendelea kuutunza huo muujiza  maana wewe ni chombo chake. Mungu akikuponya au kukubariki usinyamaze kimya waambie wengine habari za Yesu aliyekuponya. Jifunze kutoka kwa mwanamke msamaria. Uponyaji wa nafsi yake ulipelekea watu wengi wa mji wa Samaria kuokoka. Soma kile kitabu cha Yohana sura ya nne mistari 30 ya kwanza utaiona habari hii. 

 

Mpenzi msomaji wangu mpaka hapa naamini utakuwa umepata kitu cha kukusaidia labda nikuambie hivi  siri kubwa ya mafanikio ni kuliweka neno la Mungu kwenye matendo, si unajua imani pasipo matendo imekwisha kufa katika nafsi ya huyo mtu mwenye imani hiyo. Nimeamua  kuandika ujumbe  huu baada ya kuona wana wa Mungu wengi imefika mahali  wanakuta yale ambayo Mungu aliwapa kama majibu ya maombi yao yameshaharibiwa na shetani, wapo waliozaa watoto wao wakafa na walimuomba sana Mungu kuhusu hao watoto nk. Sasa  ni imani  yangu kwamba tangu sasa jambo lolote ambalo Mungu atakupa kama jibu la maombi yako utalimiliki.

 

 Ndimi katika huduma

Patrick Samson  Sanga

Tuendelee kuombeana.

NINI NI MAPENZI YA MUNGU KWA MWANADAMU?

September 16, 2006

Na;Patrick Samson Sanga.

Mathayo 7:21 inasema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”

Naamini kabisa kama kweli wewe unahamu ya kuingia katika ufalme wa Mungu basi ni lazima utataka kujifunza yapi ni mapenzi ya Mungu kwako ili uyatende na uweze kuurithi uzima wa milele. Yesu anasema si kila mtu, sio watu, bali mtu aniambiaye Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa Baba.…………kwa lugha nyepesi maana yake wapo wengi wenye kusema Bwana Bwana lakini hawataurithi ufalme wa milele kwa sababu ya kutotenda mapenzi ya Mungu.

Hivyo basi kwa sababu si kila mtu, aniambiaye………….., maana yake kwa kila mtu chini ya jua kuna mapenzi ya Mungu ya kutekeleza, na mapenzi ya Mungu maana yake ni yale ambayo Mungu anataka watu wake wayatende . Sasa lengo au shabaha ya ujumbe huu ni kujibu swali letu kwamba nini  ni mapenzi ya Mungu kwa mwanadamu na hivyo kukupa maarifa yatakayokusaidia kuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yako .

Baada ya kuwa nimemuomba Mungu anijulishe na kujifunza zaidi kuhusu mapenzi ya Mungu nilipata  maarifa yafuatayo kuhusu mapenzi ya Mungu, Mapenzi ya Mungu unaweza kuyagawanya  katika makundi makubwa mawili kama ifuatavyo;
(a) Ni mapenzi ya Mungu uongozwe na Roho Mtakatifu.

Ukisoma 1Wakorinto 12:3 Biblia inasema “kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema Yesu amelaaniwa wala hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana,  isipokuwa katika Roho Mtakatifu sasa ili uelewe vizuri soma kwanza mistari hii katika Isaya 46:9-10 ; “ Kumbukeni mambo ya zamani za kale, maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado nikisema , shauri langu litasimama , nami nitatenda mapenzi yangu yote” unaweza ukarudia tena kusoma hiyo mistari ndiyo tuendelee.

Mungu anasema yeye ndiye autangazaye mwisho tangia mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka. Maana yake ni hii Mungu anakujua vizuri kuliko unavyojijua. Pia tayari Mungu anayo ratiba kamili ya maisha yako tangia ulipozaliwa. Na anajua kwa nini alikuumba na anao wajibu au kusudi ambalo anataka ulitekeleze, na hii ina maana haukuzaliwa kwa bahati mbaya.

Sasa ili uweze kulitumikia kusudi/shauri la Bwana katika kizazi chako unatakiwa uongozwe na Roho Mtakatifu. Maana katika zaburi 32:8 anasema “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama’.

Mimi sijui kusudi la Mungu kwako ni nini?, ila ninachojua kwa mujibu wa Biblia  kila mmoja ana wajibu wa kuutekeleza. Na Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji wa wewe kutekeleza huo wajibu uliopewa na Mungu chini ya jua. Ikiwa ni huduma, siasa, utawala, ofisi, biashara n.k. Anaposema nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea maana yake katika mambo ya rohoni na hata ya mwilini, Roho Mtakatifu atakuongoza kuyatenda yale ambayo ni mapenzi ya Mungu. Maana katika warumi 8:14 anasema ” kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho Mtakatifu hao ndio wana wa Mungu”.

Sasa kama hauongozwi na Roho Mtakatifu katika kulitumikia shauri / kusudi la Bwana katika maisha yako ya kiroho au kimwili maana yake unaongozwa na roho nyingine ya dunia hii ambayo nia yake ni mauti. Na mtu wa namna hii hata akitoa unabii au pepo kwa jina la Yesu atakataliwa maana anafanya hayo kwa kujikinai siyo Mungu Roho Mtakatifu anayemuongoza.

(b) Ni mapenzi ya Mungu ulitendee kazi neno lake.

, Warumi 2:13 inasema “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki“. Tazama, haki ya kuurithi ufalme wa Mungu haiko kwa wale waliosikia au kusoma kwamba tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu kwa maana hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao.Bali haki ipo kwa wale ambao siku zote wanatafuta kuwa na amani na watu wote na pia wale ambao wanaishi maisha  ya utakatifu . Yakobo 1:22 inasema “Lakini  iweni watendaji wa Neno wala si wasikilizaji tu, hali mkijidangaya nafsi zenu”. Neno la Mungu ni jumla ya mawazo na njia za Mungu kwa wanadamu za kuwasaidia kuishi  katika mpango wa Mungu.

Limebeba mapenzi ya Mungu, hukumu, amri, mafunuo na maagizo ya Mungu kwa mwanadamu. Sasa kwa mfano imeandikwa usiue, usizini sasa si yule anayesikia kwamba usiue,au usizini ndiye anayehesabiwa haki bali ni yule asiyeua wala kuzini. Kushindwa kulitendea kazi Neno la Mungu ni kushindwa kuyatenda mapenzi yake maana hayo mapenzi yake yamebebwa kwenye neno la Mungu.

Anaposema enendeni kwa Roho, halafu wewe unaendenda kwa mwili na unajua nia ya mwili ni mauti ,Je unategemea kuurithi uzima wa milele? Kwa lugha nyingine na nyepesi maana yake ni mapenzi ya Mungu tuwe na imani yenye matendo. Ukisema nakiri na kuamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka ili niokolewe, maana yake unatakiwa kutekeleza yale ambayo Yesu anakuagiza maana Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo.

Hebu soma habari hii. Yakobo 2:14 –26 Mstari wa 14 unasema “Ndugu zangu yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je ile imani yaweza kumwokoa? Na ule wa 24 unasema “Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa na haki kwa matendo yake, si kwa Imani peke yake”.

Kumbuka imani inafanya kazi pamoja na matendo yake, yaani kwa kushirikiana na matendo yake. Uzao wa Imani ni – kile ulichosikia (ulichoamini) + matendo yake.
Imani yeyote ile, iwe ni ya Mungu kukuagiza kufanya jambo fulani au iwe ya wewe kuiumba ina matendo yake. “Yakobo 2:22” . Ukitenda kinyume cha hayo matendo yake hautafanikiwa. Mfano:- kama Ibrahimu angemtoa sara kuwa dhabihu kwa Mungu  asingehesabiwa haki na kuwa rafiki wa  Mungu . Tendo la Imani ya Ibrahimu ilikuwa ni kumtoa Isaka. Ndiyo maana Mungu alimhesabia haki.

Mapenzi ya aina yeyote ile ya Mungu kwako yamebebwa katika makundi mawili niliyokutajia. Hivyo jifunze kutulia na kusikiliza uongozi wa Roho Mtakatifu na kisha pili ujifunze kutendea kazi yale ambayo Mungu amesema katika neno lake.

Mtu afanyaye hayo hakika hatakosa kuurithi uzima wa milele. Maana yeye mwenyewe amesema katika Zaburi 32:8 kwamba “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama”. Sasa akikufundisha na kukuonyesha njia Yesu maana yake anakuongoza katika njia ya uzima maana yeye alikuja ili uwe na uzima, kisha uwe nao tele Yohana 10:10.

Neema ya Bwana Yesu na iwe nawe siku zote.

KWA NINI VIJANA WENGI HAWAJAKA KWENYE NAFASI ZAO KI-MUNGU?

September 16, 2006

Na : Patrick Sanga.

Iyohana 2:14

 Kila kundi katika kanisa, jamii na hata nchi Mungu amelipa nafasi na wajibu wake maalumu wa kutekeleza. Pia Mungu anao mtazamo wake binafsi na matarajio yake kwa hayo  makundi

mbali mbali ndani ya nchi. Vijana, watoto, wababa, wazee, wanawake, viongozi wote / yote yana mtazamo wake mbele za Mungu. Ukimuuliza Mungu  nini mtazamo  wako  kwa vijana, atakujibu  soma vizuri IYohana 2:14 maana  yake Mungu anawatazama vijana kama watu wenye nguvu, watu ambao neno la Mungu linakaa ndani yao na pia wamemshinda mwovu.

 Sasa  ukirudi  mazingira  halisi unaona kwa  asilimia kubwa vijana wengi hawako kwenye nafasi ambazo Mungu aliwakusudia. Lengo la somo hili ni :-         Kueleza sababu za kwa nini  vijana wengi hawajakaa  katika nafasi zao.         Kumweleza kijana mambo ya kujiepusha nayo ili  aweze kukaa kwenye nafasi yake.         Kumpa kijana maarifa yatakayomsaidia kurejea kwenye nafasi yake na ili aweze kutekeleza matarajio ya Mungu kwake. Zaidi ujumbe huu umekusudia kulenga na kuelewesha vijana waliokoka, nazungumza  na vijana waliookoka maana hawa ndio ambao Mungu amewatamkia maneno haya au kuwa namtazamo huu juu yao. Zipo sababu  nyingi lakini hizi zifuatazo ni za msingi na zimesababisha wengi kuishi maisha nje ya kusudi la Mungu na kufa bila kutekeleza matarajio ya Mungu  kwao sababu hizo ni:-

         Moja vijana wengi hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu.

 Biblia inasema katika matendo ya Mitume 1:8 kwamba “lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajia  juu yenu Roho  Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika  Yerusalemu, na katika uyahudi wote, na samaria, na hata mwisho wa nchi”. Hivyo vijana wengi hawajakaa katika nafasi zao  kwasababu wengi wa vijana leo makanisani  hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu si kwamba  Mungu hataki kuwajaza lakini shida ipo kwa vijana wenyewe wengine kutotaka kujazwa nguvu hizo, lakini wengine hawajui nini wafanye wajazwe  nguvu za Roho  Mtakatifu  na wengine wanajua lakini hawana kiu ya kujazwa nguvu hizo.

         Pili vijana wengi hawajui namna ya kuenenda kwa Roho .

Paulo kwa warumi anasema” kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” Warumi 8:14 na pia kwa wagatia  anasema” Basi nasema  enendeni kwa Roho hamtatimiza kamwe   tamaa za mwili “Gal 5:16.         Kuna  wengi waliojazwa lakini si wote wanaoenenda au wanaoishi wa Roho. Vijana wengi Mungu amewapa  vitu vizuri  sana ndani yao lakini kwa sababu ya kukosa utiifu na kutoenenda kwa  Roho wameshindwa kusimama kwenye nafasi zao.    

Tatu  vijana wengi wameshindwa kushirikiana  na upako wa Mungu uliodhihirishwa kwao.

Hili ni tatizo kubwa kwa  kweli, Mara nyingi Mungu  amekuwa akiwapa upako, nguvu au uweza wa kufanya mambo  mbalimbali vijana. Sasa si vijana wote  wanaojua  namna  ya kushirikiana  na  huo upako ambao Mungu aliwapa kwa jambo fulani  Mfano, Mungu anaweza akampa kijana upako wa kuomba lakini  kijana  huyo badala ya kuomba yeye anaangalia  mpira, au ni mwanafunzi anatakiwa kusoma na Mungu ameleta upako  huo  sasa yeye anaenda kuomba mambo huwa hayakai hivyo. Upako lazima utumike kwa kusudi  lile  uliotumiwa. Upako wowote unaokuja kwako unakuja kwa kusudi maalumu. 

Nne Kukosa maarifa ya Mungu.

Mungu anasema katika Hosea 4:6 kila kipengele cha kwanza  watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa na pia katika Zaburi 119:9 anasema “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii akilifuata neno lake”. Sasa kwa sababu  nazungumza na vijana naweza nikaweka mistari huu hivi “Vijana wangu wanaagamizwa kwa kukosa maarifa. Maarifa yanayozungumzia hapa ni mafundisho ya neno la Mungu.

Vijana wengi wako  tayari kuangalia mechi mbili mfululizo kuanzia saa nne kasoro usiku hadi saa  nane kwa masaa ya Kitanzania, lakini hawako tayari kusoma Biblia kwa saa moja, wako tayari kuangalia “Movie” za kinigeria, au za kizungu hata masaa matatu (3) lakini si kuangalia na kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu. Na Biblia inasema Apendaye mafundisho hupenda maarifa. Sasa kwa vile vijana wengi hawapendi mafundisho ndiyo maana hawako kwenye kusudi la Mungu. 

Tano, vijana wengi bado wanaipenda dunia,

Mzee Yohana katika 1Yohana 2:15” Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, mtu akiipena dunia kumpenda Baba  hakupo ndani yake”. Na pia  Daudi anasema katika Zaburi  1:1 Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki wala  kusimama katika njia ya wakosaji wala     hakuketi barazani pa wenye mzaha.Ni vijana wachache sana katika  kanisa la leo ambao wako tayari kujikana nafsi zao kwa ajili ya Mungu wengi wanapenda kupoteza muda kwa habari  zisizo za Msingi, wengi wanapenda mzaha na utani, ni vijana wachache  ambao wanaweza kuacha kuangalia mchezo kwenye TV, au  akakataa kwenda kutembea ufukweni kwa lengo  la kuomba, au kusoma Neno, ninachojaribu kusema hapa ni hiki, najua kila jambo lina wakati wake, lakini ni vijana wachache sana waliojizuia katika mambo ya mwili kwa ajili ya kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu.

Sita, Vijana wengi hawajazivaa silaha za vita.

 Waefeso 6:11 Vaeni Silaha zote za Mungu, mpate kuzipinga hila  za shetani.Viajana wengi wameshindwa kumshinda mwovu kwa sababu hawazajivaa silaha za vita. Wengine hawajui silaha za vita ni zipi? Lakini wengine wanajua lakini hawajazivaa. Ile sura ya sita ya waefeso 6:10-18 Paulo anazungumzia silaha za vita, ambazo ni kwlei, haki, amani, Imani, wokovu na Neno la Mungu. Sasa hizi ni silaha na kama ni silaha zina namna zinavyovaliwa na namna zinavyotumika. Sasa si vijana wote waliozivaa silaha, wengi hawasomi neno la Mungu, hawatendi haki, wengi wana imani ya maneno isiyo ya  Matendo.

Saba, Vijana wengi wanaishi bila kuwa na malengo katika maisha yao / maono.

Mithali 29:18. Inasema “Pasipo maono watu huacha kujizuia bali ana heri mtu yule aishikaye sheria”. Hivi leo  ukiwauliza vijana wengi kwamba una maono au hasa malengo gani katika maisha yako? Asilimia kubwa watakujibu  sina malengo  yeyote  yale.Wakati huo huo hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya Yeremia  29 :12. Kwa kila mtu Mungu analokusudi maalum la kumuumba na pia anayo malengo na mikakati ya kumpa huyu mtu atekeleze katika maisha yake. Sasa kwa sababu vijana wengi  hawana na hawajajua  hayo malengo ndio maana wanafanya  kila kinachotokea mbele yao bila kujua  kama ni kusudi la Mungu.

    Naamini  baada ya kuwa umesoma ujumbe huu umepata maarifa ya kukusaidia kukaa katika nafasi yako kama kijana kwa sababu umeshajua sababu za kuktokukaa kwenye nafasi yako.

 

KWA NINI MUNGU ANATAKA TUENENDE KWA ROHO?

September 16, 2006

Na; Patrick Sanga.

 Ukisoma katika warumi 8:14 Biblia inasema “kwa kuwa wote wanaoongozwa  na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” na pia Paulo kwa wagalatia anasema” Basi nasema Enendeni kwa Roho,wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili Wagalatia  5:16. 

Hapa tunaona jinsi Paulo anavyosisitiza kwa makanisa ya Rumi na korinto kuhusu suala zima la kuongozwa  na Roho  Mtakatifu. Anawaambia warumi kwa  kuwa wote wanaongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana  wa Mungu maana yake haijalishi  ana umri gani, ni wa dhehebu gani, jinsia gani maadamu anaongozwa  na Roho wa Mungu huyo ni mwana wa Mungu na bado anawaagiza wagalatia akisema Basi nasema  enendeni   kwa Roho………….. anaposema enendeni maana  yake  mkiongozwa  na Roho, au mkimfuata  Roho katika yale anayowaagiza. Maneno haya yanaonyesha  zipo sababu za msingi  kwa nini tunatakiwa kuongozwa  na Roho  sasa hapa sizungumzii kazi za Roho mtakatifu najua zipo kazi nyingi anazozifanya Roho Mtakatifu lakini mimi nazumgumzia sababu za kuongozwa  na Roho Mtakatifu, ambaye ndio agano jipya la Mungu kwetu (Yeremia 31:31) katika hiyo Yeremia Neno linasema “Angalia siku zinakuja asema Bwana nitakapofanya  agano jipya na nyumba ya Israel. Sasa ukiendelea kusoma mistari inayofuata utaona anazungumzia habari za kutia sheria yake katika mioyo ya watu.

Sasa hili ndilo agano jipya la Mungu pamoja na wanadamu. Sasa usipojua kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho na siyo akili zako, au mazoea, au taratibu za kwako n.k. hautajua umuhimu wa kuongozwa na Roho Mtakatifu na pili hautaona sababu za kuongoza na Roho Mtakatifu. Sasa  lengo la ujumbe huu ni kukufundisha sababu za msingi  za kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na siyo akili  zako au mawazo yako. Sasa baada ya utangulizi huo mfupi na tuangalie sababu hizo za msingi. 

Moja,

Ili tusizitimize tamaa za mwili wagalatia 5:16

“Basi nasema enendeni kwa Roho , wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Tunatakiwa tuenende kwa Roho ili tusizitimize tamaa za mwili. Siku zote mwili na Roho ni maadui nia ya mwili ni mauti na nia ya Roho ni uzima na amani (Warumi  8:7). Maana  yake siku zote mwili utakuongoza kufanya mambo ambayo mwisho wake ni mauti ya kiroho na  hata kimwili pia.

Utakuongoza katika  tamaa zake, sasa usipoongozwa na Roho huwezi  kujizuia kutekeleza tamaa za mwili na kwa sababu hiyo wewe si mwana wa Mungu   na mtu wa namna  hii hataingia mbinguni kamwe.  Katika 1Wakorinto 6:9-10 anasema “Au  hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme  wa Mungu? Msidanyanyike, waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala  waabudu  sanamu, wala wazinzi, wala  wafiraji, wala walawiti, wala walevi, wala watamanio, wala walevi wala   watukanaji, wala wanyang’anyi.Sasa utakapoongozwa na Roho Mtakatifu utaratibu wake utakuacha huru mbali  na hayo mambo ya mwili au nia ya mwili na utakuongoza katika uzima  na amani  na kulitenda tunda la Roho ambalo  ni upendo, furaha, amani, uvumilivu utu wema  , fadhii, uaminifu, upole na kiasi “Wagalatia 5:22-23”.

 Mbili,

Ili tupate kuyaelewa mafumbo ya Mungu  na kuyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni.

1Wakorinto 2:10 inasema “ Lakini  Mungu  ametufunulia  sisi kwa Roho, maana Roho huchunguza yote hasa mafumbo ya Mungu” na ule mstari wa 13 unasema “ Nayo twayanena , si kwa maneno yanayofundishwa  kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa  na Roho, tukiyafasiri mambo ya Rohoni  kwa maneno  ya Rohoni. Hapa najua walio  wachungaji, walimu  wa neno la Mungu au viongozi wa vikundi mbalimbali vya kiroho watanielewa zaidi.

sikiliza Roho Mtakatifu ndiye mwenye uwezo wa kuchunguza kilichopo kwenye ufahamu wa Mungu kuhusu wewe, ndoa yako, kanisa lako, biashara yako, masomo yako, nchi  yako n.k. sasa akishachunguza ndiyo anakujulisha maana wewe ulikuwa hujui. Pia Roho Mtakatifu ndiye  anayekusaidia kuyanena, kuyafundisha au kuyafafanua maneno ya Mungu kwa  watu wake,  anaposema kuyafasiri  maana yake kuyafundisha mambo ya Rohoni kwa jinsi / namna ya Rohoni.

 Hivyo kama  wewe ni kiongozi au mwalimu wa neno  la  Mungu, ukiongozwa na Roho, yeye atakuongoza / atakusaidia kuwafundisha hao watu neno la Mungu kwa jinsi  ya Rohoni yaani kwa mfumo wa Rohoni kulingana na watu ulio nao, maana yeye ndio mtunzi wa hilo Neno,soma mwenyewe 2Petro 2:21” maana  unabii haukuletwa popote kwa mapenzi  ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Tatu,

 

Ili   tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu na kuyapokea mambo ya Roho na Mungu .

Iwakorinto 2:12 inasema “Lakini sisi hatukupokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa  na Mungu” na ule wa 14 unasema “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei  mambo ya Roho wa Mungu maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya Rohoni. Unapoongozwa  na Roho Mtakatifu ndipo anapokusaidia kujijua wewe mwenyewe vizuri. Anaposema  upate kuyajua yale ambayo Mungu amekupa katika maisha yako.Roho mtakatifu atakusaidia kujua aina ya vipawa  ulivyonavyo, karama za Rohoni ulizonazo, huduma ulizonazo kama umeitwa huko, atakusaidia kujua vizuri unaweza kufanya  nini na nini  huwezi, kipi ufanye  na kipi usifanye, atakusaidia kujua baraka zako za kiroho  na kimwili pia. Kwa kifupi  atakusidia kulijua kusudi   la Mungu katika maisha yako na vipi ufanye ili uweze kulifikia hilo kusudi na zaidi  atakupa upako/ nguvu za kuweza kuyapokea yale yote anayo kuagiza ili uweze kulifikia kusudi lake kwako na kuzirithi baraka zako maana katika zaburi 32:8  anasema “Nitakufundisha  na kukuonyesha njia utakayoienda nitakushauri, Jicho langu likikutazama”.

 Nne,

Ili atusidie kuomba yale tunayotakiwa kuyaomba kwa wakati huo.

Warumi 8:26” kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua   kusikoweza kutamkwa”. Udhaifu unaozumgumziwa ni wa namna  mbili moja si rahisi kwa jinsi  ya  mwili kuomba kwa muda mrefu kwa sababu mwili ni dhaifu na pili udhaifu tulionao ni kushindwa kuomba jinsi inavyotupasa kuomba.

 Sasa  tunapoongozwa na Roho, maana yake moja anatusidia tuweze kuomba na zaidi anatufundisha namna ya kuomba  na kutuongoza  yapi tuyaombee kwa wakati huo  au kipindi hicho. Mfano wewe unaweza ukawa unaomba upako wa Roho Mtakatifu katika huduma na yeye  Roho Mtakatifu, anajua kwamba  ameshakutia mafuta  na shida uliyonayo ni kutokujua namna ya kushirikiana na upako wake ulio juu yako. Hivyo yeye atakuongoza kuomba kwa habari ya kushirikiana  na upako aliouweka juu yako. Kwa  kifupi yeye kwa sababu ndiye mwenye maisha yako atakuongoza siku zote kuomba yale unayotakiwa kuyaomba kwa majira hayo iwe kuhusu masomo, ndoa, kanisa, nchi n.k.

Tano,

Ili atuongoze katika kufanya maamuzi.

 2Wakorinto 3:17  Basi Bwana ndiye Roho, walakini alipo Roho  wa Bwana, hapo ndipo penye  uhuru”  pia ukisoma warumi 8:1-2 inasema  “sasa, basi hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu, kwa sababu sheria ya Roho wa uzima  ule ulio katika kristo Yesu imeniacha huru, mbali  na sheria ya dhambi na mauti”  kufanya maamuzi ni sehemu  ya maisha ya mwanadamu. Yapo  maamuzi  mengi sana  ambayo mwanadamu anatakiwa kufanya na hawezi kukwepa kuyafanya.

Sasa Mungu kwa kulijua  hilo ametupatia Roho Mtakatifu ili atusaidie katika kufanya  maamuzi. Roho Mtakatifu anapokuwa Bwana   kwako, yaani  mtawala, kiongozi ndipo anapokupa uhuru juu ya kufanya maamuzi katika maisha yako. Maana yake ulikuwa hujui nifanye nini? Niamueje ? Sasa yeye anakuletea uhuru ndani wa  kufanya jambo ambalo anajua ni la mafaniko  kwako. Kumbuka siku zote nia ya Roho ni uzima na amani.

 Huenda ziko sababu nyingi ni kwa nini unatakiwa uenende  kwa Roho, lakini hizi tano ndizo Mungu alizonipa tuweze kushirikiana kujifunza. Ni imani yangu kwamba utakapoamua kutaka na kupenda kuongozwa na Roho ndipo utakapoona Mungu akijifunua kwako .

 

Tuendelee  Kuombeana