MAMBO YA KUFANYA/KUZINGATIA KATIKA KIPINDI CHA UCHUMBA

 Patrick & Flora Sanga

Mpenzi msomaji tunakusalimu kwa jina la Yesu!

Baada ya kuwa tumepata maombi ya vijana wengi kutaka kujifunza habari za Uchumba, mke wangu pamoja nami tumeona ni vema tukaandaa somo hili ambalo tunaamini litafanyika msaada kwa vijana wengi ambao wapo kwenye uchumba au wanajiaandaa kuingia katika eneo hili. Hata hivyo somo hili ni pana sana, kwa sasa tumeandika vitu vichache vya msingi, tunaamini kwamba huko mbele tutaandika kitabu chake rasmi.

Katika kitabu cha Muhubiri 3:1 Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”. Hivyo mwanadamu katika maisha yake hapa chini ya jua  kuna vipindi mbalimbali anavyovipitia hii ni pamoja na kipindi cha uchumba kwa sehemu kubwa ya watu.   

Katika kipindi hiki yapo mambo mengi ambayo wachumba hufanya, mengine ni mazuri na mengine hayafai kabisa. Na hii yote inatokana hasa na mitazamo au tafsiri ya uchumba kwa watu husika. Fahamu kwamba tafsiri unayokuwa nayo juu ya mchumba wako ndiyo inayokuongoza kujenga mahusiano ya aina fulani pamoja naye.

Lengo la somo hili ni;

Kuongeza ufahamu wa wachumba kuhusu kipindi hiki na Kuwapa vijana maarifa ya kuwasaidia kuishi kwa nidhamu ya Ki-Mungu katika uchumba wao. Pia ni kuwafikirisha vijana wanaotarajia kupita katika kipindi hiki mambo ya kuzingatia. Si wachumba wengi wanajua, Mungu anawataka wafanye nini katika uchumba wao au kwa lugha nyingine si wachumba wote wanaojua kwa nini kipindi cha uchumba kipo. Naam katika somo hili tumeandika mambo hayo kinaga ubaga.

Kwa kuwa suala la uchumba ni pana na lina mitazamo mingi, yafuatayo ni mambo tuliyozingatia katika uandishi wa somo hili;

  • Kuna makundi mbalimbali ambayo yana taratibu zao kuhusu mchakato wa mtu kumpata mke au mume kikiwepo kipindi cha uchumba. Makundi hayo ni pamoja na makanisa, makabila, familia nk.
  • Wachumba wanaweza kutofautiana kwa kiwango cha elimu, uchumi, ufahamu juu ya mambo mbalimbali, kikabila, umri na hata kwa rangi pia.
  • Kuna baadhi ya wachumba hadi kufikia muda wanakubaliana kwamba watakuja kuishi pamoja walishafahamiana tangu zamani na wengine hawakufahamiana.
  • Wachumba wanaweza wakatoka katika madhehebu/makanisa tofauti na hili ni kwa kuzingatia madhehebu/makanisa mengi yaliyopo.

Lengo letu ni kuandika juu ya mwongozo wa Neno la Mungu katika kipindi cha uchumba. kwa lugha nyingine, je Mungu anataka wachumba wafanye nini katika kipindi chao cha uchumba?. Kumbuka uchumba ni kipindi/wakati. Basi kama ni wakati jua kabisa kuna baadhi ya mambo ambayo ni lazima yafanyike, kwani Biblia inasema katika Mhubiri 8:5b “ Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu”, neno hukumu linamaanisha maamuzi, mambo ya kufanya.   

Yafuatayo ni mambo ya msingi kufanya katika kipindi cha uchumba;

Jambo la kwanza –  Mruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana wa uchumba wenu

2Wakorinto 3:17 ‘Basi Bwana’ ndiye Roho; na alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru’.

Kumbuka Roho Mtakatifu ni msaidizi. Hivyo basi ni vema kumtumia vema hasa katika nyanja hii ya mahusiano katika kipindi hiki cha uchumba. Ni Roho Mtakatifu pekee mwenye uwezo wa kukujulisha mambo na siri nyingi kuhusu mchumba wako hata kama yeye hataki kukueleza. Ukimruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana, yeye atakuongoza katIka kufanya maombi yanayolenga maeneo ya msingi juu ya huyo mwenzako. Kila mtu ameumbwa pamoja na mapungufu fulani au kwa lugha nyingine mapungufu/ udhaifu (weakness) ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Roho Mtakatifu anapokuwa Bwana wa mahusiano yako yeye atakusaidia kuona madhaifu au mapungufu ya mwenzako kama kitu cha wewe kujivunia(Strength) kwa maana ya kuona udhaifu wa mwenzako kama kitu chema na si kibaya.

Kumbuka Paulo katika 2Wakorinto 12:9-10. —‘Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ….kwa hiyo napendezwa na udhaifu——- maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. Hivyo Roho Mtakatifu atabadilisha tafsiri ndani yako za vyote unavyoona kwa mwenzako huenda juu ya umbile lake, umri wake, macho yake, kabila lake viwe vitu vya wewe kujivunia. Zaidi Roho Mtakatifu pia atakuongoza katika maombi yatakayosidia kuuondoa ule udhaifu ambao umekuja si katika mapenzi ya Mungu, yaani wa kishetani.

Jambo la pilini wakati wa kuweka msingi imara wa uchumba wenu na kufahamiana zaidi.

Hili jambo ni la muhimu  kuzingatia. Ni vema wachumba wakatafsiri na kuelewa vizuri maana ya uchumba. Wachumba wanapaswa kuwa na mipaka fulani katika uchumba wao na  kuwa makini kwa kujilinda na mazingira ya kila namna ambayo yanaweza yakapelekea wao kuanguka dhambini. Ni vema mkajua kwamba ninyi ni wachumba na si wanandoa. Na kama ni wachumba basi uchumba una mipaka yake na hamruhusiwi kufanya mambo ya wanandoa. Mipaka hii iwe kwa habari ya kutembeleana,kupeana zawadi, mawasiliano (ingawa mnapaswa kuwa makini na lugha mnazotumia pia) nk.  Lengo la kutafsiri misingi ya mahusiano yenu ni kujiwekea mipaka na mazingira yatakayowasaidia kuishi maisha ya nidhamu, ushuhuda na kumletea Mungu utukufu.

Sambamba na hili sehemu kubwa ya wachumba huwa wanakuwa hawafamiani vizuri. Japo wapo baadhi ambao walianza tangu shule za msingi/sekondari/chuo na sasa wamechumbiana hivyo kwa sehemu wanafahamiana vema. Kwa wale wasiofahamiana vema huu  ni wakati wa kumjua mwenzako vizuri kwa maana ya kabila lake, familia yake, umri wake, interest zake, matatizo aliyo nayo yeye binafsi au ya kifamilia, mitazamo yake juu ya mambo mbalimbali kama uchumba, ndoa, maisha, wokovu, neno la Mungu nk. Huu ni wakati wa kumjua mwenzako kwa njia ya maswali mbalimbali ya msingi yanayohusu vitu nilivyovitaja hapo juu. Lengo hapa ni kujua mapungufu/madhaifu(weakness) na mazuri(Strength) za mwenzako ili mjue namna ya kukabilana na mapungufu na namna ya kuendeleza yaliyo mazuri.

Ni vema pia kuulizana historia zenu za maisha ya nyuma. Kabla ya kuokoka umepitia katika mifumo gani ya maisha ambayo imechangia kukufanya uwe ulivyo. Kabla ya kumpata uliye mpata ulikuwa umefuatwa na wangapi na uliwakubalia au la, na kama uliwakubali kwa nini mliachana, na sasa wako wapi, je bado wanakufuatilia. Hii itawasaidia sana kujipanga vizuri kimaombi na katika mahusiano yenu na zaidi itawasaidia kuweza kuchukuliana na kuhifadhiana katika madhaifu ya kila mmoja. 

Mungu anapowaunganisha anakuwa na kusudi maalum. Hivyo jua kwamba huyo mwenzi uliyepewa umepewa kwa ajili ya kusudi fulani la Mungu. Ni wachumba wachache sana ambao pindi wanapokutana kila mmoja anakuwa anajua walau kwa sehemu kwa nini aliumbwa. Sasa ni vema mkae chini mfikiri, nini Mungu anataka kukifanya duniani kupitia ninyi? Na zaidi angalieni kazi zenu au yale mnayoyasomea, Je mtawezaje kuliimarisha agano la Bwana kwa pamoja kama mke na mume?.

Hapa maana yetu mnatakiwa kujibu maswali yafuatayo? Je ni kwa nini mlizaliwa? Je kwa nini Mungu amekuunganisha na huyo uliye naye sasa? Na je kupitia elimu, bisahara zenu au kazi mlizonazo mtawezaje kuimarisha agano la Bwana?, Kwa kuzingatia vipawa na uwezo Mungu aliowapa, je ni wapi Mungu anataka kuwapeleka na kuwafikisha? Kama ndani yenu mna huduma fulani, je ni watu gani ambao Mungu atataka mshirikiane nao katika huduma hiyo?, je ipi ni nafasi yenu katika mwili wa Kristo na taifa kwa ujumla? Ni vema zaidi mwanaume akajua wito/ kusudi aliloitiwa ili pia amshirikishe na mwenzake.

Kufanikiwa kwa hili kunahitaji uwepo muda wa kutosha wa wachumba kukutana ili kupanga na kuweka mambo yao mbalimbali, na kama ni watu walioko mbali basi suala la mawasiliano kwa njia mbalimbali kama simu, barua pepe, na barua na hata zawadi ni la muhimu.

Jambo la tatu– ni wakati wa kulinda wazo la Mungu hadi litimie.

Siku zote uamuzi wowote unaoufanya una gharama. Naam uchumba pia una gharama nyingi Sana za kuzikabili kuliko unavyofikiri. Gharama hizo ni pamoja na muda, pesa, mawasiliano, maombi, uhuru nk. Kumpata mchumba au mwenzi ambaye ni wa kusudi la Mungu, usidhanie ndio umemaliza. Kama huo uchumba wenu ni wa mapenzi ya Mungu muwe na hakika mtakutana na vita kubwa sana katika kipindi hicho cha uchumba na lengo ni kuwatenganisha. Ni lazima mjifunze siku zote kuombeana kwa kumaanisha maana Shetani naye yupo kazini ili kuvuruga hayo mahusiano.

Kumbuka huyo mwenzi ni agano toka kwa Bwana hivyo unawajibika kumlinda, kumlinda ni pamoja na kuhakikisha wewe hausabibishi au haufanyiki chanzo cha ninyi wawili kuanguka dhambini, au ukamwacha na kumsababishia majeraha ya nafsini na hivyo kuharibu mahusiano yake na Mungu. Wapo watu waliofikia kuharibu mahusiano yao na Mungu kisa mchumba, saa ya ibada imefika mchumba anasema twende zetu out bwana, unataka kufanya maombi ya kufunga mchumba anasema kesho nitakutoa out, inagharimu sana muda wa kuwaza pia kwa ajili yake na familia yake au mahitaji mbalimbali aliyo nayo.

Zaidi pia uchumba unaweza kukunyima uhuru hata wa kuwa na maongezi na rafiki zako, maana kuna baadhi ya watu huwa hawataki kuona mchumba wake anaongea au kucheka na watu wengine, na pia kuna wengine ni wachumba lakini wamewekeana taratibu ngumu utafikiri wanandoa kabisa na ukweli zinawatesa ila kwa sababu hataki kumpoteza huyo mchumba wake inabidi avumilie.  Jambo tunalosisitiza hapa ni kwamba, uchumba una gharama nyingi angalia mahusiano yako na Mungu yasiharibikie hapa.

Jambo la nne– ni wakati wa kupanga malengo na mikakati yenu ya baadae.

Mithali 29:18a “Pasipo maono, watu huacha kujizuia’

Hili si jambo ambalo vijana wengi hulipa kipaumbele linavyostahili. Katika hili ni vema wachumba wafikirie mapema ni aina gani ya maisha ambayo wangependa kuwa nayo, na pia je ni aina gani ya ndoa wanataka kufunga, tatu je ni wapi wangependa kuja kuishi kwa maishayaoyote. Haya yatawasaidia wahusika kujipanga ndani na nje kukabiliana na yaliyo mbeleyao.Kamawanataka kufunga harusi kanisani basi maana yake wanahitaji kuwa na maandalizi mazuri kifedha, waweke katika muda kila wanalotaka kuelekea katika harusiyaoili iwasaidie kujiaadaa mapema. Malengo yoyote yale ambayo mtaweka basi hakikisheni yanatekelezeka, yanafikika, yanapimika na mnayapangia muda wa utekelezaji.

Mambo zaidi ya kuzingatia katika malengo yenu;

Katika hili ni vizuri wachumba waangalie nafasi yao kifedha imekaaje, na changamoto zinazowakabili wote kwa pamoja. Je hali yao kifedha inawaruhusu kuzikabili gharama za maandalizi ya ndoa kwa ujumla. Je hali ya kimaisha ya kijana wa kiume inamruhusu wakati wowote baada ya kuchumbia aweze kufunga harusi kama anataka. Je nafasi zao kielimu zikoje, je kama zinatofautiana ni kwa kiwango gani? Na je tofauti zao kiuchumi na kitaaluma zinaweza kuwa kikwazo kwao kuoana, au kwa wazazi wao nk. Na je baada ya kuwa wamegundua na kupima uwezo wao katika hayo mambo mawili, je wanaweza wakasaidianaje ili wafike mahali pazuri wote wawili.

Vijana wengi wa kiume huwa wanakosea sana hapa, wengi huwa wanasema sitaki kuchumbia/kuoa mpaka niwe nimesha jikamilisha kiuchumi, niwe angalau na maisha mazuri. Sisi hatushauri sana dhana hii, ukweli ni muhimu kwa kijana wa kiume akjikamilisha kwa yale mambo ya msingi. Lakini fahamu kwamba kuna wakati mwingine kuendelea kwako kiuchumi, au kuvuka kwako kimaisha ni rahisi zaidi pale unapokuwa na mchumba au ndoa yako. Tunasisitiza tena ni vema wachumba wakae chini na kufikiri ni kwa namna gani wataendelezana kiuchumi na kitaaluma. Angalizo, ni vema uwe na uhakika kweli huyo mtu ni wa mapenzi ya Mungu kwa maana ya kuwa ni wa kwako kweli, maana wapo wachumba ambao wamekuwa wakisaidiana mpaka kulipiana ada, kupeana mitaji, kununuliana nyumba, magari nk, halafu mwishowe mmoja anavunja maagano, maumivu yake ni makubwa sana.

Jambo la tano – ni wakati wa matengenezo na kuzijenga nafsi zenu

Wachumba wengi huwa wanafichana mambo mengi sana wanapokuwa wachumba na matokeo yake hawayashughulikii mapema na hivyo yanakuja kuwaletea shida kwenye ndoa. Huenda kabla hujakubaliwa wewe tayari mwenzako alikuwa amesha wakubali vijana au mabinti wengine kwamba ataolewa nao au kuwaoa. Pia  kama ni msichana huenda ameshawahi kubakwa, au kutokana na masumbufu ya kupata mtu sahihi na wakati mwingine kuachika mara kwa mara imefika mahali huyo msichana akasema sitaki kuja tena kuolewa. Zaidi  huenda  mmoja wenu huko nyuma ameshawahi kufanya uasherati au zinaa kabla hamjachumbiana. Au kuna mwingine amekuwa akisumbuliwa na tatizo la harufu, kufanya tendo la ndoa na mapepo nk.

Haya yote na mengine mengi yanayofanana na haya yana athari kubwa sana kiroho na kimwili kwenu kama wachumba na wanandoa watarajiwa kama hayatashughulikiwa vema katika kipindi hiki cha uchumba. Licha ya kuwa na athari mambo hayo yamepelekea nafsi za watu au wachumba wengi kujeruhika. Nafsi inapojeruhiwa inaharibu ndani ya mtu mfumo wa kufanya maamuzi, mfumo wa utiifu kwa Mungu wake, mfumo wa kunia na kuhisi pia. Sasa mifumo hii inapoharibika inapelekea watu kufanya maamuzi ambayo yapo nje ya mapenzi ya Mungu kabisa. Nawajua baadhi yao ambao wameacha na wokovu, na, wengine wamekata tamaa ya kuolewa, wapo walioamua kuolewa na mataifa ilimradi ameolewa nk.

Hivyo basi tumieni wakati huu kufanya matengenezo na kujengana nafsi zenu kwa maana ya kuombeana sana, pili kwa kuongeza ufahamu wenu katika neno  la Kristo hasa maandiko yanayolenga uponyaji katika nafsi zenu, tatu kufuta na kufisha mapatano/maagano yote ambayo mmoja wenu aliyafanya huko nyuma na watu wengine na pia kufuta picha za kubakwa na kujenga ufahamu wa mtu aliyeathirika kisaikolojia kutokana na mambo kama hayo kwa njia ya Damu ya Yesu. Hatua hizi zitawasaidia kurejesha mifumo iliyoharibika na kuziruhusu nafsi zenu zifanye kazi kama inavyotakiwa. 

Jambo la sita – ni wakati wa kujua taratibu mbalimbali kuelekea kwenye ndoa

Tumeshasema, kila dhehebu au kabila wana taratibu zao kuhusu uchumba hadi ndoa. Hivyo ni vema wachumba, wakafuata taratibu ambazo zimewekwa na makanisa yao hasa zile ambazo zipo katika mapenzi ya Mungu. Lakini pia lazima tukubali kwamba kuna baadhi ya taratibu za makanisa, makabila na hata madhehebu ambazo nyingine zipo tu lakini hazitekelezeki na nyingine hazimpendezi Mungu.

Sasa ni vema wachumba wazijue hizo taratibu na wajue je wanaweza kuzitekeleza au la, na kama hawawezi wafikirie kabisa wanafanyeje. Mfano kuna baadhi ya makanisa ambayo hayaruhusu mtu wa kwao aoe au kuolewa na mtu wa nje ya dhehebu hilo. Sasa hii ina maana kama una mchumba wa aina hiyo jipange kujibu maswali ya wazee wa kanisa na Mchungaji vizuri. Na zaidi kuna baadhi ya makabila na familia hazitaki uoe au kuolewa na watu nje ya kabila lako, au aliyekuzidi umri kama wewe ni kijana wa kiume nk. Hivyo ni vema kuzijua hizo taratibu ili mjue mnajipangaje kukabiliana nazo. Ushauri wetu ni huu kama una uhakika huyo mtu ni wa kutoka kwa Mungu basi simamia la Bwana maana lipi jema, kumpendeza Mungu au wanadamu?. Kumbuka Mungu ndiye mwenye ratiba ya kila mmoja wetu.

Suala la  kukagua/kupima afya zenu kwa pamoja.

Kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa suala la ukimwi limechukua sura mpya na kuleta mtafaruku ndani ya kanisa hasa kwa vijana wanochumbia kabla ya kupima afya zao. Siku hizi jambo hili limewafanya wachungaji kuomba sana kwa habari ya vijana ndani ya kanisa. Sasa kama mlikuwa hamjapima afya zenu mpaka mmechumbiana basi chukueni hatua mwende kupima. Ni vema wachumba wakapima mapema afya zao ili jambo hili lisije likawaletea shida baadaye, maana kwa sheria ya nchi yetu wachungaji hawaruhusiwi kufungisha ndoa kama mmoja wa wahusika ameathirika.

Upimaji wa afya zenu ni wa muhimu kwani, ndani ya makanisa kuna rekodi ya vijana wengi tu ambao wameshaathirika na huenda si kwa sababu ya zinaa, maana kwa mujibu wa watu wa afya njia za maambukizi ni nyingi. Kuna wengine wamezaliwa nao, kwa nia ya kuongezewa damu,kutumia vifaa kama nyembe, sindano nk. Hata hivyo swali la msingi inabaki kwamba je, liko tumaini kwa mtu aliyeathirika kuoa au kuolewa?   

Tukueleze hivi, hakuna jambo gumu lolote la kumshinda Bwana, hii ni pamoja na ukimwi, kama Mungu alimfufua Lazaro, alitenganisha bahari ya Shamu na watu wakapita, kama Yesu alitembea juu ya maji, basi naomba ujue kwamba Ukimwi hauwezi kuzuia kusudi la Mungu hapa duniani kwa wale awapendao na kwa sababu hiyo tunasema hata kama mtu ana ukimwi na Mungu bado ana kazi naye hapa duniani, hakika atamponya huo ukimwi na atampa mke au mme.

Faida na lengo la kupima ni hili, hata kama majibu yatatoka mmoja ameathirika isiwe mwanzo wa ninyi kuachana. Kama mna uhakika Mungu aliwaanganisha huu ndio wakati wa kurudi mbele za Mungu kwa maombi ya uponyaji na kujipanga zaidi juu ya hilo. 

Jambo la saba – ni wakati wa kuongeza ufahamu wenu kuhusu nafasi yako kwenye ndoa.

Je umeshawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu anakupa mke au mme? Yamkini zipo sababu nyingi lakini baadhi yake ni; Mungu anakupa mke kama msaidizi, mlinzi, na pia unapopata mke au mme unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana na pia ni kwa sababu ya zinaa ndio maana unahitaji mwenzi. Hizi ni baadhi ya sababu zilizoko ndani ya Biblia. Hivyo basi tafuteni wanandoa mnaowaamini na zaidi waliokoka  muwaulize   kuhusu wajibu  wa kila mmoja kwa nafasi yake kwenye ndoa. Katika hili baadhi ya makanisa  huwa yana utaratibu wake wa nani atahusika na maelekezo ya aina hii kwa wachumba. Hivyo kama kanisa lako lina utaratibu huo, fuata huo utaratibu.

Katika ndoa kuna mambo mengi sana ambayo mtatakiwa kufanya, ni vema kufuata mwongozo na ushauri wa viongozi wenu au wachungaji wenu kuhusu nini mnatakiwa kufanya katika ndoa yenu. Angalizo hapa ni hili, uwe makini na vyanzo vya ushauri au mafunzo katika eneo hili ili lisije kuleta madhara baadae. Usitafute wala kufuata kila ushauri, bali sikiliza pia uongozi wa Mungu ndani yako.

Jambo la nane– Msifanye tendo la ndoa, maana jambo hili litaharibu mpango wa Mungu na kusudi lake kupitia ninyi.

Wakati wa uchumba, si wa kufanya mapenzi au kufanya michezo ya mapenzi. Tunarudia tena ili kuonyesha msisitizo kwamba chonde chonde jamani, uchumba sio ndoa, maana uchumba unaweza kuvunjika. Hairusiwi kabisa kwa wachumba kufanya mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa kabla ya ndoa. Kitendo cha Mungu kukujulisha/kukupa huyo mwenzako kama mke/mume mtarajiwa haina maana mna haki ya kufanya mambo ya wanandoa. Mungu kukupa huyo mwenzako sasa ni taarifa kwamba  huyu ndugu ndiyo atakuwa mkeo au mmeo na anakupa taarifa sasa ili ujipange kufanya mambo ya msingi mnayotakiwa kuyafanya katika kipindi cha uchumba. Kipindi cha uchumba ndicho kipindi ambacho wachumba wengi sana wanavuruga kusudi la Mungu, na kuharibu maisha yao ya baadae na ndoa yao kwa ujumla.

Ndoa nyingi sasa hivi zina migogoro kwa sababu wakati wa uchumba walidiriki kufanya tendo la ndoa. Vijana wengi hawajajua kufanya tendo la ndoa kipindi cha uchumba lina madhara gani kwao na ndio maana wengine wanafanya. Biblia inasema katika Mithali 6:32 “Aziniye na mwanamke hana akili kabisa, afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake mwenyewe”. Hata kama ukifanya tendo la ndoa na mchumba wako ambaye mlibakiza siku moja kufunga harusi, bado umezini.

Ndani ya nafsi ya mtu kuna akili, hisia, nia na maamuzi. Biblia inaposema afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake ana maana hii, dhambi hii inapofanywa, ina haribu mfumo wa utiifu na uamnifu kwa Mungu wako, inapelekea kukosa usikivu wa rohoni kabisa, ina haribu mfumo wa kufikiri, kunia na kufanya maamuzi. Na kwa sababu hiyo si rahisi tena kusikia na kutii uongozi wa Roho Mtakatifu. Kwa watu ambao wamezoea kuwa na mahusiano mazuri  na Mungu watanielewa ninachosema hapa.

Zaidi kuna baadhi ya wachumba kweli hawafanyi tendo la ndoa bali wanafanya michezo ya mapenzi. Michezo ya mapenzi (Fore play) ni maalum kwa ajili ya wanandoa, na ni sehemu ya tendo la ndoa. Hivyo kufanya michezo ya mapenzi ni kufanya mapenzi kwa sababu ile ni sehemu ya mapenzi. Kuna vitu unavichochea,  unaamusha hamu ya mapenzi au unayachochea mapenzi. Biblia inasema katika Mhubiri 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala  wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe.”

Mungu pia anachukia michezo ya mapenzi soma Isaya 57:4-5 “Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani, juu ya nani mmepanua vinywa vyenu, Na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi….. Wachumba wengi hawajui haya kwa sababu si makanisa yote yanayofundisha maswala ya mahusiano ya wachumba kimpana.

Mpaka hapa tunaamini umeshajua hasara za jambo hili  na utazijizuia kabisa kulifanya. Michezo ya mapenzi ni pamoja na kunyonyana ndimi, kushikana sehemu ambazo zinaamsha ashiki ya mapenzi kama sehemu za siri, matiti, kiuno nk, pamoja na kuangalia picha za ngono. Katika kipindi ambacho tumemtumikia Mungu kupitia vijana tumejifunza na kukutana na kesi mbalimbali za aina hii na kuona namna Shetani anavyovuruga mpango wa Mungu kwa vijana. Mwenye sikio na asikie neno ambalo Roho wa Bwana awaambia vijana ili kulida kusudi la ndoa.

Ni imani yetu kwamba mambo haya nane yameongeza ufahamu na hivyo kuwa maarifa ya kutosha kukusaidia kuenenda kwa mapenzi ya Mungu katika kipindi cha uchumba.

Bwana awabariki

163 comments

  1. Mtumishi naamini alichokiweka Mungu ndani yako kinatumika ipasavyo. Naamini wale Vijana wenye masikio ya rohoni wanasikia hata sisi wenye ndoa, maana tunayachukua kuwafundisha watoto wetu ili wakue kwa njia ipasayo.

    Like

  2. Mtumishi Mungu wng akubariki nimebarikiwa sana na ujumbe huu mimi nina mchumba wng naamini ni Mungu kanionyesha ujumbe huu nahitaji maombi ili nami niifikie hiyo ahadi ya Mungu kwetu ya kuwa mke na mume ubarikiwe any news please send to me through ma e-mail amen. From Morogoro I’m so happy.

    Like

  3. Amina. Thanks for your good advice to youth and I appreciate it. please produce another MODULES concerning the same issue on above.
    I request you to make an attachment for me through my e-mail: valentine_joachim@yahoo.com

    ALIYEKUUMBA AKULINDE NA KUKUONGOZA DAIMA

    Like

  4. Mtumishi nimesoma somo lako la namna ya kumtambua mchumba na hili la sasa, kwa kweli mimi huwa ninafurahi sana ninapokutana na kweli hata kama inanigharimu kiasi gani. Kwa kweli mtumishi kwa sasa nahitaji kumjua mke wangu nahitaji msaada wa maombi yako.

    Like

  5. nimesoma vitabu vingi vya mausiano lakini sijawai kubarikiwa kama nlivyo barikiwa leo mungu azidi kukutunza

    Like

  6. shaloom nimebarikiwa sana na hili somo,nilitamani sana kua na uchumba wa namna hii lakini shetani alifanikiwa kuniingilia nakuanguka dhambini hadi nikapeta mtoto nje ya ndoa na baada ya apo mwanaume amekua mzito kujitambulisha nyumbani wala kufanikisha ndoa nimebaki naumia sana nashindwa nifanyaje naona kama sina jinsi na ndoto zangu zimeishia apo.

    Like

  7. Nimebarikiwa sana na mafundisho haya, natoa WITO kwa VIONGOZI wa makanisa wawe wanatoa mafundisho ya namna hii kwasababu hali tuliyonayo ni mbaya sana mbele za MUNGU.

    Like

  8. Hongera sana kwa kuelimisha jamii, ila mimi nina swali, mpenzi wangu nampenda sana na naamina ananipena na tunategemea kuoana je kwakuwa tumewahi kulala kitanda kimoja jabo hili linaweza kusababisha tusifikie malengo ya kuoana? tafadhali naomba nisaidie

    Like

  9. Mtumishi nimebarikiwa sana na mafundisho yako kuhusu mambo ya msingi kuzingatia ktk Uchumba.Naomba unitumie masomo haya ktk email yangu.Yameniimarisha sana.UBARIKIWE sana Mtumishi.Usiache kunitumia.

    Like

  10. Wooow!! Wonderful teachings! I like it, may I please get some more teachings and some other updates through my email address! please I mean it!.
    Stay blessed servant of God!

    Like

  11. Mungu akubarik i sana, mimi nina mchumba na tumezoea kufanya tendo la ndoa kwa muda mrefu,nifanyaje na mwakani nataka nifunge ndoa. Na kufanya tendo la ndoa na mchumba ni kosa kwa mujibu wa Mhubili 3:1.

    Like

    • Hello Mo, nina maswali kadhaa juu yako, si lazima uyajibu hapa lakini nataka nikufikirishe? je kwanza wewe na mchumba wako mmeokoka au la? Na endapo unajua kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa ni dhambi kwa nini kufanya hivyo? Umekuwa kwenye uchumba na huyo binti kwa muda gani? je kwa kipindi mlichokuwa pamoja unafikiri wewe utakuwa mume bora kwake na yeye kuwa mke bora kwako? Ubarikiwe kwa kuwa muwazi maana wapo vijana wengi ambao wanafanya hayo na wanafunga ndoa kimya kimya wakidhani Mungu hajui tena wengine wakiwa wajawazito. Ushauri wangu kwako ni huu, kama mlikuwa mmeokoka basi tubuni maana mmekuwa mkimwasi Mungu katika hili. Najua itakuwa ni vigumu sana kwenu kwa hatua mliyofikia kujizuia kufanya tendo la ndoa mpaka hiyo mwakani mtakapofunga ndoa hivyo angalieni uwezekano wa kukamilisha taratibu za ndoa yenu ikibidi mfunge mwaka huu. Na endapo unaamini huyo atakuwa ndiye mwenzi sahihi wa maisha yako ya ndoa, pia kaa na mchumba wako na mwelekeze madhara ya jambo hilo kiroho na kwenye future yenu na hivyo mjizuie kufanya tendo hilo mpaka wakati muafaka na lengo ni kuwa waaminifu kwa Mungu, naam ni lazima kuwe na mipaka kuanzia sasa na sio tena mtubu halafu muendelee na jambo hilo. Kama hujaokoka nakushauri fanya uamuzi wa kuokoka halafu tulia ndani ya Kristo uukulie kwanza wokovu mambo ya ndoa yatafuata taratibu. Kama upo huru kujibu maswali haya hapa karibu na itawasaidia wasomaji wengine kukusaidia zaidi, vinginevyo yajibu kupitia email yangu paxifari@gmail.com ili niendelee kuwasiliana na wewe zaidi.

      Like

  12. Bwana awabariki kwa somo zuri sana ambalo kwa hakika limenifungua katija vitu mbalimbali.mungu wa mbinguni awabariki.je naweza kupata contact kwa ajili ya maswali mengine.make nahitaji msaada sana wa kiroho katika hili swala la uchumba.

    Like

  13. Mungu aliyeniongoza kufungua website hii ainuliwe,na Mungu aliyekupa ufunuo wa somo hili akubariki sana kwa kuwa alikusudia ku2ponya kweli…nami hakika nimeponywa na kipengele kilichozungumzia michezo ya mapenz kwel Mungu anisamehe sana na huyu mwenzangu,2naomba maombi yak m2mishi naamin umeshapata picha ya nin kinachosumbua ujana we2 na hasa niombee nidhamu ya mahusiano,AMEN&BARIKIWA

    Like

    • Amina, utukukufu kwa BWANA Yesu, ubarikiwe kwa kuwa muwazi, maanisha mbele za Mungu juu ya toba yako, daima ninaomba kwa ajili yako na vijana wengine BWANA awawezeshe kuishi kwa nidhamu katika maisha yao ya uchumba mpaka ndoa pia. Barikiwa sana tuendelee kuombeana.

      Like

    • Utukufu kwa Mungu, ili swali kuna wakati nimeshajibu mara kadhaa huko nyuma, kimsingi kimaandiko hairuhusiwi au haikubaliki kutokana na ukweli kwamba ingawa wote tu wanadamu lakini katika ulimwengu wa roho hatufanani na hasa kwa maana ya kusudi la Mungu kwa kila mwanadamu, ila kwa mara chache sana jambo la namna hii linaweza kuruhusiwa na Mungu kwa kusudi lake maalumu kama ilivyokuwa kwa Hosea. Naam kwa hiari binafsi mtu aliyeokoka anaweza kuamua kuoa siyeokoka na kwa hali ya kibinadamu mambo yakaonekana mazuri lakini in reference to God’s purpose on that person life linakuwa ni kosa au changamoto na ndiyo maana hairuhusiwi kuoa au kuolewa na mtu asiyeokoka, si hivyo tu bali anaweza pia kukufanya ukamsahau Mungu wako kama ilivyokuwa kwa Mfalme Suleman.

      Like

  14. Nakushukuru sana ktk haya uliyoandika kwan yamenionesha njia ktk uchumba wangu. Yako ambayo nilikuwa nakosea ss nimepona kwan kila neno lenye pumzi lafaa kwa mafundisho. Mungu awe nawe ktk kufundisha umma mi binafs nimefaid sana na elimu/mafundisho yako.

    Like

  15. NILIKUA NAUULIZA KUSU KUNYWA POMBE
    biblia inasema katika 1timotheo 5:23 kua Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo kwa ajili ya magonjwa yakupatayo mara kwa mara JE, mungu anaruhusu watu kunywa pombe

    Like

  16. Je Watu Waliojihusisha Katika Tendo La Ndoa Kabla Ya Ndoa, Wakiingia Katika Ndoa Wana Nafasi Ya Kutubu? Asante Kwa Somo Zuri Mtumishi Wa Mungu Mimi Nimefunguliwa Sana!

    Like

    • Amina, pengine sijalielewa swali lako vizuri, ila ninachofikiri una maanisha hao watu walikuwa wanafanya tendo la ndoa kabla ya ndoa halali hadi walipofunga ndoa. Kama ndicho hiki una maanisha fursa ipo, hata hivyo msingi wa kutubu unaweza usionekane wazi kwa kuwa tayari hao watu sasa ni wanandoa. Hata hivyo ni muhimu wanandoa hawa wakajua kwamba walimtenda Mungu dhambi na hivyo mioyoni mwao wakamaanisha kutubia makosa waliyofanya kabla ya ndoa ili athari za makosa yao zisiendelee kuitesa ndoa yao. Baadhi ya athari kubwa zinazowatesa wanandoa waliopitia maisha ya namna hii ni kutokuaminiana na kusikia hukumu ndani yao, sambamba na kuona kama maombi yao hayasikilizwi na Mungu
      Hata hivyo kama swali lako linahusu wale ambao bado hawajafunga ndoa, msisitizo tunaotoa ni kwamba vijana wajitunze na wajizuie kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa, na kama wameshafanya kabla ya ndoa, watubie na wakusudie kutokurudia mpaka wakifunga ndoa

      Like

  17. asante kwa msaada wako mheshimiwa….Tushirikiane kuisambaza hii habari kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho…+25565577426

    Like

  18. This is good teachings. Thanks very much saints of Almighty God. I pray that may God through the name of Jesus Christ gives you more wisdom on his work. Amen

    Like

    • Mtumishi, Mungu akubariki sana uzid kutimiza kusudi lake kwa vijana..nimebarikiwa na hili somo kwan Roho Mtakatifu ameniongoza nikaona hili somo naamin litasaidia kulinda uchumba wetu..asante nimepata aman. Jina la Yesu lizidi kutukuzwa

      Like

      • Amen, BWANA Mungu alinde uchumba wenu na mkamilishe lile jema lilioanza, zingatieni hayo, hakikisha na mwenzako anapata ujumbe huu ausome pia ili kuwa na ufahamu kwa pande zote

        Like

  19. nashukuru sana mtumishi wa Mungu kwa Bwana kukuongoza vyema kuweza kutuletea somo hili ili limeze kutusaidia kwan wengine tupo katk kipndi kizito saana ambacho ni cha mateso katka uchumba naweza sema hasante sana na Mungu akubariki AMEIN.

    Like

  20. Ahsante Mtumishi Kwa Kutupatia Uzoefu Wa Suala La Mahusiano/ Uchumba. Lakini Nikuulize, Kwanini Unasisitiza Engagement Ya Labda Taratibu Za kabila, Familia, Dini, Na Koo; Wakati Maamuzi Na Malengo Ya Kuhusiana Ni Ya Wawili?.

    Like

  21. Amen….ama kwa hakika nimejifunza na nimefunguliwa kile ambacho kilikua swali katika kichwa changu. ubarikiwe na mungu mtumishi

    Like

    • Utukufu kwa Mungu kwa yote afanyayo kupitia blog hii, kukumbatiana kwa maana ya salaam si vibaya, lakini endapo mazingira ya tukio hilo kufanyika ni hatarishi basi kuna uwezekano wa kumpa ibilisi nafasi(Waefeso 4:27) ambapo vijana wanaweza kufikiri kwamba sasa unaweza hata kumbusu mwenzako, kisha kunyonyana ndimi nk. Nina wafahamu vijana wengi ambao kwao kunyonyana ndimi na kupeana mabusu katika uchumba wanaona sawa, katika hili nasema si sahihi kwani kufanya hivyo ni kuyachochea mapenzi kabla ya muda wake. Naam ni vizuri vijana watjitunze na watunze heshima ya Mungu kila mahala.

      Like

  22. Mungu awabariki na kuwarinda kwa baraka hizi za rohoni nimebarikiwa mmekuwa neema kwa utukufu mlioachilia hii in neema ya pekee

    Like

    • Naitwa Abednego nikiwa Kenya, nimesoma ujumbe huu Na nimeona ukiwa na
      mafuta ya Roho Mtakatifu ndani yake,nilicho gundua ni kwamba ndoa nyingi zimepata shida maana watu hawana mafundisho ya kutosha wakati wa uchumba wao,mfano hapa Kenya hakuna uchumba (courtship)ila watu hawa huishi alafu waoane baadaye(dating) mambo ambayo Biblia hairuhusu hata kidogo,kwa hivyo watanzania wenzangu neema ingalipo kwetu na tusiichezeshe,tuwe chini ya watumishi w Mungu na tutaonana ndoa zetu ziki prosper(kudumu)na kuinuliwa zaidi,Mungu wa amani awabariki wasomaji wote pia na mtumishi aliye funuliwa haya.

      Like

  23. tunashukuru sana Mtumishi kwa mafundisho yako mazuri kwani vijana wengi wanapotea kwa kukosa maarifa pia kukosa mafundisho ya maisha ya uchumba, inasikitisha sana kwamba hata vijana wakristo tena waliokoka nao wako kwenye hilo group la vijana wanaosema eti siwezi kununua mbuzi kwenye gunia inasikitisha sana. Tena unakutana na kijana aliyeokoka unashauriana naye kutokufanya tendo landoa lakini cha ajaabu anachojibu eti niafadhali nifanye dhambi ilimradi tuu nihakikishe ninacho kichukua kiko salama halafu baada ya hapo nitatubu, jamani jamani sisi vijana tunaelekea wapiiiiiii!!!!! tunaitwa wana wa Kristo lakini imani yetu iko wapi? kweli tunakubali kumweka Mungu pembeni halafu tunampa shetanai nafasi ya kwanza? Mungu utuhurumie sisi vijana. Mwenye sikio na asikie neno ambalo Roho wa Bwana awaambia vijana ili kulida kusudi la ndoa

    mimi nimesikia na nimejifunza mengi sana Mungu anisaidie ili niweze kumaliza kipindi hiki cha uchumba salama na mwisho Mungu ajichukulie utukufu.

    Mungu akubariki sana Mtumishi na azidi kukuinua katika utume wako ili kuwasaidia vijana kuondokana na imani potofu ya kifikra na kujua nini kusudi la Mungu ndani yao. Barikiwa sana

    Like

    • Amen Mary ubarikiwe pia kwa mchango wako muhimu, naam ni maombi yangu Mungu afungue fahamu za vijana ili waweze kujua siri hizi na kulitumikia kusudi la Mungu kwa ukamilifu.

      Like

  24. Ni somo zuri linawafaa vijanaila Kufikia hatua hiyo ni ngumu sana na inahitaji msaadaw wa Mungu tu na naweza kusema si kwa nguvu wala kwa uweza ila kwa neema zake mwenyezi
    Mungu.

    Like

  25. Maandiko yanaishi, bandiko hili lina zaidi ya miaka mitano lakini limefanyika msaada kwa wengi. Asante mtumishi kwa somo zuri, binafsi nimejifunza mengi na Mungu anisaidie nisimame katika nafasi yangu.Mungu aibariki huduma hii ili izidi kuwakomboa vijana.

    Like

  26. Nimeelewa vizuri sana watumishi wa Mungu awabariki sana.Nilikuwa na ombi he mnapatikana wap au kama kuna namba za simu ambazo tunaweza kuwapata kwa maswali zaidi

    Like

  27. Bwana YESU asifiwe sana Mtumishi.

    Binafsi namshukuru sana MUNGU,na pia nakushukuru wewe Mtumishi kwa masomo yako kuhusu Uchumba.Nilipata link yako mwaka 2012 na kusoma makala zako kuhusu uchumba.

    Napenda kukutaarifu kwamba,MUNGU mwema nimeshapata mke mwema kutoka kwa Bwana YESU,”NI MKE MWEMA SANA” namshukuru sana MUNGU.

    Namwomba MUNGU tuendelee kukua kiroho zaidi mimi na mke wangu pamoja na watoto ambao MUNGU anaendelea kutujaalia.

    “HIVYO BASI,MTUMISHI WA MUNGU,KWANGU MIMI NAOMBA UWE UNANITUMIA MASOMO YA KUISHI NDANI YA NDOA NA MAMBO MENGINE MENGI YAHUSUYO NDOA”

    Hapa kwenye Uchumba Nimevuka tayari MUNGU Mwema.

    MUNGU AKUBARIKI SANA MTUMISHI WA MUNGU SANGA.

    Like

    • Amen na utukufu kwa Yesu wetu, hakika hizi ni habari njema na zenye kujenga na kutia moyo, hongereni sana. Changamoto kwangu ni muda, lakini kwa neema ya Mungu nitajitahidi kufanyia kazi ombi lako jipya. Maombi yenu ni muhimu kwa huduma hii.

      Like

  28. Mungu akubariki sana mtumishi kwa somo zuri lenye baraka hasa kipindi hiki ambacho vijana wengi wanafuata mifumo ya kidunia kumpata mke, ni kweli kabisa ukifuata principles hizi lazima Mungu athibitike

    Like

  29. Daah namshukuru MUNGU Sana kwa mafundisho yako yamenififufua Na kunipa majibu ya maswali yote ya kiroho Na kimwili, MUNGU akubariki Sana Mtumishi

    Like

  30. Asante Mungu kwa kunifumulia kuiona hii blog..nimebarikiwa sana baba keep blessed ila ombi langu kwako sala zako kwa vijana ni muhimu mno ,ili tuweze kumtambua yupi sahihi wa kujenga nae mahusiano hadi kufunga nae ndoa .nitabarikiwa ktk hili na tumaini langu kwa Mungu litatukuka

    Like

  31. Aksanti sana ndugu kwa mafundisho haya yenye maana na ambayo niaminivyo yataokoa maisha ya vijana wengi kiafia na kiroho.
    Mimi pia ni mpastori anayehusika na huduma hiyo na nimebarikiwa vya kutosha
    Acha Mungu akuongezee hekima na maarifa pia na kukubariki.
    Rev. Olivier

    Like

  32. Nimebarikiwa sana mtumishi wa Mungu na hili somo, pia nafsi inanihukumu maana nipo kwenye mahusiano na tayari tumesha wahi kumkosea Mungu, lkn kwa mafundisho yako nahisi kama nimeamka toka usingizini. Je, tufanyeje sisi wachumba ambao tayari tulikuwa tumeshafanya uzinifu ili kutengeneza mahusiano yetu na Mungu na tuweze kuzifikia ndoto zetu za kuwa wanandoa kama tulivyoahidiana? Ushauri wako mtumishi ni wa muhimu sana kwetu. Na Mungu akubariki kwa kufumbua macho ya wengi tuliokuwa usingizini kwa habari ya mahusiano. Nimekupenda bure brother.

    Like

    • Amen Brother, utukufu kwa Yesu kwa yote atendayo kupitia masomo haya. Naam hukumu hiyo ni kwa sababu BWANA anakupenda na anataka usimame kwenye nafasi yako ili kumtumikia yeye sawasawa na kusudi lake kwako. Hivyo moja usijihukumu bali hakikisha unatengeneza na Mungu wako kwa kuanza upya. Pili endapo una uhakika huyo mwenza wako ni wa mapenzi ya Mungu basi naye anapaswa kutubu na kutengeneza na Mungu na kisha wekeni mipaka na ongezeni umakini ili msije jikuta mnarudia tena kule mlilokotoka. Mungu wa rehema na akurehemu na kukupa nafasi ya kuanza upya katika shauri lake. Kwa msaada zaidi wasiliana nami kwa namba 0755816800 siku za weekend, Jumamosi au Jumapili.

      Like

  33. Mtumishi wa Mungu ubarikiwe sana. Nimepitia andiko lako na nimeona uwepo wa Roho Mtakatifu wakati unaandika andiko hili lenye baraka sana, ubarikiwe sana mtu wa Mungu.
    kwa upendo wa Kristo naomba kutumia sehemu ya andiko hili katika kitabu changu cha masula ya ndoa kwa ajili ya kuwaelimisha wapendwa wingine juu ya maisha ya ndoa kabla na baada ya ndoa

    Like

Leave a reply to sanga Cancel reply